TPA yataja sababu za kulalamikiwa, yawagusa wateja

Muktasari:

  • Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekiri bado kuna malalamiko yanayotokana na usumbufu kwa wateja wao wakati wa kuchukua au kusafirisha mizigo kutoka kwa baadhi ya vitengo vyao.

Dodoma. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imekiri bado kuna malalamiko yanayotokana na usumbufu kwa wateja wao wakati wa kuchukua au kusafirisha mizigo kutoka kwa baadhi ya vitengo vyao.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi, Agosti 13,2022 na Mkurugenzi wa Mipango, Ubora na Udhibiti wa TPA, Dk Boniface Nobeji wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa shughuli za bandari kwa mwaka 2020/21 na mwelekeo wao kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Hata hivyo, Dk Nobeji amesema si kila lalamiko linasababishwa na watendaji au watumishi wa mamlaka hiyo bali kuna taasisi zingine na wakati mwingine wateja wenyewe kwa kutokukamilisha baadhi ya nyaraka ili mtu aweze kuchukua mzigo wake.

Dk Nobeji amesema mamlaka hiyo ina mtandao mpana na ndani yake kuna taasisi 34 hivyo wanabeba changamoto nyingi za wadau kwa hiyo kuna baadhi ya maeneo yawezekana kuwa wao lakini pengine kuna haja ya kuangalia na upande wa wanaohudumiwa.

“Hilo la malalamiko hatukatai, lakini linapaswa kuangaliwa na upande wa pili kwa tunaowahudumia nao kuona kuna nini.”

“Wakati mwingine sisi tunatimiza wajibu wetu lakini mtu anakuja hana nyaraka na mzigo umeshakaa siku nyingi kwa hiyo lazima tujiridhishe kwanza,” amesema Dk Nobeji.

Kuhusu mafanikio amesema kwa mara ya kwanza katika mwaka wa fedha uliopita TPA imefanikiwa kukusanya Sh1 trilioni licha ya muda mrefu kuwa na lengo hilo lakini hawakufikia na kwa mwaka huu wa fedha wanalenga kukusanya Sh1.2 trilioni.

Kingine wamefanikiwa kuwa na ulinzi na usimamizi mzuri wa mizigo ya wateja wao kutoka nchi tano ambazo zinahudumia na bandari za Tanzania huku akieleza wamerasimisha bandari 20 katika maeneo mbalimbali ambapo sasa zinachangia kwenye usafirishaji wa mizigo kwa halali.

Ametaja kwa mwaka uliopita walitoa huduma ya mizigo kwa tani 20 milioni, makasha 823,000, shehena ya magari ilifikia 203,932 ikiwemo meli kubwa ya magari iliyokuwa na magari zaidi ya 4000 lakini akazitaja bandari za Mtwara na Mwanza kwamba zimekuwa zikifanya vizuri na kuongeza shehena za mizigo.