TRA yazindua dawati la kuwawezesha wafanyabiashara Mara
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, akihutubia wakati wa uzinduzi wa dawati maalumu la uwezeshaji biashara mkoani humo. Picha: Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Uanzishwaji wa dawati maalumu la uwezeshaji biashara ni agizo la Serikali kwa lengo la kuwatambua, kuwasikiliza na kuwawezesha wafanyabiashara hasa wasio na sekta rasmi ili hatimaye waweze kurasimishwa na kuboresha shughuli zao.
Musoma. Baadhi ya wafanyabiashara mkoani Mara wameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa elimu na kuwalea ili waweze kukua kibiashara hasa wafanyabiashara kutoka sekta zisizokuwa rasmi ili kuongeza wigo wa ajira nchini.
Wafanyabiashara hao wametoa ombi hilo mjini Musoma leo Ijumaa Septemba 12, 2025 wakati wa uzinduzi wa dawati maalumu la uwezeshaji biashara ambapo wamesema wafanyabiashara kutoka sekta zisizokuwa rasmi wanakabiliwa na changamoto nyingi hali ambayo kwa namna moja ama nyingine inakwamisha ustawi wao.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo maarufu Machinga Mkoa wa Mara Chacha Kichere amesema sekta ya biashara kwa ujumla inaweza kutumika kama suluhisho la tatizo la ukosefu wa ajira nchini endapo itapata uwezeshaji na usimamizi mzuri.
"Hii sekta ikisimamiwa vema itakuwa suluhisho la kudumu kuhusu ukosefu wa ajira nchini ambapo pia hali hiyo itasaidia kuongezaka kwa makusanyo ya kodi za serikali na hata pato na uchumi wa mwananchi," amesema
Mariam Ismail amesema kutokutambuliwa kwa wafanyabiashara hao wa sekta zisio rasmi ni moja ya sababu inayosababisha wafanyabiashara hao kukopa mikopo yenye riba kubwa maarufu kama kausha damu hivyo kusababisha kushindwa kuendeleza biahsra zao kwa ufanisi.
"Hakuna anayetutambua kwahiyo hata ukitaka kukopa kwenye taaisis rasmi hauwezi kupata mkopo mwisho wa siku unajikuta unaangukia kwenye kausha damu matokeo yake unatumikia mkopo badala ya kuboresha biashara," amesema
Akitoa maelezo kuhusu dawati hilo maalumu la uwezeshaji biashara, Meneja wa TRA Mkoa wa Mara, Nassoro Ndemo amesema pamoja na mambo mengine dawati hilo litasaidia katika kuwatambua na kuwaunganisha na fursa mbalimbali wafanyabiashara wote wakiwepo wasio rasmi.
Amesema sekta isiyo rasmi ina umuhimu mkubwa katika uchumi wa nchi kwani imetoa ajira nyingi lakini inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwepo biashara hizo kutokurasimishwa.
"Dawati hili pamoja na mambo mengine linalenga kuwatambua, kuwasikiliza na kuwawezesha ili kukuza biashara zao na hatimaye ziweze kurasimishwa hatua ambayo mbali na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa kodi lakini pia itasaisia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla" amesema
Ndemo amesema mamlaka hiyo imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa kodi kwa mwaka 2024/25 ambapo walikusanya Sh194.6 bilioni sawa na asilimia 102 ya lengo la kukusanya Sh190.2 bilioni.
Amesema uwepo wa dawati hilo utakuwa chachu kwa mamlaka hiyo kukusanya mapato zaidi kwa maendeleo ya nchi na watu wake kwani wafanyabiashara wengi watatambuliwa na kuwezeshwa ikiwa ni pamoja na kuunganishwa na taasisi za serikali sambamba na za kifedha.
Akizindua dawati hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema uanzishwaji wa dawati hilo ni moja ya mkakati wa Serikali wa kutaka kurasimisha sekta zote nchini ili kujenga uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Kanali Mtambi amesema dawati hilo linapaswa kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto za wafanyabiashara mkoani humo hasa wafanyabiashara wadogo ili kuwawezesha kukua na kuwa wafanyabiashara wakubwa.
"Shirikianeni na taasisi zote za Serikali ili kuweka mfumo mzuri wa kuwahudumia wafanyabiashara hawa pia niwaagize hakikisheni mnatoa huduma kwa weledi zile enzi za wafanyabiashara kuwakimbia watumishi wa TRA zimepitwa na wakati mahusiano mazuri yatasaidia kuboresha biashara na kukuza kiwango cha kodi," amesema
Kanali Mtambi amefafanua Serikali inaamini baada ya urasimishaji wa biashara hizo na matumizi sahihi ya dawati hilo changamoto za wafanyabiashara zitapata suluhisho la kudumu.