Twende zetu kileleni yaongeza njia mbili

Mhifadhi utalii katika hifadhi ya Mlima ya Mlima Kilimanjaro, VitusĀ  Mgaya akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa kampeni za twende zetu kileleni 2023. Picha na Fina Lyimo

Muktasari:

  • Zoezi la kupanda Mlima Kilimanjaro linatarajiwa kuanza Desemba 3, 4 na 5, mwaka huu, huku njia mbili zikiongzwa ambazo ni Machame na Lemosho na hivyo kurahisha upandishaji watalii ajili ya maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru katika kampeni ya twenzetu kileleni.

Moshi. Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9 mwaka huu, zoezi la kupanda Mlima Kilimanjaro linatarajiwa kufanyika Desemba 3, 4 na 5, mwaka huu, huku zikiongezwa njia mbili.

Njia hizo ni pamoja na ile ya Machame na Lemosho ambazo zitatumika kupandisha watalii watakao panda mlima huo kwa ajili ya maadhimisho hayo.

Akizungumza leo Ijumaa oktoba 20, 2023, Mhifadhi Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (Kinapa), Vitus Mgaya amesema kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatakuwa tofauti na miaka ya nyuma.

Utofauti huo unatokan na watalii kuwa na uhuru wa kuchagua njia, tofauti na miaka ya nyuma ambapo walikuwa wakitumia njia moja pekee ya Marangu.

Amesema pia kutumia njia tatu za Lemosho, Machame na Marangu, kumetoa fursa kwa makampuni ya utalii kuwenza kupandisha watalii katika mlima huo kupitia malango matatu tofauti, hatua ambayo itaongeza idada ya watalii watakao panda mlima huo kwa ajili ya kusherekea maadhimisho hayo ya uhuru

"Mwaka huu ni msimu wa tatu kutokana na uhitaji wa watalii tumeongeza wigo kwa makampuni ya watalii kuweza kupandisha watalii katika kampeni ya twende zetu kileleni kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru," amesema Mgaya

Amesema wameongeza kampuni mbili ambazo zitaratibu upandishaji wa watalii katika mlima huo na kwamba njia ya Marangu itaratibiwa na kampuni ya Zara Tours, njia ya Machame itaratibiwa na kampuni ya Afrikani Zoom huku Lemosho ikiratibiwa na African Cenic.

Ofisa Masoko Kampuni ya uokoaji watalii Mlima Kilimanjaro Kilimed Air, Peter Sarakikya, amesema kuwa wamejiandaa kushiriki kikamilifu katika kuwahudumia watalii katika hifadhi ya mlima huo.