TRC yakunwa kasi ujenzi Bwawa la Julius Nyerere

Muktasari:

  • Kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kupatikana kwa umeme wa uhakika utakaoendesha mitambo itakayotumika kwenye mradi wa reli ya kisasa

Rufiji. Uongozi wa Shirika la Reli nchini Tanzania (TRC), umepongeza kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) huku ukisema kukamilika kwake kutasaida kupatikana umeme wa kuendesha mitambo itakayotumika kwenye mradi wa reli ya kisasa (SGR).

Huo ni muendelezo wa viongozi mbalimbali kutembelea kuona maendeleo ya mradi huo uliofikia asilimia 83.3 baada ya Makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu wastaafu waliowahi kuhudumu katika Wizara ya Nishati kufanya hivyo nyakati tofauti.

Akizungumza jana, baada ya kutembelea mradi huo unaojengwa katika Bonde la mto Rufiji mkoani Pwani, Mkurugenzi wa Mitambo wa TRC, Mhandisi Heriel Emanuel aliyeambatana na viongozi wengine wa taasisi hiyo alipongeza kasi ya ujenzi wake na kubainisha kwamba unaenda sambamba na ujenzi SGR.

"Mradi huu ni mradi mkubwa na unatekelezwa na serikali,tuna imani kukamilika kwake kutasaidia  katika shughuli za uendeshaji mashine katika mradi  wa SGR na kukamilika kwa miradi hii kutaleta manufaa makubwa kwa taifa ", alieleza Mhandisi Makange.

Akifafanua kuhusu maendeleo ya mradi huo, Mhandisi Mkazi wa JNHPP, Lutengano Mwandambo alisema kazi za mradi zinaenda vizuri na kuwa had sasa umefikia asilimia 83.3 ya ujenzi wake.

Alisema ujazaji maji ndani ya bwawa umefikia mita 135 kutoka usawa wa bahari kutoka mita 71.5 wakati bwawa lilipoanza kujazwa maji mnamo Disemba,22, 2022.

Aidha Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Shirika la Umeme nchi,(Tanesco), Elihuruma Ngowi alieleza faida za kukamilika kwa mradi huu ikiwemo kuwa na umeme wa uhakika, kilimo, utalii, uvuvi, miundombinu na usafirishaji pamoja na huduma ya maji safi na salama.

“Huduma hizo zote zinapatikana na  zote kwa pamoja zitawanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla wake na kukuza uchumi wetu,”alisema

Kina cha maji kinachohitajika kulijaza bwawa hilo ni mita za ujazo 163 hadi mita 184,hivyo hadi sasa kiwango kilichobakia ni mita za ujazo 49 kufikia ujazo wa mita 184.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa  Tanesco, Maharage Chande alisema shughuli ya ujazaji maji katika bwawa hilo unatarajiwa kuchukua miezi 18 ili kupata kiwango cha maji kitakachokuwa na uwezo wa kuzungusha mitambo ya kufua umeme kwenye mradi huo unaotegemewa kuzalisha  megawati 2,115 za umeme.