TRA yapendekeza somo la kodi kufundishwa shuleni

Muktasari:

Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) imependekeza kwa Kamati ya Taifa ya Uboreshaji wa Mitaala inayoongozwa na Profesa Makenya Maboko kufundishwa kwa somo la kodi kuanzia shule ya msingi ili kujenga utamaduni wa kupenda kulipa kodi.

Dodoma. Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imependekeza kwa kamati ya Taifa ya Uboreshaji wa Mitaala inayoongozwa na Profesa Makenya Maboko kufundishwa kwa somo la kodi kuanzia shule ya msingi ili kujenga utamaduni wa kupenda kulipa kodi.

 Hayo yamesemwa leo Jumapili Septemba 25, 2022 na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu ya Mlipakodi, Richard Kayombo wakati akizungumza na Mwananchi Digital.

Amesema kwa kuwa elimu imekuwa bure wanaamini kwa kutoa elimu hiyo kuanzia ngazi ya chekechea kutawezesha wananchi wote kuguswa na elimu ya mlipakodi na hivyo kujenga utamaduni na uzalendo wa kulipa kodi.

“Wataelewa vyanzo vya mapato vinatokana na kodi wanayolipa ambayo inatumika kujenga miundombinu ya barabara na mingine. Wataelewa pia kulipa kodi si adhabu,”amesema Kayombo.

Amesema wanafunzi wanaweza kufundishwa kidogo kidogo kuanzia chekechea kwa kadri kamati hiyo itaona inafaa na kujenga uelewa kwa wananchi walio wengi.

Amesema mapendelezo hayo yametokana na maoni ya wadau kwa nyakati tofauti ambao wamesema kama elimu hiyo ingefundishwa hata uchungu wa kulipa kodi ungepungua.

Amesema hata utafiti uliofanywa na TRA mwaka 2012 umeonyesha kuna haja kuanza kutoa elimu katika ngazi ya chini ili kuongeza ufahamu kuhusu masuala ya kodi.

Pia wabunge wamekuwa wakitoa mapendekezo yao kila mwaka wakati wa bajeti kuwa somo la kodi lifundishwe kuanzia ngazi za chini ili kupunguza ugumu na kujenga uzalendo wa kuilinda miundombinu ya Serikali.

Amesema kamati hiyo imepokea mapendekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi.