TMDA yawakumbuka wafungwa, mahabusu mkoani Mara
Muktasari:
- Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki imetoa msaada wa dawa za kutibu binadamu za Sh23 milioni kwa ajili ya zahanati zilizo chini ya Jeshi la Magereza Mkoa wa Mara.
Musoma. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki imetoa msaada wa dawa za kutibu binadamu za Sh23 milioni kwa ajili ya zahanati zilizo chini ya Jeshi la Magereza Mkoa wa Mara.
Msaada huo umekabidhiwa mjini Musoma leo Ijumaa Juni 24, 2022 na meneja wa kanda hiyo, Sophia Mziray ikielezwa kuwa kuna uhitaji wa dawa kwa ajili ya kutibu wafungwa na mahabusu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, meneja huyo amesema ofisi yake ilibaini uhitaji ya dawa baada ya kufanya ziara katika mkoa wa Mara kwa jili ya kampeni ya kutokomeza matumizi ya bidhaa za tumbaku mkoani humo.
"Dawa hizi ni kwa ajili ya kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu na tunaamini zitasaidia kupunguza upungufu wa dawa kwenye zahanati za Magereza hivyo kuoboresha huduma zitolewazo kwa wafungwa na mahabusu pamoja na watumiaji wengine" amesema
Mganga mkuu wa mkoa wa Mara, Dk Juma Mfanga ameutaka uongozi wa Magereza kuhakikisha dawa hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa huku akiahidi kuendelea kuwasiliana na TMDA ili kuleta msaada wa aina hiyo kadri itakavyowezekana.
" Kawwida dawa za serikali zinakuwa na nembo maalum lakini kwa hapa najua TMDA hawajaweka nembo, sasa hali hiyo isitumike kama kigezo cha dawa hizi kupelekwa kwingine ikiwepo kwenye maduka kwa ajili ya kuuzwa isipokuwa ni kwa ajili ya matumizi ya magereza kama ilivyokusudiwa," amesema
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mara, Hospitius Mendi mbali na kushukuru kwa msaada huo ameiomba taasisi hiyo kuendelea kutoa msaada wa aina hiyo kwani mahitaji ya dawa ni makubwa tofauti na hali halisi ingawa hakutoa takwimu.
Amesema dawa hizo zitapelekwa kwenye zahanati sita za magereza zilizopo mkoani Mara na kuahidi kuwa zitatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa.
" Serikali huwa inaleta dawa kwa zahanati zetu kama kawaida lakini kama mnavyojua mahitaji yapo kila siku hivyo ushiriki wa waduu wengine ni muhimu ili kuboresha zaidi huduma zetu kwa ustawi wa jamii yetu," amesema Mendi.