TPDC kuongeza uzalishaji wa gesi

Muktasari:

  • Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linatarajia kujenga bomba lenye urefu wa mita 35 kwaajili ya kusafirishia gesi kutoka Kijiji cha Ntoria, Kata ya Nangurwe kwenda  katika kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo Madimba mkoani Mtwara.

Mtwara. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linatarajia kujenga bomba lenye urefu wa mita 35 kwaajili ya kusafirishia gesi kutoka Kijiji cha Ntoria, Kata ya Nangurwe kwenda  katika kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo Madimba mkoani Mtwara.

Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli, Tanzania (TPDC)  Dk James Mataragio wakati wa ziara ya Bodi ya Wakurugenzi wa TPDC katika kituo cha utafiti wa gesi na mafuta cha Ntoria alisema kuwa, wanatarajia kuongeza uzalishaji hadi kufikia futi za ujazo 140 kwa siku kutoka futi za ujazo 60 zilizokuwa zikizalishwa awali.

Alisema kuwa kituo hicho kimefanya tafiti na ugunduzi ambapo wapo katika hatua za kuendeleza eneo  ambapo miezi 18 ijayo gesi itaanza kuzalishwa katika eneo hilo.

 “Mpaka sasa tunayo gesi yenye futi za ujazo trilioni 57.54 ambayo iko baharini na tunayo zaidi ya futi za ujazo trilioni 40 na trilioni 10 ziko nchi kavu tumetumia futi za ujazo trilioni moja tu mpaka sasa ambayo nchi kavu pekee.

“Unajua hii gesi ikishazalishwa lazima isafiswe ndio maana tumefikiria bomba tunaanza kuivuna siku siyo nyingi kwa sasa tunachukua data za mitetemo ambapo zitatupa maeneo ambayo tutafanya uchorongaji mkubwa nia ni kuongeza gesi ili tuzalishe kwa wingi zaidi,” alisema Dk Mataragio.

Naye Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa TPDC Balozi Ombeni Sefue alisema kuwa wamefanya ziara katika maeneo hayo ili kuweza kuona kazi zinazofanywa na taasisi hiyo inayojihusisha na gesi na mafuta.

Kwa sasa Soko duniani la mafuta ni zuri hata wawekezaji wanaonyesha nia ya kuwekeza  na serikali inafanya majadiliano tunapoona tafiti zikiendelea na uchimbaji ukifanyika kwetu ni faida kubwa na nchi kwa ujumla,” alisema Balozi Sefue.