UCHAMBUZI-Ni hatari kutumia Wi-Fi za bure

Muktasari:

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), imerahisisha mambo mengi duniani kuanzia kuwasiliana, kujifunza, kujiburudisha na hata kufanya biashara za kimtandao.

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), imerahisisha mambo mengi duniani kuanzia kuwasiliana, kujifunza, kujiburudisha na hata kufanya biashara za kimtandao.

Hata hivyo, tahadhari nyingi zimekuwa zikitolewa kuhusiana na wimbi la taarifa za watu kudukuliwa na wahalifu.

Moja ya njia inayokua kwa kasi ya kuwapatia watu huduma za mitandao, ni matumizi ya Wi-Fi ambapo kumekua na wimbi kubwa la huduma hizi kutolewa bure maeneo mbalimbali ya umma.

Katika utafiti mwingi uliofanywa na wanausalama wa mtandao, watu wengi wamekua wakipendelea huduma hii ya bure ya Wi-Fi inayowawezesha kuingia mtandaoni kirahisi na bila malipo.

Uchunguzi uliofanywa na kampuni ya usalama mtandao “Norton” iliyopewa jina la “Norton Wi-Fi risks report” imeeleza kua asilimia 53 ya watumiaji wa Wi-Fi, wanashindwa kutambua huduma salama na isiyo salama.

Wengi wanaotumia Wi-Fi za bure zinazopatikana maeneo ya umma, huzitumia kuingia mitandaoni hufanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuingia katika mitandao ya kijamii, kuangalia barua pepem na wakati mwingine kufanya miamala ya kibenki kupitia mitandao.

Matumizi yote hayo yanaweka taarifa za mtumiaji katika hatari ya kudukuliwa kirahisi na wahalifu mtandao pamoja kusababisha upoteaji wa fedha. Aidha, kupitia kitu kinachoitwa “Packet Sniffing/ Eavesdropping”, mhalifu anaweza kupata taarifa mbali mbali za mtumiaji.

Kwa muda sasa wahalifu mtandao wamekua wakitengezeza Wi-Fi za mtego kwenye maeneo ya umma kwa malengo ya kukusanya taarifa za watu pamoja na kusambaza programu hatarishi (malware) zenye malengo mbalimbali kwenye vifaa vya kielektroniki vitakavyojiunga na Wi-Fi hizo za mtego.

Watumiaji wa Wi-Fi hizo wanapo jiunga na kuanza kuchapisha taarifa zao, wao wanaanza kukusanya taarifa za watu zinazopita kwenye mtandao kupitia njia inayojulikana kitaalam kama “Man In the middle attack” ambapo kila kinachopita mtandaoni, mhalifu mtandao anakua na uwezo wa kukunyaka na baadaye anaweza kutumia taarifa muhimu anazoweza kuzipata kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wizi wa fedha kupitia mtandao.

Bahati mbaya zaidi mbali na mambo ya kibinafsi, kuanzia kipindi cha janga la Uviko-19 hadi sasa ambapo kampuni nyingi zimekuwa zikiruhusu wafanyakazi wake kufanya kazi wakiwa maeneo yoyote, zimejikuta zikipoteza taarifa zao muhimu kutokana na baadhi ya wafanyakazi kupendelea kutumia Wi-Fi za bure kwenye maeneo ya umma.

Hamasa kubwa inatolewa kwa watumiaji kutumia huduma za kimtandao zinazo tolewa na simu zao (mobile data) kwani ndio salama zaidi na inaweza kukupa uwezo wa kuruhusu vifaa vingine vya kielektroniki kujiunga pale unapowezesha “Hotspot” ambayo hufanya kazi mithili ya Wi-Fi.

Ikiwa kutokana na sababu mbalimbali unalazimika kutumia Wi-Fi tofauti na unayoweza kuiwezesha kupitia simu, basi utumie Wi-Fi inayokutaka kuweka nywila (neno la siri) kabla ya kuanza kupata huduma za kimtandao.

Ingawa hakuna mengi unayoweza kufanya ili kufanya Wi-Fi za umma kuwa salama zaidi, unaweza kufanya baadhi ya mambo ili kusaidia kuweka taarifa zako salama kwenye Wi-Fi za umma kwa kutumia programu ya VPN.


Unajilindaje unapotumia Wi-Fi za umma?

Hakikisha unapata maelezo ya kutosha kuhusu programu ya VPN kabla ya kupakua kwani kuna baadhi ya VPN, ambazo hutengenezwa na wahalifu mtandao kwa malengo hasi.

Kupitia Wi-Fi zinazopatikana katika maeneo ya umma, usitumie kuingia kwenye mitandao yenye taarifa zako za kibinafsi au za kifedha. Daima chukulia kuwa

Ili kuwa salama, hakikisha tovuti unayo itembelea imesimbwa kwa njia fiche (ikimaanisha kuwa URL ya tovuti inaanza na https). Ikiwa unafikiri umeingia kwenye tovuti iliyosimbwa kwa njia fiche, lakini ukajikuta kwenye ukurasa ambao haujasimbwa, ondoka mara moja.

Usitumie nenosiri sawa kwenye tovuti tofauti, kwani huko kunaweza kumpa mtu anayepata ufikiaji wa mojawapo ya akaunti zako kufikia akaunti zako nyingi.

Zingatia maonyo. Vivinjari vingi vya tovuti hutoa tahadhari kabla ya kutembelea tovuti ya kitapeli au kupakua programu hasidi. Usipuuze maonyo hayo. Pia hakikisha kivinjari chako na programu za usalama zimehuishwa ( updated).

Badilisha mipangilio ya kifaa chako ili kisiunganishwe bila ridhaa yako kwenye Wi-Fi iliyo karibu. Kwa njia hiyo, utakuwa na udhibiti zaidi wa lini na jinsi ya kutumia Wi-Fi ya umma.

Yusuph Kileo ni mtaalamu wa usalama mtandaoni na mchunguzi wa makosa ya dijitali. Anapatikana: WhatsApp: +254 (0) 702 071 272 | Twitter: @YUSUPHKILEO