Tira, BoT wavutiwa na huduma mpya ya bima benki ya Exim

Sunday November 07 2021
New Content Item (1)

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Jafari Matundu alisema katika kufanikisha huduma hiyo benki hiyo tayari imekwisha waandaa vema baadhi ya wafanyakazi wake mahususi kwa ajili ya kutoa huduma kwa kushirikiana na kampuni za Bima 10 ambazo zinashirikiana na benki hiyo kuendesha huduma hiyo.

By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Nchini (Tira) pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zimeunga mkono ushirikiano unaoshuhudiwa hivi sasa baina ya taasisi za kifedha pamoja na makampuni ya bima nchini katika kutoa huduma mbalimbali za kibima huku zikionesha kuvutiwa  na huduma mpya ya bima ijulikanayo kama "Bima Tu, Malipo Tuachie” inayotolewa kupitia benki ya Exim Tanzania.

Wakizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa huduma hiyo ya "Bima Tu, Malipo Tuachie”, iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Meneja wa Leseni na Usimamizi wa mwenendo wa soko wa Tira, Hillard Maskini pamoja nae Meneja wa Usimamizi wa Taasisi za Fedha wa BoT, Nassor Omary walisema ushirikiano huo pamoja na mambo mengine utaongeza wigo wa kuwafikia wateja na wanachi kwa ujumla na hivyo kukuza sekta ya bima  sambamba na kuboresha huduma za kibenki nchini.

Katika kutekeleza huduma hiyo mpya  benki ya Exim imeshirikiana na kampuni 10 kubwa za bima nchini ili kuwaletea wateja wake huduma bora za Bima zikiwemo, Bima ya Afya, Bima ya safari na Bima ya Maisha ambazo zote zitatolewa pamoja chini ya benki hiyo.

“Ushirikiano huu unaoendelea hivi sasa ni hatua nzuri zaidi kufikiwa katika historia ya utoaji wa huduma za kibima nchini. Ndio maana sisi kama wadau na wasimamizi wakubwa wa sekta hii ya Bima tunazipongeza sana taasisi za kifedha ikiwemo benki ya Exim kwa kuendelea kutuunga mkono kwa kuwa kupitia ushirikiano kama huu utasaidia kuongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma za kibima nchini,’’ alisema  Maskini aliyemuwakilisha Kamishna wa Tira,  Mussa Juma

New Content Item (1)

Meneja wa Leseni na Usimamizi wa mwenendo wa soko wa TIRA Hillard Maskini akizungumza kwenye hafla hiyo.

Alisema nia ya serikali kwa sasa ni kuongeza wigo wa mtandao wa utoaji huduma za bima kwa jamii ya watanzania ambao kwa sasa ni asilimia 28.6 tu ndio waliofikiwa na huduma hiyo.

Advertisement

“Hivyo basi nadiliki kusema kwamba  "Bima Tu, Malipo Tuachie” ni huduma inayoshabihiana na azma ya serikali ya kupanua ushiriki wa wananchi wengi zaidi katika huduma za bima. Zaidi naamini kupitia huduma hii tutafanikiwa kuvutia watanzania wengi kujiunga na huduma za bima kwa kuwa sasa hawatahofia suala malipo ya mkupuo kwa kuwa Exim mpo kazini leo kwa ajili ya kesho yao.’’ Alisema.

Kwa upande wake  Nassor pamoja na kupongeza ushirikiano huo, alisema BoT imekuwa ikiunga mkono huduma za Bima kupitia mabenki yaani Bancassurance kwa kuwa pia inaongeza tija kwa taasisi hizo katika kuwahudumia wananchi.

“Ongezeko la watumiaji wa huduma za Bima nchini kupitia katika taasisi za kifedha, pamoja na faida nyingine za moja kwa moja kwa wananchi wenyewe pia ni faida kwa wadau yaani mabenki, mashirika ya bima na serikali. Na hiyo ndio sababu BOT tumekuwa tukivutiwa na ushirikiano wa aina hii.  Hiki tunachokishuhudia leo kinatupa faraja na matumaini makubwa sana...hongereni sana,’’ alisema Nassor aliyemuwakilisha Naibu Gavana wa BoT Dk. Bernard Kibesse

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Jafari Matundu alisema katika kufanikisha huduma hiyo benki hiyo tayari imekwisha waandaa vema baadhi ya wafanyakazi wake mahususi kwa ajili ya kutoa huduma kwa kushirikiana na kampuni za bima 10 ambazo zinashirikiana na benki hiyo kuendesha huduma hiyo.

“Si tu kwamba wafanyakazi wetu wamepatiwa mafunzo mahususi kufanikisha mpango huu bali pia wameidhinishwa na mamlaka husika kuwa wameiva katika kuwasaidia wateja wetu hususani katika utoaji wa elimu kuhusu huduma za bima wanazohitaji...kwa hiyo tumejipanga haswa,’’ alisisitiza.

Akifafanua zaidi kuhusu huduma hiyo Mkuu wa Kitengo cha huduma za Bima kwa mabenki wa benki hiyo, Melchizedeck Muro, alisema kupitia huduma hiyo benki ya Exim itatoa mikopo itakayowawezesha malipo ya huduma za bima za aina mbalimbali kupitia Kampuni 10 za bima zinazoshirikiana na benki hiyo na wakopaji wataendelea kulipa taratibu mkopo huku wakiendelea kunufaika na bima hizo.

New Content Item (1)

Katika kutekeleza huduma hiyo mpya benki ya Exim imeshirikiana na kampuni 10 kubwa za bima nchini ili kuwaletea wateja wake huduma bora za Bima zikiwemo, Bima ya Afya, Bima ya safari na Bima ya Maisha ambazo zote zitatolewa pamoja chini ya benki hiyo.

“Hiyo ndio sababu tukaamua kusema "Bima Tu, Malipo Tuachie”. alisema  Muro huku akiyataja makampuni ambayo yanashirikiana na Exim kutoa huduma hiyo kuwa ni Jubilee Insurance, Fist Assurance, Heritage Insurance, GA Insurance, Alliance Life Assurance na Britam Insurance.

Mengine ni UAP Insurance, ICEA Lion General Insurance, Strategies Insurance, na Alliance Insurance corporation.

 Zaidi Muro alibainisha kuwa katika utoaji wa huduma hiyo Benki hiyo imejipanga kuhakikisha kwamba inatoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu huduma za bima ili kuondoa changamoto zinazotokana na ukosefu wa elimu hiyo miongoni mwa wateja wao.

Hafla hiyo ilihudhuliwa pia na wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa makampuni ya Bima yanayoshiriki katika kufanikisha huduma hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Kampuni ya Bima nchini (ATI), Khamis Selemani wateja pamoja wafanyakazi wa benki hiyo.

Advertisement