Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ubunifu nishati mbadala suluhu utunzaji mazingira

Mkurugenzi wa Kuja na Kushoka Manufacture, Leonald Kushoka akionyesha baadhi ya mashine za kutengeneza mkaa mbadala, majiko bunifu alipotembelewa na mwandishi wa makala haya. Picha na Johnson James

Tabora. Katika jitihada za kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia nchini, wabunifu mbalimbali wamekuwa wakibuni mbinu mbadala zinazosaidia kupunguza utegemezi huo.

Leonald Kushoka, mbunifu kutoka mkoani Tabora, ambaye ni Mkurugenzi wa Kuja na Kushoka Manufacture, amejikita katika utengenezaji wa majiko banifu na mashine za kutengeneza mkaa mbadala na kuchakata mazao.

Katika mahojiano na Mwananchi, Kushoka anasema alianza kuunda bunifu hizi za nishati mbadala mwaka 2018. “Nilianza kutengeneza mashine za kuchakata mazao mwaka 2008, lakini mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa misitu uliosababishwa na ukataji miti ovyo, vilinisukuma kubuni mashine za kutengeneza mkaa mbadala mwaka 2018,” alieleza Kushoka.


Utengenezaji wa mashine

Kushoka amejikita katika kutengeneza mashine za nishati safi, ikiwemo majiko banifu, mashine za kuchakata mkaa mbadala na mkaa mbadala wenyewe, ambayo inachangia kupunguza matumizi ya nishati za asili kama kuni na mkaa wa kawaida.

Kuhusu teknolojia anayotumia, alisisitiza kuwa anazingatia ubora akiwa na lengo la kusambaza mashine hizo kwa taasisi na watu binafsi wanaoweza kuanzisha na kufanya uzalishaji mkubwa wa mkaa mbadala, jambo litakaloisaidia jamii kuacha kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Akifafanua zaidi kuhusu mkaa mbadala, alisema “malighafi za kutengeneza mkaa mbadala hazihitaji ukataji wa miti, kwani kwa kiasi kikubwa ni mabaki ya mimea, pumba, maranda, mpunga, maganda ya karanga na mabaki yote ya mimea kwa ujumla wake.”

Akizungumzia ufanisi wa mkaa na majiko, alisema hayatoi moshi na moto wake ni mkali kuliko wa mkaa au kuni.

Mwaka 2018, Kampuni ya Kuja na Kushoka, inayomilikiwa na Kushoka iliibuka mshindi wa kwanza kitaifa kwenye mashindano ya ubunifu wa mkaa mbadala yaliyoratibiwa na Wizara ya Muungano na Mazingira.


Ubunifu na fursa za kiuchumi

Kushoka alieleza kuwa utengenezaji wa mashine za nishati safi umeleta faida kubwa kwake na kwa jamii.

“Nimepata tenda ya kufunga mashine za nishati safi kwa zaidi ya shule 100 kote nchini, pamoja na wateja wa rejareja. Hii imeongeza kipato kwa kampuni yangu.”

“Kinachonipa moyo zaidi ni kuona Serikali inatambua kazi yetu na inatupa ushirikiano,” aliongeza Kushoka, ambaye pia alikuwa mshindi wa tatu kitaifa kwenye mashindano ya ubunifu ya kitaifa yaliyofanyika mwaka 2022.

Alisema malighafi anazotengenezea mashine hizo hupatikana kwa urahisi. “Malighafi muhimu kama mota na injini za dizeli zinapatikana kwa urahisi madukani, jambo linalonisaidia kutengeneza mashine nyingi bila changamoto,” alisema.

Kutokana na tofauti za aina za wateja na idadi ya watumiaji wa mashine hizo, Kushoka anazitengeneza kulingana na uhitaji na uwezo wa wateja. “Tuna mashine zinazoweza kutengeneza kilo 30 za mkaa mbadala kwa siku, za kilo 100 kwa saa, na hata za kilo 300 kwa saa. Mbali na mkaa mbadala, tumeanzisha pia uzalishaji wa mashine za kutengeneza kuni mbadala. Gharama zinatofautiana kulingana na aina ya mashine anayotaka mteja,” alifafanua.

Alisema, “soko kubwa ni watu binafsi wanaonunua mashine tunawaelekeza namna ya kuzitumia na kuzalisha nishati wao wenyewe,” alisema.


Changamoto na mapendekezo

Pamoja na mafanikio hayo, Kushoka alitaja changamoto zinazohitaji kushughulikiwa, ikiwemo ukubwa wa kodi za malighafi na bidhaa anazotengeneza.


Fursa za ajira

“Hadi sasa nimeajiri vijana 13, wanne wakiwa Dar es Salaam wanaouza mashine na nishati ya mkaa mbadala, na tisa wapo hapa (Tabora),” alisema.

Alifafanua kuwa ubunifu wa nishati safi siyo umeme na gesi pekee, bali pia mkaa na kuni mbadala. “Tukitumia nishati hizi kwa pamoja, tutashinda vita dhidi ya uharibifu wa mazingira. Watu wengi wataacha kukata kuni na kuchoma mkaa,” alisema.


Serikali yatoa neno, mzongozo

Mkurugenzi Mkuu Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (Tirdo), Profesa Mkumbukwa Mtambo alisema changamoto wanayopata watengenezaji wa mkaa mbadala ni ukosefu wa malighafi pamoja na bidhaa wanazotengeneza kukosa ubora.

Kuhusu ubora wa mkaa unaotengenezwa, alisema kwa mikoa 12 nchini wamebaini sampuli 43 zilizochunguzwa asilimia 52 hazina ubora unaohitajika.

“Watengenezaji wengi wa mkaa mbadala bado wanatumia mkaa kutengeneza bidhaa hiyo, kwa hiyo tulichofanya ni kutoa mafunzo namna ya kutengeneza mkaa mbadala kupitia baadhi ya malighafi kama vifuu vya nazi, taka na pumba za mpunga,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa masuala ya Kiuchumi na Umaskini (Repoa), Dk Donald Mmari ambaye ni mshirika wa Tirdo katika utekelezaji wa mradi wa kuwajengea uwezo wajasiriamali wanaojihusisha na kutengeneza mkaa mbadala, alisema uharibifu wa mazingira unachochewa na matumizi ya nishati.

“Pamoja na kwamba tunafanya tafiti kwenye masuala ya kisera za kiuchumi na kijamii, moja ya mambo tuliyobaini ni uharibifu wa mazingira kunakohusiana na shughuli za binadamu, ikiwemo matumizi ya nishati inayotokana na kuni.

“Mwaka 2015 upotevu wa misitu ulikuwa hekta 300,072 baada ya miaka saba (2022) upotevu wa miti ukaongezeka kufikia hekta 469,420, ikiwa ni ongezeko la asilimia 26,” alisema.

Dk Mmari alisema ukataji huo mkubwa wa miti unakwenda kuongeza ukame na majanga, akisisitiza biashara ya mkaa ni kubwa lakini hakuna halmashauri inayodhibiti uzalishaji wake.

Kuhusu mikoa yenye watengenezaji wengi na watumiaji wa mkaa mbadala, Mkuu wa Kitengo cha Mazingira Tirdo, Kunda Sikazwe alisema Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kuwa na idadi kubwa ya watu wanaotumia na kutengeneza nishati hiyo.


Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.