TMF yatumia Sh30 bilioni kuimarisha tasnia ya habari

Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Muktasari:
Kiasi hicho ni tangu mwaka 2008 ambapo kimetolewa kwa awamu tofauti lengo likiwa kukuza tasnia ya habari nchini.
Dar es Salaam. Mfuko wa Habari Tanzania (TMF) umetumia kiasi cha dola 17.7 milioni za Marekani sawa na Sh38 bilioni katika kuwawezesha waandishi wa habari nchini kuandika habari mbalimbali zikiwepo za uchunguzi na habari za vijijini.
Kiasi hicho ni tangu mwaka 2008 ambapo kimetolewa kwa awamu tofauti lengo likiwa kukuza tasnia ya habari nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2008, mfuko huo umetoa misaada ya kuwawezesha waandishi wa habari zaidi ya 570, na zaidi ya taasisi za habari 120.
Sungura pia amesema baada ya mafanikio hayo ya awamu mbili, Septemba 22, ndiyo utakuwa mwisho wa awamu ya pili na kuja na ya tatu ambayo itakuwa chini ya Watanzania na jina litabadilika na kutambulika kama Tanzania Media Foundation.
Amesema TMF mpya itaanza kazi kwa kukutana na wadau mbalimbali wa habari nchi nzima, na kufanya nao kazi ili kubaini habari ambazo zitaleta mabadiliko chanya kwa taifa.
“Kuna vyombo vya habari vimefanya kazi nzuri na yenye weledi mkubwa kwa kuandika habari za uchunguzi za kina kama tulivyokubaliana, lakini kuna ambavyo hatutafanya nao kazi tena kutokana na kukiuka makubaliano na kutofanya kazi kama walivyoaihidi” amesema Sungura.