TMDA yaonya matumizi holela dawa ya Vega
Mkaguzi wa Dawa TMDA Kanda ya Kusini, Elias Magambo akiwa ameshika dawa ijulikanayo kama Vega ambayo imekuwa ikitumiwa na vijana kwaajili ya kuongeza nguvu za kiume. Picha na Florence Sanawa.
Muktasari:
- Vidonge vya Vega 100mg vina kiuongo cha Sildenafi kinachotibu tatizo la uume kutosimama kwa kuongeza mtiririko wa damu kwenye uume.
Lindi. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Kusini imeonya matumizi ya dawa ya kuongeza nguvu za kiume aina ya Vega bila kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, kwani watumiaji wanaweza kushindwa kabisa kushiriki tendo la ndoa.
Kwa mujibu wa mtandao wa Yebi Health, vidonge vya Vega 100mg vina kiuongo cha Sildenafi kinachotibu tatizo la uume kutosimama kwa kuongeza mtiririko wa damu kwenye uume.
Akizungumza na Mwananchi jana Agosti 4 katika banda la TMDA katika maonyesho ya kilimo Nanenane mkoani hapa, Mkaguzi wa dawa Kanda ya Kusini, Elias Magambo alisema kuwa matumizi ya dawa hiyo yanaongezeka kwa kasi bila hali inayoweza kuchangia vijana hao kutokuwa na nguvu kabisa.
“Hii dawa maarufu kama Vega imekuwa ikitumiwa na wanaume hasa vijana wadogo kwa ajili ya kuongeza nguvu za kiume wakidai kuwa wanakwenda kuwakomesha wanawake, lakini inaweza kuwa ni hatari,” amesema.
Amesema kama dawa hiyo isipotumiwa kwa uangalifu inaweza kusababishia matatizo ya baadaye kwa watumiaji kushindwa kushiriki tendo la ndoa na hivyo wataendelea kuitumia kila watakapotaka kukutana na wenzi wao.
Mbali na matumizi ya kuongeza nguvu za kiume, Magambo alibainisha kuwa dawa hiyo pia hutumiwa na watu wenye shinikizo la damu.
“Nitoe wito kwa vijana kuacha kutumia dawa hii kwa kuwa madhara yake ni makubwa hivyo ni vema kuanza kufanya mazoezi na kubadilisha mfumo wa maisha ikiwemo matumizi na aina vyakula,” amesema Magambo.
Kwa upande wake Abdallah Juma mkazi wa Lindi mjini amesema kuwa serikali ione umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii kwakutumia njia mbalimbali ili kusitisha matumizi ya dawa hiyo ambayo inaathari kubwa kwa jamii yetu.
"Kwanza kwanini utumie dawa za kuongeza nguvu ina maana hujiamini hii sio sawa tunadhani tunawakomoa wanawake lakini kumbe starehe ya siku moja inaweka madhara kwa muda mrefu zaidi hivyo kukufanya ushindwe kabisa.
Naye Amina Hussein binti mkazi wa Lindi amesema kuwa wanaume wengi wamekuwa na tabia hiyo ya kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume nao wanaona kama desturi.
“Wengi hufanya hivyo kama kutukomoa na wakiona sifa sisi kuwasifia bila kujali afya zao jambo ambalo linaweza kusababisha tukapoteza wanaume wanaojiamini ndani ya nyumba,” amesema Amina.