Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyekata rufaa kesi ya ubakaji akwaa kisiki Mahakama ya Afrika

Muktasari:

  • Kiture aliyekuwa anatumikia kifungo katika Gereza Kuu la Ukonga jijini Dar es Salaam, alifungua shauri la fidia namba 010/2019 dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akidai haki zake mbalimbali za msingi zilikiukwa katika mwenendo wa kesi yake kuanzia hatua za uchunguzi, usikilizwaji wa shauri mahakamani hadi hukumu



Arusha. Jitihada za Idd Kiture kujinusuru na kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kubaka mtoto wa miaka 12 zimegonga mwamba katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), baada yakutupiliwa mbali ombi lake.

Kiture aliyekuwa anatumikia kifungo katika Gereza Kuu la Ukonga jijini Dar es Salaam, alifungua shauri la fidia namba 010/2019 dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akidai haki zake mbalimbali za msingi zilikiukwa katika mwenendo wa kesi yake kuanzia hatua za uchunguzi, usikilizwaji wa shauri mahakamani hadi hukumu.

Kutokana na hilo, aliomba Mahakama hiyo ya Afrika itamke haki zake za kibinadamu zimekiukwa na alipwe fidia ya Dola 10,000 za Marekani (Sh26 milioni) na kufutwa kwa hukumu na aachiliwe huru.

Hata hivyo, baada ya uchunguzi na usikilizwaji wa pande mbili, Junu 5, 2026 Mahakama hiyo mbele  jopo la majaji wanane wa Mahakama ya Afrika wakiongozwa na rais wa Mahakama hiyo, Blaise Tchikaya pamoja na makamu wa rais, Chafika Bensaoula ilitupilia mbali baadhi ya hoja za msingi na kutamka kuwa  hakukuwa na sababu za kisheria za kufuta hukumu au kumuachia huru.


Kesi ilivyokuwa

Awali, katika shauri hilo, Serikali ya Tanzania iliwasilisha pingamizi ikidai Mahakama ya Afrika haikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Serikali pia ilidai kuwa, Mahakama hiyo haina mamlaka ya kuamuru kuachiwa huru kwa mwombaji.

Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali hoja hizo ikieleza kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 3(1) ya Itifaki ya Mahakama ya Afrika, ina mamlaka ya kusikiliza madai yanayohusu tafsiri na matumizi ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu pamoja na mikataba mingine ya haki za binadamu ambayo Tanzania imeiridhia.

Mahakama pia ilifafanua kuwa Ibara ya 27(1) ya Itifaki inaipa uwezo wa kutoa amri zinazofaa kurekebisha ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwamo kuamuru kuachiwa huru kwa mwombaji endapo mazingira ya shauri yatathibitisha uwepo wa ukiukwaji unaostahili hatua hiyo.

Katika uchunguzi wake kuhusu kupokewa kwa shauri hilo, Mahakama ilikataa hoja ya Tanzania kwamba Kiture alipaswa kwanza kuomba mapitio ya uamuzi wa Mahakama ya Rufani kabla ya kufungua shauri la kimataifa.

Majaji walibaini kuwa mwombaji alikuwa tayari ametumia njia zote za ndani za kisheria baada ya kesi yake kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, Mahakama Kuu ya Tanzania na hatimaye Mahakama ya Rufani, ambayo ndiyo chombo cha juu zaidi cha kimahakama nchini.

Mahakama ilikumbusha kuwa ombi la mapitio ya uamuzi wa Mahakama ya Rufani ni njia ya kipekee ya kisheria ambayo mwombaji hakuwa na wajibu wa kuitumia kabla ya kuwasilisha shauri mbele ya Mahakama ya Afrika.

Katika hoja za msingi, Kiture alidai kuwa alibaguliwa na kunyimwa usawa mbele ya sheria, haki ya kukata rufaa, haki ya kusikilizwa kwa haki, haki ya kusikilizwa ndani ya muda unaofaa pamoja na haki ya kutofanyiwa vitendo vya kikatili au vinavyodhalilisha utu.

Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali madai mengi baada ya kubaini kuwa hayakuungwa mkono na ushahidi wa kutosha.

Kuhusu madai ya ubaguzi na ukosefu wa usawa mbele ya sheria, Mahakama ilisema mwombaji alishindwa kuthibitisha namna haki hizo zilivyokiukwa.

Kadhalika, madai kwamba alinyimwa haki ya kukata rufaa yalikataliwa baada ya kubainika kuwa alitumia kikamilifu haki hiyo hadi Mahakama ya Rufani ya Tanzania.

Mahakama pia ilikataa madai kuwa kesi yake ilicheleweshwa isivyo halali kutokana na kwa mujibu wa hukumu hiyo, muda wa kesi kuanzia Mahakama ya Wilaya hadi Mahakama ya Rufani ulifikia miaka sita, miezi mitano na siku moja, lakini mazingira ya shauri hilo hayakuonesha ucheleweshaji unaoweza kuhesabiwa kuwa ukiukwaji wa haki ya kusikilizwa ndani ya muda unaofaa.

Aidha, Mahakama ilikataa madai kuwa alihukumiwa kwa kutumia hati ya mashtaka yenye kasoro.

Hata hivyo, Mahakama ilibaini kuwepo kwa dosari za kiutaratibu katika hati hiyo, lakini ilisema dosari hizo hazikusababisha dhuluma ya haki kwa sababu mwombaji alifahamu mashtaka yaliyokuwa yanamkabili na aliweza kujitetea ipasavyo.

Madai kwamba alipigwa na kufanyiwa ukatili wakati wa mahojiano ya polisi nayo yalitupiliwa mbali kwa kukosa ushahidi wa kuthibitisha tuhuma hizo.

Hata hivyo, Mahakama ilikubaliana na hoja moja muhimu ya mwombaji kuhusu kukosa msaada wa kisheria.

Majaji walibaini kuwa Kiture hakupata uwakilishi wa kisheria wakati wa kesi yake licha ya kushtakiwa kwa kosa zito la kubaka mtoto wa miaka 12, ambalo adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela.

Mahakama ilieleza kuwa, kwa kuzingatia uzito wa kosa hilo na masilahi ya haki, Tanzania ilikuwa na wajibu wa kumpatia msaada wa kisheria bila malipo hata kama hakuwa ameomba msaada huo.

Kwa msingi huo, Mahakama iliamua kuwa Tanzania ilikiuka haki yake ya kupata msaada wa kisheria kama inavyolindwa chini ya Ibara ya 7(1)(c) ya Mkataba wa Afrika ikisomwa pamoja na Ibara ya 14(3)(d) ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR).

Licha ya kubaini ukiukwaji huo, Mahakama ilisema mwombaji hakuthibitisha kuwa alipata hasara ya mali iliyotokana moja kwa moja na ukiukwaji huo, hivyo ilikataa madai yake ya fidia ya mali.

Badala yake, Mahakama ilibariki kulipwa fidia ya Sh500 za Tanzania kwa madhara ya kimaadili yaliyotokana na kunyimwa msaada wa kisheria. Mahakama pia iliamuru kila upande kubeba gharama zake za shauri.