Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ubovu barabara wasababisha wananchi kulipa nauli ya bodaboda Sh30, 000 Kibakwe

Muktasari:

Wananchi wa Kijiji cha Wangi kilichopo Tarafa ya Kibakwe, Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, wanakumbwa na adha ya usafiri kutokana na ubovu wa barabara kuanzia Kijiji Lwihomelo hadi Kata ya Wangi.

Mpwapwa. Wananchi wa Kijiji cha Wangi kilichopo Tarafa ya Kibakwe, Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, wanakumbwa na adha ya usafiri kutokana na ubovu wa barabara kuanzia Kijiji Lwihomelo hadi Kata ya Wangi.

Wananchi wamekumbwa na kadhia hiyo ya usafiri kwa muda mrefu ya kufika jimboni Kibakwe, ambako kuna huduma mbalimbali za jamii, kutokana na ubovu wa barabara kuanzia Kijiji cha Lwihomelo hadi ilipo Kata ya Wangi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wananchi, changamoto kubwa ya eneo hilo ni usafiri unaotokana na maji ya Mto Itiliko kujaa hasa wakati wa masika hasa kuanzia mwezi Novemba hadi katikati ya Mei, ambapo wakazi wa eneo hilo hujikuta wapo kisiwani kwa muda.

Kijana Haruna Ismail anasema maendeleo ya Kata ya Wangi yanacheleweshwa na miundombinu mibovu ya barabara katika kata hiyo, jambo lililosababisha nauli ya kwenda Kibakwe Sh15, 000 na kurudi pia Sh 15,000 kwa  mtu mmoja kwa umbali wa takribani kilometa 15 hadi 20.

Anasema kuna wakati alitaka kuhama kijiji hicho kwa sababu alikuwa anashindwa kumudu gharama za usafiri huo wa bodaboda. 

Anasema kwa kuwa diwani wao Madotela Chabuluma ana nafasi mbili kwenye baraza la madiwani, anayo nafasi ya kutatua kero zao lakini, haelewi wapi anakwama, hasa kushughulikia ubovu wa barabara. Anafafanua kuwa mambo mengine ambayo viongozi walipaswa kuyawekea kipaumbele ni suala la umeme kwa kila kaya. Pia, kumalizia kupaua jengo la ofisi za kata, kujengwa shule ya sekondari ya kata pamoja na kuboresha Shule ya Msingi Wangi ambayo ni kongwe, lakini miundombinu yake ni mibovu.

Barabara

Mkulima Dismass John anasema kwamba, ahadi iliyotolewa ni kwamba baada ya mvua za sasa kuisha kazi ya kuchimbua barabara itaanza. Hata hivyo, hofu yake ni kwamba huenda ikawa ni kuziba mashimo pekee na siyo kuitengeneza kwa kiwango cha changarawe kama ilivyo kwa barabara nyingine za kata za jirani.

Anasema ipo haja ya kutafuta suluhu ya kudumu kwa barabara hiyo, likiwemo daraja linalotenganisha Wangi na Lwihomelo, kwenye Mto Itiliko jambo ambalo linaweza kupunguza makali ya nauli kwa usafiri kwani hata magari yanaweza kufika kwa uhakika.

Mwananchi mwingine ambaye hakupenda jina lake liandikwe anasema, suala la barabara bado litaendelea kuwa changamoto kwa sababu kila mwaka wa fedha, bajeti inatengwa lakini haoni matokeo kwenye kuboresha miundombinu ya barabara.

Mfanyabiashara maarufu wa nyama kijijini hapo, Elyuta Lukosi maarufu George anasema kwamba kikao cha kijiji kilichofanyika hivi karibuni, viongozi wao waliahidi kwamba barabara hiyo itaanza kufanyiwa kazi baada ya mvua kuisha lakini hakuna uhakika iwapo itachimbuliwa kwa mikono na wanakijiji au na Tarura, maana imekuwa ni ahadi ya muda mrefu.


