Tembo wavamia, waharibu mazao Mufindi
Mufindi. Taharuki imeibuka kwa Wakazi wa Kata ya Idunda Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa baada ya tembo kuvamia mashamba na kuharibu mazao mbalimbali yakiwemo mahindi, maharage, viazi pamoja na alizeti.
Akizungumza kwa njia ya simu leo ijumaa Juni 23, 2023 Diwani wa Kata hiyo Atanasi Nyigo amesema tembo hao wamevamia katika kata hiyo majira ya usiku Juni 20, 2023 na kufanya uharibifu wa mazao hayo katika maeneo yao.
"Wiki mbili nyuma tembo hawa walipita katika kata yetu lakini hawakuleta madhara yoyote kama ambavyo wamefanya safari hii wamepita na kuharibu mazao ya wananchi ambayo walikuwa wanategemea kuvuna kwa ajili ya chakula na biashara," amesema Nyigo na kuongeza kuwa;
"Tunaiomba Serikali ifikie mahali tembo hawa waweze kudhibitiwa ili kupunguza changamoto ya wananchi kuharibiwa mazao yao kwa sababu sisi tupo mbali na hifadhi.”
Ofisa Wanyamapori Wilaya ya Mufindi, Rachel John amekiri tembo hao kuvamia na kufanya uharibifu wa mazao ya Wananchi wa kata hiyo huku akisema mpaka kufikia jana tembo hao walikuwa tayari wameondoka kwenye maeneo hayo.
"Kwa sasa maofisa wetu wa kilimo na mwenyekiti wa kijiji wanafanya tathimini ya mazao kwa watu ambao mashamba yao yameharibiwa…hadi kufikia Juni 26 ndio tutakuwa na idadi kamili ya hekari zilizo haribiwa." amesema John
Pia ofisa huyo ameeleza kwamba eneo hilo ni mapito ya wanyapori kwenda hifadhi ya Mpanga Kipengere iliyopo Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe ambapo kila mwaka wanyama hao hupita maeneo hayo.
"Kwa mwaka huu tulipata changamoto kwa sababu ya simba ambao wapo Iringa hivyo askari wetu walikwenda huko, wakati leo tunajipanga kwenda tayari tembo hao wamesharudi porini." amesema ofisa huyo
John amewasihi wananchi kuchukua tahadhari ya kuvuna mapema mazao yao badala yake ya wasiyaache shambani muda mrefu ili kuepuka kupata hasara ya kuharibiwa kwa mazao yao na tembo hao.
Hata hivyo amesema kuwa wananchi wanapaswa kutumia mbinu ambazo walielekezwa kuzungushia katika mashamba yao ikiwemo kutengeneza matofali ya pilipili na uzio wa oil chafu kwa lengo la kuzuia tembo hao.