TMA yawatahadharisha wakulima viazi mabadiliko tabianchi
Muktasari:
- Ongezeko la joto nchini limeleezwa kupunguza uzalishaji wa zao la viazi mviringo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa kipindi cha miaka ishirini ijayo kutokana na mabadiliko ya tabianchi hususan mvua chache na ukame.
Mbeya. Ongezeko la joto nchini limeleezwa kupunguza uzalishaji wa zao la viazi mviringo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa kipindi cha miaka ishirini ijayo kutokana na mabadiliko ya tabianchi hususan mvua chache na ukame.
Meneja wa Huduma za Hali Hewa ya Kilimo kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Isack Yonah amesema leo Jumatano, Juni 8, 2022 mkoani hapa kwenye kikao kilichohusisha wadau wa kilimo, makampuni ya pembejeo, watafiti na maofisa kilimo kilichoratibiwa na Mradi wa Craft kwa udhamini wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi.
Yonah amesema kuwa mabadiliko ya tabianchi yataleta athari kubwa ya uzalishaji kwa kipindi cha miaka ishirini ijayo. Hivyo ni vyema watafiti, maofisa kilimo na wadau kushirikiana ili kusaidia wakulima kuzalisha mazao mbadala tofauti na viazi mviringo
''Kikao hiki kitatoka na majibu ya nini kifanyike katika kusaidia Serikali na wakulima wanaozalisha mazao ya kilimo cha biashara kwa kutoa elimu ya kilimo mbadala ili kuwaepusha na hasara kutokana na mabadiliko ya tabia nchi,'' amesema.
Ameongeza kuwa TMA imekuwa ikifanya utabiri wa mara kwa mara kuangalia hali ya kilimo na mazao kwa miaka ijayo hivyo ni wakati kwa wakulima kubadilishwa kimtazamo mapema kabla athari kujitokeza kwa kuzalisha mazao yanayo himili ukame.
Ofisa Kilimo Mwandamizi kupitia Mradi Craft wa kilimo himilivu cha mazao, Godyfrey Kabuka amesema wamelazimika kukutana na wadau hususan wakulima lengo la kutoa elimu ya athari ya mabadiliko ya hali ya hewa katika uzalishaji na kutoa fursa za kilimo mbadala kinacho himili ukame
Amesema mradi huo unatekelezwa kwa miaka mitano ambao unawakutanisha wadau kueleza mabadiliko kwenye sekta ya kilimo na kutoa elimu ya athari katika uzalishaji wa viazi mviringo na kutoa fursa zilizopo kwenye mnyororo wa thamani
''Nishauri watafiti kuja na mpango wa mbegu bora ambazo zitastahili ukame lengo likiwa ni kuwawezesha wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuzalisha mazao yanayokabiliana na ukame,''amesema.
Mkulima wa viazi, Stella Mwamakula amesema upungufu wa mvua umeathiri uzalishaji katika baadhi ha maeneo nchini ikiwa ni pamoja na gharama za mbolea kutoka Sh40,000 mpaka 120,000 na kwamba hali ya kupungua kwa uzalishaji kuna wakatisha tamaa na kuomba elimu ya kilimo mbadala kipewe kipaumbele.