Changamoto ya elimu

Akizungumzia kuhusu miundombinu ya barabara inavyochangia gharama za usafiri kwa walimu wa Shule ya Msingi Wangi, Mwalimu Shomi Nasoni anasema maendeleo siku zote huletwa na wananchi wenyewe kwa kushirikiana na viongozi wao.

Anasema changamoto kubwa ni miundombinu ya barabara kufika kijijini hapo. Anafafanua kuwa changamoto hujitokeza kwa walimu wanapotakiwa kwenda kupata mafunzo ya kazi wilayani Mpwapwa.

“Kutokana na ubovu wa barabara humlazimu mwalimu kutumia takribani shilingi elfu sabini (70,000) kwenda na kurudi iwapo atalazimka kulala mjini kutokana na kuchelewa usafiri. Nasoni anaongeza kuwa,

kutokana na miundombinu mibovu ya kufika Kata ya Wangi, huwatia shaka walimu wanapofika eneo hilo kufanya kazi kwa sababu huduma kama za kibenki zote zinapatikana wilayani.

“Tunawashawishi wenzetu kubaki kituo cha kazi, lakini baadhi wakionyesha nia kwamba wanaangalia mazingia tu na siyo sehemu ambayo watafanya kazi kwa muda mrefu,” anasema Nassoni.

Anasema kwa sasa shule hiyo ina vyumba vya madarasa 10 ambapo inalazimika kuweka wanafunzi zaidi ya 70 kwenye darasa moja ili kukidhi mahitaji. Anashauri kwamba kungekuwepo wa shule ya sekondari ya kata katika Kijiji cha Wangi, ingewaepushia wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda Kata ya Wotta.

Shule ya Msingi Wangi ni miongoni mwa shule kongwe nchini iliyoanzishwa tangu mwaka 1976, ina jumla ya wanafunzi 552 kuanzia darasa la kwanza hadi darasa la saba. Idadi ya walimu jumla yao ni 10 baada ya kuongezwa wengine wanne.

Shule hiyo ina matundu ya choo 10, huku idadi ya wanafunzi ikiwa haiendani uwiano na matundu hayo yaliyopo. Vilevile hakuna nyumba za walimu. Mwalimu mkuu anaishi kwenye nyumba  iliyoachwa na mwanakijiji mmoja.


Sekondari ya kata

Anafafanua kwamba mwaka jana ilielezwa kuwa, eneo la shule ya Msingi Wangi lipatalo ekari  takribani 11 litagawanywa na kujengwa shule ya sekondari ya kata na

“Kiasi cha fedha Sh100 millioni kilitengwa kwa ajili ya kazi hiyo, lakini  fedha hizo ilielezwa zimekwenda kujenga shule ya sekondari ya Kata Wotta.


Huduma ya umeme

Geofrey Samson (siyo jina lake halisi) anasema nyumbani kwake bado hajafikiwa na umeme licha ya kwamba serikali imesaidia kata hiyo yenye vijiji vinne vya Wangi, Lwihomelo, Kidabaga na Nyandu kufikiwa na umeme.

 Anasema uhalisia wa jambo hilo kuwa watu wengi wamepata umeme, haiendani na uhalisia kuwa umeme huo umezifikia kaya chache ambazo zipo barabarani, na ni

asilimia 10 ya wanakijiji wote ndio waliopata umeme huku takribani asilimia 90 wakiwa hawana umeme,” anafafanua. “Umeme wa njia tatu (3 phase) umesambazwa kwa kiwango kidogo  jambo ambalo linakwamisha mipango mingi ya maendeleo, hasa uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo,” anasema.


Huduma ya afya

Mwanakijiji mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini anasema, huduma za afya kijijini hapo zinapatikana lakini ipo haja zahanati kupandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya ili ikidhi mahitaji ya kuhudumia eneo hilo.

