Uchaguzi Konde ulivyoonyesha ukomavu wa demokrasia Zanzibar

Muktasari:

  • Licha ya mivutano ya mara kwa mara ya kisiasa visiwani Zanzibar bado visiwa hivyo vimeendelea kuonyesha ukomavu wa kidemokrasia kila zinapofanyika chaguzi.

Zanzibar. Licha ya mivutano ya mara kwa mara ya kisiasa visiwani Zanzibar bado visiwa hivyo vimeendelea kuonyesha ukomavu wa kidemokrasia kila zinapofanyika chaguzi.

Katika siku za karibuni kulikuwa na hali ya kutoelewana kati ya viongozi na wafuasi wa Chama cha ACT-Wazalendo dhidi ya wenzao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulikotokana na matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa jimbo la Konde uliofanyika Julai 18, 2021.

Takribani mwaka mmoja, uchaguzi wa Jimbo la Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar umefanyika mara tatu ili kumpata mbunge. Ndani ya muda huo baadhi ya viongozi na wanachama wa ACT-Wazalendo ambacho ndicho chama kinachoshirikiana na CCM kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) walionyesha dalili za kutaka kujiondoa kwenye Serikali hiyo.

Kimsingi ukomavu wa kisiasa na busara za viongozi vilichangia kupungua kwa uhasama na chuki ya kisiasa visiwani Zanzibar baada ya kufanyika marebisho ya Katiba ya mwaka 2010 yaliyotoa mwanya kwa vyama viwili shindani kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

SUK ilipunguza uhasama na chuki ya muda mrefu uliosababishwa na itikadi za kisiasa kiasi cha watu kutoshirikiana katika misiba, harusi na shughuli mbalimbali za kijamii.

Uchaguzi wa Mkuu uliofanyika Oktoba 2020 katika jimbo la Konde Khatibu Said Haji (marehemu) wa ACT-Wazalendo aliibuka kidedea katika kinyang’anyiro hicho. Hata hivyo alifariki dunia Mei 2021 katika hospitali ya Taifa Muhimbili najimbo hilo kubaki wazi.

Julai 18, 2021 uchaguzi mdogo wa Jimbo hilo ulifanyika tena na Sheha Faki Mpemba (CCM) alishinda kwa kupata kura 1,796 dhidi ya Mohamed Said Issa (ACT-Wazalendo) aliyepata kura 1,373 kati ya kura 5050 zilizopigwa.

Ushindi huo wa Mpemba (CCM), ulilamikiwa na ACT-Wazalendo kuwa ulijaa mizengwe na ulipoka ushindi wao hivyo wanatafakari uwapo wao ndani ya SUK. Waliweka wazi kuwa hawaoni sababu ya kuendelea kushirikiana na wenzao wasiofuata misingi ya kidemokrasia.

Baada ya mivutano ya hapa na pale, Agosti 2, mwaka huu, Mpemba alitangaza kujizulu kabla hajaapishwa akidai kuna watu wanamtishia Amani yeye na familia yake.

Siku chache baada ya kujiuzulu kwa Mpemba, Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud wakati akizungumza na wazee wa chama hicho Chakechake Pemba, alifichua siri kwamba Mpemba amejiuzulu baada ya yeye (Othman) na viongozi wengine wa chama hicho kuzungumza na Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Hussein Mwinyi na kuwaeleza dhuluma iliyofanyika katika uchaguzi huo.

Baada ya Mpemba kujiuzulu, jimbo lilibaki tena wazi hivyo Nec ikaanza mchakato wa kutanganza upya uchaguzi wa marudio ambao ulifanyika Oktoba 9, 2021.

Katika matokeo ya uchaguzi huo, meza ilipinduliwa ambapo mgombea wa ACT, Issa alitangazwa na Nec kuibuka mshindi katika jimbo hilo kwa kupata kura 2,391 akifuatiwa na mgombea wa CCM, Mbarouk Amour Habib aliyepata kura 794 kati ya kura 3,408 zilizopigwa huku halali zikiwa 3,338 na kura 70 ziliharibika.


Viongozi wafunguka

Kaimu Naibu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Salim Bimani anasema katika uchaguzi wenye haki ni lazima wangeshinda jimbo hilo maana hakuna rekodi ya CCM kushinda Pemba.

Anasema msingi wa wao kuwemo ndani ya SUK ni kuleta umoja na kuhakikisha nchi inaongozwa kwa kuzingatia sheria na Katiba hivyo wanapoona ridhaa ya wananchi inapindishwa hawawezi kuvumilia.

Bimani anasema ACT-Wazalendo wako tayari kukubali kushindwa kwenye eneo ambalo haki ilitendeka na mgombea wao alishindwa lakini si kama ilivyofanyika Konde ambapo CCM walilazimisha ushindi hivyo kutia doa demokrasia.

“Nchi yetu itajengwa kama kila mmoja wetu ataheshimu msingi ya demokrasia, anayeshinda apewe ushindi na aliyeshindwa ajiandae kwa uchaguzi mwingine” anasema Bimani

Bimani anasema vyombo vya ulinzi hususani jeshi la polisi vinapofanya kazi zao bila upendeleo ni wazi CCM watapata wakati mgumu wa kukabiliana na wapinzani ambao kila kukicha wanaimarika.

