TMDA yalia na uuzaji holela wa dawa

Meneja wa TMDA Kanda ya Kusini Dkt. Engelbert Mbekenga(wapili kulia) akizungumza jambo katika ukaguzi wa maduka ya dawa ukifanyika Wilaya ya Newala. Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

  • TMDA Kanda ya Kusini imeeleza kusikitishwa na uuzwaji holela wa dawa zisizoruhusiwa kwenye maduka ya dawa, huku wauzaji wa dawa hizo wakiwa hawana sifa za kufanyakazi katika maduka hayo.

Mtwara. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Kusini imewaonya wamiliki wa maduka ya dawa wanaotoa huduma zisizo rasmi kinyume na utaratibu ikiwemo kuchoma sindano na kuuza dawa zisizoruhusiwa kuuzwa kwa ngazi husika na kuwa na watumishi wasio na sifa.

Akizungumza ofisini kwake leo Machi 23 baada ya kufanya ukaguzi huo katika baadhi ya wilaya za Mkoa wa Mtwara, Meneja wa TMDA Kanda ya Kusini, Dk Engelbert Mbekenga amesema kuwa ukaguzi huo ubaini matendo maovu ya watoa huduma.

Amesema kuwa ukaguzi huo umekwenda sambamba na utoaji wa elimu kwa ngazi ya hospitali, vituo vya afya, zahanati na maduka ya dawa.

Dk Mbekenga amesema kuwa wapo watoa huduma wasio na sifa wanaotumika kuuza madawa kwa watu jambo ambalo sio sahihi sambamba na uuzaji holela wa dawa katika maduka ya dawa muhimu.

 “Muda mwingine wamiliki wanachangia kwa nia ya kutaka kupata faida kama kutoa huduma ya kuchoma sindano, kuuza dawa zisizotakiwa katika ngazi ya maduka ya dawa muhimu hili hatukubaliani nalo.

 “Nawaomba wamiliki na watoa huduma kutoa ushirikiano wakati wote wa ukaguzi, ukaguzi ni njia ya kuboresha huduma katika sekta ya afya,” amesema.

Naye Ofisa Elimu kwa umma na huduma kwa wateja wa TMDA Kanda ya Kusini, Hussein Makame amesema utoaji wa elimu kwa jamii juu ya dawa, vifaa tiba na vitenganishi ni muhimu.