TFS kuboresha hifadhi ya msitu Rau

Muktasari:

  • Msitu huo wenye ukubwa wa Hekta 584, upo kilometa tatu kutoka mjini Moshi, na hutembelewa na watalii zaidi ya 4,000 kwa mwaka, maboresho hayo yanalenda kuongeza idadi ya watalii hifadhini hapo.

Moshi. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Moshi, kujenga mahema yatakayotumiwa kwaajili ya kulala watalii katika Hifadhi ya Msitu wa Rau, hatua ambayo inatajwa itachochea ongezeko la watalii katika hifadhi hiyo.

 Hayo yamebainishwa na Mhifadhi wa TFS Wilaya ya Moshi, Zayana Mrisho wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea msitu huo, ulipo kilometa tatu kutoka Moshi mjini huku ukipokea watalii Zaidi 4,000 kwa mwaka.

“…licha idadi ya watalii inaongezeka kila mwaka, bado kunahitajika mwamko zaidi kwa watalii wa ndani, sasa ujenzi wa makambi haya, utachochea kuongezeka kwa watalii kwani watapana tafasi nzuri kwa malazi na chakula,” amesema.

Amesema moja ya jitihada ambazo wanazifanya ni kuweka makambi na kutenga maeneo kwa ajili ya nyama choma pori pamoja na kuanzisha mashindano ya baiskeli kupitia njia zilizopo ndani ya hifadhi hiyo.

Amesema pia kutakuwa na mahema ambayo yatawezesha watalii wanaohitaji kupumzika kwa siku kadhaa ndani ya msitu na kufurahia mandhari ya msitu huo.

Aidha amesema katika mapumziko ya wiki, vikundi vitapewa ridhaa ya kufanya mchakamchaka wa asubuhi au jioni kama njia ya mazoezi, lakini pia kupitia njia zilizopo ndani ya hifadhi watu wataweza kutengeneza ruti ya mashindano ya kukimbia na hata ya baskeli ili kuondoa msongamano katikati ya mji lakini pia kupata hewa ni safi.

“Jitihada mbalimbali zinafanyika ili kuhamasisha na kukuza utalii wa ndani katika msitu wa hifadhi wa Rau na moja ya jitihada hizo ni ujenzi wa makambi  ambayo yanatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha ujao,” amefafanua na kuongeza;

“Baada ya kukamilika kwa makambi hayo, kutakuwepo na michezo mbalimbali ikiwemo michezo ya watoto, nyama choma pori, na vikundi mbalimbali vya vijana vitakuwa vinatumbuiza ndani ya msitu hatua ambayo itavutia watalii wengi Zaidi.”

Mhifadhi huyo ameeleza kuwa: “Pia kutakuwa na michezo ya mbio na hata michezo ya baiskeli na watu wengi wataingia kwa ajili ya kufurahia mambo mbalimbali yaliyopo ikiwa ni pamoja na mandhari mazuri ndani ya msitu”

Kwa upande wake, Msimamizi wa Msitu huo, Devotha Mushi amesema: "Msitu huu ni wa kipekee ambao tunauita ‘Mapafu ya Mji wa Moshi,’ kwasababu unaboresha hali ya hewa ya Moshi kwa kufyonza hewa ya kaboni lakini pia  unahifadhi ardhi kutokana na miti iliyopo na unatunza vyanzo vya maji ambayo hutumika majumbani na mashambani."

Naye Afisa utalii katika hifadhi hiyo, Joseph Ally alisema Watalii wanaotembelea hifadhi hiyo, wameendelea kuongezeka kila mwaka ambapo toka Machi 2022 hadi Machi mwaka huu, watalii zaidi ya 4,000 walitembelea hifadhi hiyo.

"Hifadhi hii ina madhari yanayovutia na kuna wanyama mbalimbali na mti mkubwa wa Mvule na ambao mkongwe Afrika Mashariki ‘Mvule wa Maajabu,’ lakini pia kuna miti ambayo huwezi kuipata ukanda wowote wa Afrika Mashariki lakini hapa utaukuta," amesema na kuongeza.

"Nitoe wito kwa watalii wa ndani na nje kutembelea hifadhi hii ya mazingira asilia, ili kuweza kupata mawazo mapya na kujionea uumbaji wa Mungu na mazingira mazuri yenye kuvutia na hewa safi."