Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Trafiki aliyegongwa na daladala kuzikwa Kilimanjaro

Jeneza la Askari wa Usalama Barabarani, Tumsifu Kileo aliyefariki siku chache baada ya kugongwa na daladala iliyoacha njia eneo la mzunguko wa Mwanza Hoteli jijini Mwanza. Picha na Saada Amir

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbrod Mutafungwa askari huyo wa usalama barabarani alifariki dunia Ijumaa Februari 13 saa 8:30 mchana akiwa anapata matibabu Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.

Mwanza. Mwili wa askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Tumsifu Kileo umeagwa jijini Mwanza na kusafirishwa kwenda Lyamungo mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya maziko.

Kileo alifariki dunia kwa kugongwa na daladala iliyoacha njia wakati akitekeleza majukumu yake ya kuongoza magari.

Akizungumza leo Jumatatu Februari 16, 2026 wakati wa ibada ya mazishi nyumbani kwa marehemu, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Buhongwa, Lucas Baskely amewataka waendesha vyombo vya moto kutovitumia kama silaha ya kuua watumiaji wengine wa barabara.

“Tumempoteza Tumsifu, mimi kama mchungaji wake nimepoteza mtu muhimu sana..niwaombe mtumie chombo cha usafiri mkijua na kutunza uhai wa mwenzako. Tumia barabara ukijua kuna mwingine anahitaji kutumia. Tunaondoa sana uhai wa watu kwa sababu ya uzembe,” amesema.

Baadhi ya waombolezaji wakiwa nyumbani kwa marehemu, Tumsifu Kileo kabla mwili wake haujasafirishwa kuelekea mkoani Kilimanjaro kwaajili ya mazishi. Picha na Saada Amir

Amewataka madereva wasiwe na haraka isiyo ya lazima na kutothamini safari kuliko uhai kwa kuwa maisha ya mtu hayawezi kurejeshwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema ajali hiyo ilitokea Februari 10, 2026 saa 2:00 asubuhi katika mzunguko wa Mwanza Hoteli iliyopo katikati ya Jiji hilo.

Amesema askari huyo alikuwa pembeni mwa barabara akisubiri kusimamisha magari kupisha msafara wa mahabusu kutoka Gereza la Butimba, akiwa amevaa sare za Jeshi la Polisi.

“Gari lililokuwa limebeba abiria likielekea CCM makao makuu liliacha njia na kumgonga pamoja na mtembea kwa miguu aliyekuwa karibu naye,” amesema Mutafungwa.

Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye ibada ya kuaga mwili wa Askari wa Usalama Barabarani, Tumsifu Kileo. Picha na Saada Amir

Amesema majeruhi waliwahishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure kwa matibabu ya awali, kabla Coplo Tumsifu hajahamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata kichwani.

Mutafungwa amesema madaktari walijitahidi kuokoa maisha yake, lakini Ijumaa saa 8:30 mchana alifariki dunia baada ya jitihada za binadamu kushindikana.

Akitoa salamu za rambirambi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema askari huyo amefariki akiwa anatekeleza majukumu yake kwa uadilifu, akiwataka waliobahatika kulitumikia Taifa kufanya hivyo kwa upendo na kuacha kumbukumbu njema.

“Natoa pole kwa familia lakini askari wetu amefariki akiwa anatekeleza majukumu yake tuendelee kumuombea dua. Uwepo wa Jeshi la Polisi una umuhimu mkubwa sana ndio maana vituo vya polisi havifungwi, hivyo tuimarishe usalama na tukatae vitendo vyote vinavyowaelekeza wananchi kuweka chuki dhidi ya Jeshi la Polisi,”amesema Mtanda.