Prime
Dosari za kiutaratibu zawaokoa watatu na adhabu ya kifo
Arusha. Mahakama ya Rufaa Tanzania imebatilisha hukumu ya kifo dhidi ya Adamu Sanga, Oscar Mwakapiki na Benjamin Mwasimba, baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha shtaka la mauaji ya dereva wa bodaboda, Aidan Paulo, kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.
Mahakama ilisema kulikuwa na dosari kubwa za kiutaratibu katika uchunguzi na usikilizwaji wa kesi hiyo. Watatu hao walikuwa wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa na Mahakama Kuu Aprili 28, 2023.
Uamuzi huo ulitolewa Juni 8, 2026 katika Rufaa ya Jinai Na. 415 ya mwaka 2023 na jopo la majaji Rehema Mkuye, Sam Rumanyika na Dk Ubena Agatho.
Akisoma hukumu, Jaji Rumanyika alisema mahakama imejiridhisha kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu muhimu za kisheria na kwamba ushahidi wa mashtaka haukuondoa shaka kuhusu ushiriki wa warufani katika mauaji hayo.
Katika Mahakama Kuu, warufani walishtakiwa kwa mauaji kinyume na Kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, wakidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 2, 2019 eneo la Ituha Relini jijini Mbeya.
Kwa mujibu wa mashtaka, Benjamin Mwasimba alimdanganya marehemu kwa kumkodisha kutoka Kituo cha Mabasi cha Soweto kwenda eneo la tukio, huku akiwa amewasiliana na Oscar Mwakapiki. Ilidaiwa Adamu Sanga na mtu mwingine walikuwa wamejificha eneo hilo kumvizia.
Mashtaka yalidai kuwa marehemu aliposimama kumsaidia mtu aliyeonekana kuhitaji msaada, alichomwa kisu tumboni na kujeruhiwa vibaya, hali iliyosababisha kifo chake. Baadaye washtakiwa walidaiwa kuondoka na pikipiki aina ya Kinglion na kumtelekeza eneo hilo.
Aidan aliokolewa asubuhi iliyofuata na wasamaria wema, akiwamo shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri.
Warufani walikamatwa Desemba 2019 na baadaye wakadaiwa kukiri kosa kupitia maelezo ya onyo. Hata hivyo, mahakamani walikana shtaka hilo wakidai walilazimishwa kukiri baada ya kuteswa na polisi.
Katika rufaa yao, walidai kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria kuanzia uchunguzi hadi usikilizwaji wa kesi. Walieleza kuwa walikamatwa Desemba 2019 lakini walifikishwa mahakamani Mei 21, 2020 bila maelezo ya kuridhisha.
Pia walidai mashitaka hayakusomwa kwao kwa karibu miezi 11 na walionyeshwa tu nyaraka muhimu za mashtaka badala ya kuelezwa maudhui yake kama sheria inavyotaka.
Kwa upande wake, Jamhuri iliomba rufaa itupiliwe mbali ikisisitiza kuwa ushahidi uliwaunganisha warufani na tukio hilo.
Baada ya kupitia ushahidi, Mahakama ya Rufaa ilibaini kuwa maelezo ya onyo yaliyotumika kuwatia hatiani hayakupatikana kwa mujibu wa sheria, kwani hayakuonyesha yalitolewa kwa hiari na baadhi yalirekodiwa nje ya muda unaotakiwa.
Mahakama pia ilibaini kuwa mlinzi wa amani aliyerekodi maelezo ya mrufani wa tatu hakuchunguza madai yake ya kuumizwa kabla ya kurekodi maungamo hayo. Kutokana na dosari hizo, maelezo hayo yaliondolewa kwenye rekodi ya ushahidi.
Aidha, majaji walikosoa matumizi ya kanuni ya nia ya pamoja yaliyotumiwa na Mahakama Kuu, wakibainisha kuwa mshukiwa mwingine muhimu aitwaye Venance hakukamatwa wala kufikishwa mahakamani, jambo lililoacha maswali muhimu bila majibu.
Mahakama pia ilisema washtakiwa walinyimwa haki ya kufahamishwa kikamilifu ushahidi uliokusudiwa kutumiwa dhidi yao ili kuandaa utetezi wao. Vilevile, kucheleweshwa kufikishwa mahakamani kwa zaidi ya miezi mitano kulikiuka haki zao za msingi.
Kutokana na kasoro hizo na ukosefu wa ushahidi wa kutosha, Mahakama ya Rufaa iliruhusu rufaa, ikabatilisha hukumu ya hatia na adhabu ya kifo, na kuamuru warufani waachiwe huru mara moja isipokuwa kama wanashikiliwa kwa sababu nyingine halali za kisheria.