Tucta waomba Rais Samia asikilize kilio chao

New Content Item (1)
Tucta waomba Rais Samia asikilize kilio chao

Muktasari:

  • Shirikisho huru la vyama vya wafanyakazi Tanzania (Tucta), limesema lina matumaini na Rais mpya wa Tanzania, Samia Suluhu  Hassan atashughulikia madai yao  ya muda mrefu  yalipwe kwa wakati  ili kuinua maisha ya wafanyakazi.

Dar es Salaam. Shirikisho huru la vyama vya wafanyakazi Tanzania (Tucta), limesema lina matumaini na Rais mpya wa Tanzania, Samia Suluhu  Hassan atashughulikia madai yao  ya muda mrefu  yalipwe kwa wakati  ili kuinua maisha ya wafanyakazi.

Tucta imesema Hayati Dkt. John  Magufuli alishaanza kufanyia kazi malalamiko yao kupitia vikao maalumu alivyokuwa anafanya na viongozi wa Tucta, hivyo ni mategemeo yao Samia ataendeleza pale alipoishia mtangulizi wake kuhakikisha anamaliza changamoto hiyo kabisa.
Akizungumza Dar es Salaam leo Machi 28,2021 kwa njia ya simu  na gazeti hili, kuelezea matarajio yao kwa Rais mpya.
Kaimu Katibu Mkuu wa Tucta, Said Wamba amesema wanaanzia walipoishi na Hayati Magufuli  kwamba madai yao ya mishahara na hali bora ya maisha kwa wafanyakazi yanaendelea.
“Na matumaini yetu, rais mpya na watendaji wake watayaona madai yetu ni yamaana na yamsingi kwa maendeleo ya wafanyakazi na wananchi kwa ujumla.  mishahara, kodi na tulishaandika barua kwenda serikalini kuwaomba watupunguzie kiwango cha kodi ya mapato  ambayo wanafanyakazi wanalipa kupitia fedha zao  tunashukuru mwakajana walipunguza kwa kiasi fulani lakini safari hii  tunaomba wapunguze pia ,”
“Mishahara na marupurupu ya wafanyakazi ambayo yalisimama kwa muda mrefu  sasa tunaomba yaanze kupatikana ,” anasema
Wamba ameeleza wanamiaka minane sasa hawajaongezewa  kiwango cha mshahara na mara ya mwisho kuongezewa  ilikuwa mwaka 2013, licha ya kwamba uongozi wa shirikisho hilo umekuwa ukijitahidi kudai madai hayo kila mwaka kupitia skukuu ya wafanyakazi inayofanyika Mei Mosi kila mwaka lakini bado hawaja timiziwa.
“ Tunaamini Rais atatumia busara  na watendaji wake wengine kuangalia kilio chetu na akituongezea itasaidia kuinua morali ya ufanyaji kazi,” anasema Wamba.
Pia amesema Rais Magufuli aliwawekea utaratibu wa kukutana naye mara mbili au tatu kila mwaka na kupitia mikutano hiyo ilikuwa inasaidia kumaliza baadhi ya changamoto ndogo ndogo zilizokuwa zina wakwamisha kwenye shughuli zao.
“Tunafikiri naye Rais mpya kurithi utaratibu huo wa kukutana na vyama vya wafanyakazi kila wakati  kuondoa matatizo madogo madogo  kwa mazungumzo ya kawaida kupata ufumbuzi kuliko kuamini kufuata sheria au kuanzisha mapambano ambayo kimsingi yanawapotezea muda,” alisema.
Mwamba amemaliza kwa kutoa wito kwa wafanyakazi wote katika kipindi hiki wanatakiwa kuwa na subra  kumpa muda wa kutosha  Rais mpya kwa kuwa anakabiliwa na majukumu mengi ya kufanya, huku akiwataka kuendelea kutimiza wajibu wao wakati viongozi wa Tucta wakifanya utaratibu wa kufuatilia madai hayo.