Trump alaumiwa kila kona duniani

Rais wa Marekani, Donald Trump
Muktasari:
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesema hatua hiyo ni ya kukatisha tamaa na kwamba mkataba huo uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa hauwezi kujadiliwa upya kwa kuzingatia ombi la taifa moja.
Berlin, Ujerumani. Muda mfupi baada ya Rais Donald Trump kutangaza uamuzi wa Marekani kujiondoa kutoka kwenye makubaliano kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, wakuu wa nchi na viongozi wa kimataifa wameshutumu hatua hiyo wakisema ni ya kukatisha tamaa.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesema hatua hiyo ni ya kukatisha tamaa na kwamba mkataba huo uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa hauwezi kujadiliwa upya kwa kuzingatia ombi la taifa moja.
Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama amesema anasikitika kuona Marekani inaungana na mataifa machache yanayoukataa mustakabali mwema wa dunia. Nchi pekee ambazo hazikusaini makubaliano ya Paris ni Nicaragua na Syria.
Katika hotuba yake kali aliyotoa kutoka Ikulu ya White House, Rais Donald Trump alisema Marekani itasitisha mara moja utekelezaji wa makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Huku akitumia kauli mbiu ya "Marekani Kwanza” ujumbe aliotumia wakati wa kampeni za urais zilizomwingiza ikulu mwaka jana, Trump alisema Mkataba wa Paris utahujumu uchumi wa Marekani, utawafanya wapoteze kazi, kudhoofisha uhuru wao na kuiweka nchi hiyo milele katika hali ya kutumiwa na mataifa mengine duniani.
Trump amesema alisema mkataba huo uliosainiwa wakati wa utawala wa mtangulizi wake Barack Obama, unawaweka katika nafasi nzuri wapinzani wa nchi hiyo kiuchumi ambao ni India, China na bara la Ulaya
Trump hakutoa maelezo kuhusu ni vipi au lini mchakato rasmi wa kujiondoa utaanza lakini aliashiria kuwa mazungumzo mapya huenda yakafanyika baadaye.
Trump apingwa
Wazo hilo lilipigwa mara moja na washirika wake viongozi wa Ulaya waliojawa na hasira, ambao waliungana na viongozi kutoka kote Marekani kulaani hatua ya Trump. Katika taarifa ya pamoja, Ufaransa, Ujerumani na Italia zimesema makubaliano hayo hayawezi kujadiliwa upya.
Baadaye Trump aliwapigia simu Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May pamoja na wa Canada Justin Trudeau kuwafafanulia uamuzi wake lakini hawajaafikiana naye.
Merkel alisema amesikitishwa na hatua hiyo na akatoa wito wa kuendelezwa sera za tabianchi ambazo zitauhifadhi ulimwengu huku Rais Macron akifafanua kuwa Ufaransa na Marekani zitaendelea kushirikiana lakini siyo kuhusu suala la mabadiliko ya tabianchi.
May alimwambia Trump kuwa mkataba wa Paris unalenga kuvilinda vizazi vijavyo wakati Rais wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker, aliishutumu hatua hiyo akisema ni mbaya.
Kamishna wa mabadiliko ya tabianchi na nishati Miguel Arias Canete amesema katika taarifa yake kuwa Alhamisi ilikuwa siku ya majonzi kwa jumuiya ya kimataifa baada ya mshirika muhimu kubadili msimamo wake katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha, magavana wa Democratic wa majimbo ya New York, California na Washington waliunda muungano wa haraka, wakiapa kuendelea kuheshimu viwango vilivyokubaliwa chini ya mkataba wa Paris.
Taarifa za kisayansi zinaonyesha kwamba China na Marekani huchangia asilimia 40 ya gesi chafu ulimwenguni na watalaamu walionya kuwa ni muhimu kwa nchi hizo mbili kubakia katika makubaliano ya Paris ili yaweze kufanikiwa.
Uamuzi huo imeelezwa unaweza kuipa China nafasi kubwa kujadili masuala ya tabianchi. Nchini Marekani watendaji wakuu wa mashirika makubwa kama vile Tesla and SpaceX, wametoa taarifa ya kusikitishwa na hatua ya Trump.
Ikulu ya White House imesema itaheshimu sheria za Umoja wa Mataifa za kujiondoa kutoka kwa mkataba huo. Sheria hizo zinahitaji taifa kusubiri miaka mitatu kuanzia tarehe ambayo mkataba huo uliidhinishwa kisheria, Novemba 4, 2016 kabla ya kuanza kujiondoa rasmi.
Pia, nchi hiyo lazima isubiri mwaka mwingine mmoja. Mkataba wa Paris unazitaka nchi zote zilizotia saini kupunguza utoaji gesi inayochafua mazingira ambayo husababisha ongezeko la joto duniani.