Naibu Katibu Mkuu CCM, Abdulla Juma Mabodi anasema CCM siku zote wanahubiri amani, mshikamano na upendo na ina dhamira ya dhati kabisa kuleta mabadiliko makubwa kwa wananchi.

Hivyo anasema wameridhika na kilichotokea Konde wanaimani NEC iliyosimamia uchaguzi huo na matokeo yaliyotokea kwenye sanduku la kupiga kura na kwasasa wanajipanga na uchaguzi ujao.

“Hatujakosea popote kilichopo ni suala la kimkakati, kampeni tulifanya, kilichotokea kwenye sanduku ndio hicho, tunaiamini Tume ya uchaguzi kilichobaki sasa ni kuendelea kushirikiana kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema

Hata hivyo anasema ni vema wapinzani wakawa wanakubali matokeo ya kushindwa badala kila mara kudai kulikuwa na wizi wa kura

Anasema si sahihi kwa wapinzani kuona demokrasia imefanyika vema wanaposhinda lakini wakishindwa wanakimbilia kudai kuwapo kwa hila.

Naye Katibu wa Itikadi na uenezi, Shaka Hamdu Shaka, aliwapongeza ACT-Wazalendo kwa kushinda Konde na wao wanaamini “kuvunjika kwa koleo si mwisho wa uhunzi”

“Tutaendelea kujipanga na kushiriki katika chaguzi zinazofuata, kwetu sisi ni funzo kubwa kwakuwa tunanamini kwamba Watanzania tunaweza kufanya siasa na kuhuisha na kuitukuza demokrasia yetu na ikawa funzo kwa wengine ambao wanaiangalia Tanzania kama kioo katika mwenendo wa siasa za vyama vingi” anasema Shaka


Nini mustakbali

Seif Abeid Seif ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa, anasema matokeo hayo ni uthibitisho wa ukomavu wa demokrasia miongoni mwa wanasiasa na wafuasi wao.

anasema kinachofanyika ni kuangalia maslahi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo kimsingi iliundwa ili kuleta usawa kwa Wananchi wa Zanzibar.

“Kinachofanywa na viongozi wa pande zote mbili ni kuangalia jinsi ya kuweka mambo sawa ili isije kuibuka matatizo kama yaliyoshuhudiwa katika vipindi vilivyopita, hili ni jambo jema na linaonyesha ukomavu wa kisiasa.

Naye Abdulla Hamad anasema hali iliyotokea katika kipindi hiki inaweza kutafsiriwa kila mmoja kwa namna yake lakini jambo kubwa linalolengwa ni kuimarisha SUK.

Said Abdalla Said anasema matokeo ya Konde ni ushahidi kuwa yapo baadhi ya maeneo nchini matokeo ya chaguzi hutangazwa kwa hila na anayestahili kushinda hatangazwi.

“Namini baada ya uchaguzi huu wa Konde kutakuwa na maboresho katika maeneo mbalimbali ili tusiingie katika mvurugano wa kisiasa” anasema Said

Anasema CCM walilazimika kuonyesha ukomavu kwa kukubali kushindwa kwakuwa wangeng’ang’ania huenda hali ingekuwa mbaya katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Mwajuma Sued Ali anasema, inashangaza kwamba CCM wanaposhinda, kura zinadaiwa kuibiwa lakini wanaposhinda vyama vingine basi uchaguzi huo unatajwa kuwa huru na haki huku akihoji kwanini kuna kasumba hiyo imejengeka akilini mwa watu.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Juma Rashid Juma akisema “inatakiwa ACT wawe wavumilivu wasione wao ndio wanaonewa, sasa kama na CCM wangelalamika kwamba wameibiwa unadhani tutaenda wapi.”

Mbunge mteule

Mbunge mteule, Issa anasema siku zote uamuzi ya wananchi yangekuwa yanaheshimiwa hata maendeleo ya Zanzibar yangekuwa mbali tofauti na ilivyo sasa.

Anasema haki huwa haipotei bali hucheleweshwa kwahiyo anaamini hata uchaguzi uliofanyika Julai 18 alishinda tena kwa kishindo lakini zilifanyika figisu akatangazwa mwingine.

Anasema katika uchaguzi huu alipewa fomu zote za matokeo katika vituo 16 vilivyotumika kupigia kura tofauti na uchagzui wa mwanzo ambapo hakupewa fomu hizo licha ya kuzidai lakini alinyimwa.

Hata hivyo alisema baada ya uchaguzi kilichobaki ni kupigania maendeleo ya jimbo hilo na katika kuwatumikia wananchi hatajali vyama, kabila wala kitu chochote bali anataka kuleta amendeleo kwa kasi kwa wananchi wote jimboni humo.

“Huu ndio usawa, ninachowaahidi wananchi wa Konde ni kuchapa kazi, tushirikiane kuleta maendeleo ya Jimbo letu na Zanzibar kwa ujumla,” anasema