Kata ya Wangi inakadiriwa kuwa na wakazi wasiopungua 16,000, lakini zahanati hiyo haina miundombinu ya kuhudumia idadi hiyo ya watu. Hofu kubwa huwa ni pindi inapotokea mgonjwa wa dharura akapewa rufaa ya kwenda wilayani Mpwapwa ambako ni zaidi ya kilometa 50. Miundombinu ya barabara ni mibovu iwapo mgonjwa  atahitajika kusafirishwa kwa bodaboda hadi Kibakwe ndipo apate usafiri wa kwenda Mpwapwa.

Anasema hajawahi kushuhudia tukio la mgonjwa kuwahishwa hosptiali ya wilaya, lakini anahoji iwapo barabara ya Wangi itaendelea kuwa katika hali hiyo na mvua za masika hazitabiriki kuanza kwake na kuisha tofauti na zamani.


Ofisi za kata

Mkulima Osward John ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho anasema, kwa sasa bado wanahudumiwa kwenye ofisi za kijiji kutokana na majengo ya ofisi za kata kutokamilika. Anasema wananchi walijitolea katika ujenzi wa ofisi hizo ambazo zimebaki hatua ya kupauliwa.

 “Kukamilika kwa ofisi hizi itapunguza matukio ya uhalifu inayojitokeza hivi sasa. Anasema hatua iliyobaki ni vyema serikali ikaona umuhimu wa kulikamilisha jengo hilo kwa kupaua na kumalizia vitu vingine ili huduma mbalimbali zipatikane kwenye ofisi za kata kuliko hali ilivyo sasa.

Mtendaji wa Kata ya Wangi, Shukrani Nziga alipotafutwa kwa ajili ya kuzungumzia mambo mbalimbali pamoja na miundombinu ya barabara, alieleza kuwa hayupo eneo hilo atafutwe mtendaji wa kijijini.

Mtendaji wa Kijiji, Herith Ngeze ambaye alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia jambo lolote kwa sababu amepokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake aliyeondolewa na wananchi hivi karibuni, hivyo bado anatembelea maeneo mbalimbali kujua zaidi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpwapwa, Mwanahamisi Ally alipozungumza na mwandishi kwa njia ya simu kuhusu kero za wananchi hizo, alisema masuala ya afya, miundombinu ya umeme, barabara, elimu ni vyema wananchi wakatumia vikao rasmi kueleza kero zao kuliko  kuzipeleka ngazi za juu.

“Wapo baadhi ya wananchi wanapiga simu ngazi za juu hata Ikulu kueleza kero zao jambo ambalo siyo sahihi. Mambo mengi yanaanzia kwenye baraza la madiwani na kujadiliwa," anasema Mkurugenzi Mwanahamisi.

Anasema yapo baadhi ya mambo kama vile zahanati kuwa na uwezo mdogo wa kuhudumia wananchi hayo yanapaswa kuwasilishwa kwa viongozi kama mbunge, diwani na mtendaji wa kata.

Anasema mwaka jana mwezi wa nane ndipo alianza kazi kwenye Halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa na katika bajeti ya mwaka 2021/2022 hakuona kutengwa kiasi cha Sh100 milioni zinazoelezwa kuwa zilikwenda Kata ya Mwanawota.

“Wananchi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuanzisha na kuibua miradi mipya. Mbinu hiyo itawawezesha hata kuwatia moyo viongozi na inakuwa rahisi hata kwa serikali kuwaunga mkono wanapoonyesha jitihada,” anafafanua.

Anasema suala la miundombinu ya barabara lipo chini ya Tarura na pia suala la wananchi waliopo kando ya barabara kupata umeme anashauri ni vyema waliopitiwa mbali na nguzo mbali wavute umeme, kwani serikali ilichofanya ni kusogeza huduma hiyo.

“Mkurugenzi alisema, Yeye anazungumzia mambo yaliyo ndani ya uwezo wake, suala la miundombinu ya umeme lipo chini ya Tanesco na barabara ipo chini ya Tarura.

Hata hivyo alisisitiza kuwa, hajapokea malalamiko yoyote wala kusikia kuhusu barabara ya Lwihomelo- Wangi lakini aliahidi kufuatilia kwa wahusika idara moja baada ya nyingine mara moja.