TFS yaomba radhi abiria, Watanzania

Muktasari:
- Taarifa iliyotolewa leo Jumapili na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imezungumzia tukio la mtumishi wake kukiuka maadili ya kazi kwa kutoa lugha zisizo na staha wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi na kuahidi kuchukua hatua zaidi
Dar es Salaam. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imemwomba radhi abiria aliyekuwa akisafirisha vitanda na Watanzania kwa tukio la mtumishi wake kutoa lugha zisizo na staha zinazokiuka maadili ya utumishi wa umma.
TFS imefikia hatua ya kuomba radhi baada ya kusambaa kipande cha video mitandaoni kikionyesha mtumishi wake akikagua vitanda vilivyokuwa vimebebwa na moja ya basi na kusababisha adha kwa abiria wengine na mwenye kitanda.
Taarifa iliyotolewa leo Jumapili Desemba 30, 2018 na kitengo cha habari ya mawasiliano Serikalini imesema vitanda vilivyokuwa vikisafirishwa na abiria vililipiwa ushuru wa Serikali kupitia mfumo wa kielektroniki wa Malipo ya Serikalini (GePG) Desemba 26, 2018.
TFS imeomba radhi kwa abiria huyo na umma wa Watanzania kwa tukio hilo na usumbufu uliojitokeza na kutoa onyo kwa watumishi wa umma kuzingatia maadili ya kazi
“Wakala unaendelea kufuatilia suala hili na utahakikisha tukio kama hili halijirudii tena. Aidha, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma dhidi ya mtumishi aliyehusika na utoaji wa lugha isiyo na staha wakati akitekeleza sheria ya misitu ambapo alitegemewa kutoa elimu stahiki kwa umma,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika taarifa hiyo, imeelezwa kuwa ofisa misitu wa wilaya ya Korogwe alikuwa akitekeleza majukumu ya kusimamia Sheria ya Misitu Na. 14 ya Mwaka 2002 pamoja na Kanuni zake za Mwaka 2004.
“Ofisa huyo alikuwa akitekeleza majukumu hayo kwa mujibu wa kifungu cha 93 (Powers of officers with respect to offences) inayompa mamlaka ofisa misitu au ofisa wa Jeshi la Polisi kukagua, kukamata na kuzuia mazao yanayodhaniwa kupatikana kinyume na sheria,” imeeleza taarifa hiyo.
“Katika kutekeleza majukumu yake, ofisa wetu alimtaka abiria huyo kuonyesha hati ya kusafirishia (Transit Pass) bidhaa hizo kwa mujibu wa kanuni za misitu kifungu cha 13, sehemu ndogo ya 4 ambayo inakataza mwenye chombo chochote cha usafiri kusafirisha mazao ya misitu ambayo hayana hati ya usafirishaji ambapo abiria huyo hakuwa nayo.”
“Hata hivyo, ofisa wetu alishindwa kutafsiri masharti ya kifungu hiki na mahitaji ya utoaji wa hati ya usafirishaji kwani kama msafirishaji binafsi kwa matumizi ya nyumbani asingeweza kukidhi vigezo vya kuwa na hati hiyo,” imesema na kuongeza.
“Hati ya usafirishaji huhitaji msafirishaji kuonyesha usajili, leseni ya biashara, utambulisho wa mlipa kodi na namba ya usajili wa chombo kinachotumika kusafirisha mazao hayo pamoja na kuonyesha vituo atakavyopaswa kukaguliwa.”
Hata hivyo, TFS imetoa mwongozo kuhusu usafirishaji wa samani kutoka kwa watengenezaji au wauzaji mahali popote kuhakikisha mhusika anapatiwa risiti halali kwa malipo aliyofanya.
Hivyo, mmiliki wa samani mpya kwa matumizi binafsi halazimiki kuwa na Hati ya Usafirishaji anaposafirisha toka eneo moja kwenda jingine isipokuwa awe tayari kuonyesha uthibitisho wa nyaraka za malipo halali ya samani hizo kwa ukaguzi pale itakapohitajika.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa yeyote anayesafirisha samani zilizotumika kutoka eneo moja hadi jingine halazimiki kuwa na hati za malipo wala kuwa na hati ya kusafirishia samani hizo.
“Serikali itaendelea kufanya mapitio ya sheria ya misitu na kanuni zake ili kuepuka mkanganyiko wowote wa tafsiri ya sheria unaoweza kujitokeza na kuondoa usumbufu kwa wananchi.”