Tembo wazua kizaazaa vijiji saba Nachingwea

Muktasari:
- Wakazi wa vijiji saba wilayani Nachingwea wanaishi kwa hofu baada ya tembo kuvamia vijiji hivyo na kuharibu mazao na kujeruhi mtu mmoja.
Nachingwea. Wakazi wa vijiji saba wilayani Nachingwea wanaishi kwa hofu baada ya tembo kuvamia vijiji hivyo na kuharibu mazao na kujeruhi mtu mmoja.
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Hashimu Komba amesema tembo hao wamesababisha madhara makubwa na zimefanyika jitihada mbalimbali kuwaondoa kwa mara ya kwanza lakini wamerudi.
“Ni kweli huwa tunapata changamoto ya tembo kurudi kwenye makazi ya watu mara kwa mara hata hivyo tulishawahi kupokea taarifa ya kuonekana kwa wanyamapori hao katika vijiji mbalimbali kikiwemo cha Ilolo, Nyambi B, Ndangambo, Mbute, Nanjili na Namatekwe."
“Maofisa wetu wa idara ya wanyamapori walichukua hatua na kuanza kuwahamisha wanyama hao kutoka kwenye makazi ya watu lakini tuliongezewa nguvu kutoka Seluu walituletea askari watano.”
Katika ufafanuzi wake amesema, “unajua tembo wanapoondoka huwa wana desturi ya kurudi, sasa wamerudi mara ya pili wamesababisha madhara kwenye mazao na kujeruhi mtu mmoja ambaye anadaiwa kufariki.”
“Unajua uwepo wa wanyama hao ni matokeo ya uhifadhi mzuri wa mazingira na udhibiti wa majangili hii ndio inapelekea kutawanyika katika maeneo mengi."