Tuzo za Tehama kuchochea ubunifu, kufanyika Aprili
Muktasari:
- Tuzo hizo zinatajwa kutia hamasa zaidi kwa wadau kufanya vizuri katika maeneo mbalimbali ambayo Tehama inatumika kama vile kutoa huduma za kijamii, uzalishaji mali, utafiti, ubunifu, utawala, elimu na afya.
Dar es Salaam. Katika kuchochea ubunifu, hamasa, kutambua jitihada za kipekee zilizofanywa na wadau wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Tume ya Tehama (ICTC), kwa kushirikiana na wadau imetangaza kufanyika kwa tuzo za Tehama Aprili mwaka huu.
Tuzo hizo zinatajwa kutia hamasa zaidi kwa wadau kufanya vizuri katika maeneo mbalimbali ambayo Tehama inatumika kama vile kutoa huduma za kijamii, uzalishaji mali, utafiti, ubunifu, utawala, elimu na afya
Akizungumza mwishoni mwa juma Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama Dk Nkundwe Mwasaga amesema tume kwa kushirikiana na wataalamu, na kampuni za Tehama ni njia pekee ambayo Serikali inaendelea kutambua mchango mkubwa wa wawekezaji, wabunifu, watafiti, wajasiriamali, wanataaluma na wadau wengine wote wa Tehama katika kuchagiza maendeleo ya taifa na kufikia uchumi wa kidijitali.
"Hafla hii ya kitaifa itawaleta pamoja viongozi mbalimbali wa Serikali na Taasisi binafsi, wavumbuzi, watunga sera, wajasiriamali, wasomi, na washirika wa maendeleo ili kusherehekea ubora na mchango katika sekta ya Tehama.
"Tuzo za Tehama 2026 ni moja ya majukwaa ya kuhamasisha ukuaji wa uchumi wakidijitali kwani kwa upekee inalenga kusheherekea mafanikio ya sekta, kuchochea uvumbuzi na ushindani wenye tija, kuchochea mabadiliko ya kidijitali katika nyanja mbalimbali na kuwatambua wadau wanaochochea maendeleo ya kiteknolojia," amesema.
Dk Mwasaga amesema tuzo zitachagiza utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Uchumi wa Kidijitali na Dira ya Maendeleo ya 2050 ambayo imeainisha mageuzi ya kidijitali kama moja ya kichocheo cha kufikia malengo ya dira hiyo.
Kufuatia mafanikio makubwa ya Tuzo za Tehama 2025, yaliyorekodi washiriki 380 waliojisajili, washindi 54 waliopata tuzo kutoka sekta ya ummm na binafsi, zaidi ya wahudhuriaji 500, na watazamaji wa mtandaoni zaidi ya 15,000.
Ametoa wito kwa wavumbuzi, wataalamu wa Tehama kampuni changa (startups), watafiti, viongozi wanawake katika teknolojia, wajasiriamali, watoa huduma, wawekezaji pamoja na wadau mbalimbali kushiriki katika tuzo hizo.
Dirisha la maombi kwa washiriki wa tuzo limefunguliwa kwa wadau wote hadi Machi 15, 2026. Kwa maelezo zaidi kuhusu utaratibu wa maombi, uchambuzi, fursa za udhamini na ushiriki katika hafla hiyo, wadau wanaweza kutembelea tovuti ya tuzo.
Tuzo hizo tume inashirikiana na Chama cha Watoa Huduma za Mtandao Tanzania (TISPA) na Soft Ventures.