TPDC: Wenye magari kaeni mkao wa kula matumizi ya gesi

Saturday November 28 2020
magaripic
By Sada Amir

Mwanza. Manufaa ya uwepo wa utajiri wa gesi asilia nchini Tanzania utaanza kuonekana kwa wamiliki wa magari ambao watapunguza gharama za matumizi ya mafuta pindi mradi wa kutumia gesi kwenye magari unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Petroli nchini (TPDC) utakapoanza.

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC), Dk James Matarajio amewaambia waandishi wa habari jijini Mwanza kuwa katika hatua ya kwanza, mradi huo utaanza na magari 500 jijini Dar es Salaam kabla ya kusambazwa maeneo mengine nchini.

Dk Matarajio anayehudhuria mkutano mkuu wa Jumuiya ya Wajiolojia (TGS) unaoendelea jijini Mwanza amesema TPDC inajenga vituo vitano jijini Dar es Salaam vitakavyotumika kushindilia gesi kwenye magari.

Baadhi ya vituo hivyo vitakuwa maeneo ya Muhimbili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Feri na Kibaha kwa mkoa wa Pwani.

Kuhusu bomba la gesi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, Dk Matarajio amesema huduma hiyo ambayo tayari inatolewa jijini Dar es Salaam inatarajiwa kusambazwa kwenye mikoa mengine ya Dodoma, Tanga, Morogoro na Mwanza hadi nchi jirani za Kenya na Uganda.

“Matumizi ya gesi inapunguza gharama za nishati majumbani kwa karibia asilimia 40; ni lengo la TPDC kuona Watanzania wengi wanafikiwa na huduma hii,” amesema Dk Matarajio

Advertisement

Ili kufanikisha lengo hilo, mtendaji mkuu huyo wa TPDC amesema shirika hilo limeongeza uzalishaji wa gesi kwa asilimia 140 kutoka futi za ujazo 160 milioni mwaka 2014 hadi kufikia futi za ujazo 288 milioni mwaka 2020.


Advertisement