Dosari hati ya mashtaka yawaokoa waliohukumiwa kwa ubakaji, ulawiti
Muktasari:
- Vijana hao waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, kwa kosa la ubakaji wa genge na miaka 30 kwa kosa la kulawiti.
Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo wa Dodoma, imebatilisha adhabu ya kifungo cha maisha jela na kifungo cha miaka 30 walichokuwa wamehukumiwa watu wawili walioshtakiwa kwa ubakaji wa genge na ulawiti.
Walioachiwa ni Patrick Manyuli na Samwel Frank ambao awali katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma walishtakiwa kwa makosa mawili ambayo ni ubakaji wa genge kinyume na kifungu cha 130 (1) na 131 A(2) (1) cha Kanuni ya Adhabu na kosa la ulawiti kinyume na kifungu cha 154 (1) (a) cha Kanuni hiyo.
Wote wawili walidaiwa kutenda makosa hayo Desemba 17, 2024 katika eneo la Maili Mbili, mkoani Dodoma kwa binti aliyekuwa na umri wa miaka 19.
Hukumu iliyowaachia huru imetolewa na Jaji Juliana Masabo, Juni 6, 2026 aliyekuwa akisikiliza rufaa namba 5212/2026 iliyokuwa imekatwa na warufani hao waliokuwa wakipinga hukumu ya mahakama ya wilaya Desemba 29, 2025.
Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa hati ya mashtaka iliyotumika katika kesi yao ilikuwa na kasoro zisizotibika zilizofanya mwenendo mzima wa kesi kuwa batili.
Msingi wa rufaa
Awali, warufani hao walikuwa wamepatikana na hatia ya makosa mawili ya ubakaji wa genge na ulawiti ambapo iliwahukumu kifungo cha maisha jela kwa kosa la ubakaji wa genge na miaka 30 kwa kosa la pili, pamoja na kuamuru walipe fidia ya Sh1 milioni kwa mwathiriwa.
Siku ya tukio ilidaiwa kuwa mwathirika wa tukio hilo, alivamiwa usiku akiwa amelala chumbani kwake na wanaume wawili waliovunja mlango na kuingia ndani.
Mashahidi wa upande wa mashtaka waliieleza mahakama kuwa mmoja wa washambuliaji alikuwa na rasta huku mwingine akiwa na nywele fupi.
Wakiwa na bisibisi mkononi, walimtishia mwathiriwa, wakamziba mdomo na kumteka hadi kwenye nyumba ambayo haijakamilika ambako walidaiwa kumbaka kwa zamu na kumlawiti.
Baada ya tukio hilo, ilidaiwa kuwa watuhumiwa walitoroka huku wakimuacha mwathiriwa eneo la tukio. Mwathiriwa alifanikiwa kurejea nyumbani na kutoa taarifa kwa majirani kabla ya kwenda polisi na baadaye kupata matibabu.
Ushahidi uliwasilishwa mahakamani ukionyesha kuwa watuhumiwa walikamatwa na baadaye kutambuliwa katika gwaride la utambuzi lililoandaliwa na Jeshi la Polisi.
Hata hivyo, baada ya kutiwa hatiani na kuhukumiwa, walikata rufaa Mahakama Kuu wakipinga hukumu na mwenendo wa kesi wakiwa na sababu 14.
Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na kudai kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi bila kuacha shaka yoyote.
Pia, walieleza kuwa kulikuwa na sintofahamu kuhusu maelezo muhimu ya ushahidi pamoja na kushindwa kuwaita baadhi ya mashahidi waliokuwa muhimu katika kuthibitisha madai ya upande wa mashtaka.
Walidai kutokuwapo kwa ushahidi wa wapangaji wenza wa mwathiriwa pamoja na ofisa ustawi wa jamii, akidai mashahidi hao walikuwa muhimu katika kuisaidia mahakama kupata picha kamili ya tukio.
Uamuzi Mahakama
Hata hivyo, wakati wa kuandika hukumu yake, Jaji Masabo alibaini suala jingine muhimu ambalo halikuwa miongoni mwa hoja kuu za rufaa, akisema lilikuwa na athari kubwa kwa uhalali wa kesi nzima.
Jaji huyo alieleza kuwa katika hati ya mashtaka, mwathiriwa hakutajwa kwa jina lake kamili bali alitajwa kwa kifupi cha herufi “A.M.” pekee.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, wakati ushahidi ulipokuwa ukiwasilishwa mahakamani, mashahidi mbalimbali hawakumtaja mwathiriwa kwa kifupi hicho.
Baadhi walimtaja kama “mwathiriwa” tu, huku shahidi mmoja akimtaja kwa majina mawili, ila ilibaini hakukuwa na maelezo yoyote yaliyotolewa kuonyesha kuwa kifupi cha “A.M.” kilikuwa kinamhusu mtu huyo aliyetajwa mahakamani au mtu aliyekuwa akirejelewa na mashahidi wengine.
Katika uchambuzi wake, Jaji Masabo amesema jina la mwathiriwa ni sehemu muhimu ya maelezo ya shtaka kwa sababu humwezesha mshtakiwa kuelewa kikamilifu tuhuma zinazomkabili na kuandaa utetezi wake.
Amesema sheria inahitaji hati ya mashtaka kuwa na taarifa zote muhimu zinazohusu kosa linalodaiwa kutendwa ili kuhakikisha haki ya mshtakiwa ya kusikilizwa inalindwa.
“Katika kesi hii rekodi iko kimya kuhusu kama kulikuwa na hali maalumu au amri ya mahakama inayoidhinisha matumizi ya vifupisho badala ya jina halisi la mwathiriwa,” amesema.
Amesema hata kama amri hiyo ingekuwapo, upande wa mashtaka ulipaswa kuhakikisha ushahidi wote unaendana na maelezo yaliyomo kwenye hati ya mashtaka ili kuepusha mkanganyiko.
Mahakama ilisisitiza kuwa pale ambapo ushahidi unaotolewa unatofautiana na maelezo yaliyomo kwenye hati ya mashtaka, upande wa mashtaka una wajibu wa kurekebisha hati hiyo kwa mujibu wa sheria ili iendane na ushahidi unaotolewa.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, kushindwa kufanya hivyo kulisababisha tofauti kubwa kati ya mashtaka yaliyofunguliwa na ushahidi uliowasilishwa mahakamani.
Jaji Masabo alikubaliana na hoja za mawakili wa pande zote mbili kwamba dosari hiyo ilikuwa ya msingi na iligusa haki za warufani kupata usikilizwaji wa haki.
Amesema kasoro hiyo haikuwa ya kiufundi inayoweza kurekebishwa baadaye, bali ilikuwa dosari kubwa iliyoathiri uhalali wa kesi yote tangu mwanzo.
Kutokana na hitimisho hilo, Mahakama Kuu iliamua kuwa mwenendo mzima wa kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma ulikuwa batili kwa sababu ulijengwa juu ya hati ya mashtaka yenye kasoro isiyotibika.
Kwa msingi huo, mahakama ilifuta mwenendo wa kesi, ikafuta hatia zote zilizokuwa zimepatikana dhidi ya warufani na kuweka kando adhabu zote zilizokuwa zimetolewa na kuamuru warufani waachiliwe huru kutoka gerezani mara moja, isipokuwa kama wanashikiliwa kwa sababu nyingine halali kisheria.