Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Treni ya umeme Dom-Dar yadaiwa kupata hitilafu, yakwama kwa muda

Muktasari:

  • Treni ya reli ya umeme (SGR) kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam imedaiwa kukwama kwa muda mkoani Morogoro usiku wa Alhamisi Agosti 1, 2024.

Dar es Salaam. Treni ya reli ya umeme (SGR) kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam imedaiwa kukwama kwa muda mkoani Morogoro usiku wa Alhamisi Agosti 1, 2024.

Treni hiyo iliyokuwa imebeba abiria na wageni mbalimbali waliotoka kwenye uzinduzi wa huduma za SGR zilizofanyika mkoani Dodoma jana.

Mmoja wa abiria aliyekuwa katika chombo hicho ameiambia Mwananchi Digital  kuwa safari ilianza bila changamoto mishale ya saa 2 usiku. 

"Tumetoka vizuri tu Dodoma," anaeleza. "Lakini tulipofika katikati ya Stesheni ya Mkata na Moro ikiwa kama saa 4:33 usiku ikasimama ghafla  na kuzima kabisa, hadi sasa saa 5:33 usiku bado tupo hapa."

Abiria Peter Nyanje, ambaye ni mhariri aliyeshiriki uzinduzi Dodoma, ameripoti changamoto hiyo kupitia ukurasa wake wa Instagram, akiandika:

"Ni saa tano usiku tulitoka Dodoma kwenye uzinduzi wa SGR. Wakati tunakaribia station ya Morogoro treni imesimama ghafla njiani, air conditions zimezima, milango haifunguki. Tumekwama hapa sasa ni zaidi ya nusu saa. Tupo takribani watu 1,000 humu ndani."

Mwananchi haijathibitisha chanzo cha changamoto hiyo, wala idadi ya abiria waliokuwa kwenye treni kutoka kwa mamlaka husika.

Tunaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuutafuta uongozi ama msemaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) ili kupata undani zaidi wa kilichojiri.

Hata hivyo, taarifa kutoka kwa abiria zinaonesha saa 5:35 usiku, treni hiyo ilifanikiwa kuendelea na safari yake mpaka Morogoro, kabla ya kuendelea kuelekea Dar es Salaam.

Hii haikuwa treni pekee iliyorejea Dar es Salaam jana ikiwa na wageni kutoka katika uzinduzi Dodoma.

Treni nyingine ya awali iliyoondoka Dodoma saa 1 usiku ikiwa na viongozi, wasanii na wadau mbalimbali, ilifanikiwa kufika Dar es Salaam bila changamoto.

"Tulitoka Dodoma saa 1 usiku tukasimama kushusha watu kwenye stesheni za Kilosa, Morogoro, Ngerengere na Pugu, tukaingia Dar es Salaam saa 5.32 usiku," anaeleza abiria aliyekuwa kwenye treni hiyo.

Anaeleza, "hakukuwa na changamoto zozote.  Tulisubiri tu kwa dakika 25 hivi hapo Pugu ili kuipisha treni ya Dar-Dodoma."

Endelea kufuatilia mitandao yetu ya Mwananchi