Rais wa CWT asomewa mashtaka 14 ya rushwa, uhujumu uchumi
Muktasari:
- Wakati rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Suleiman Ikomba, akisomewa mashtaka hayo, James Asagwile ameteuliwa kukaimu kiti cha mweka hazina.
Dodoma. Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Suleiman Ikomba amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma na kusomewa mashtaka 14 yanayohusisha tuhuma za rushwa, kuunda genge la uhalifu na uhujumu uchumi.
Ikomba amefikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu Juni 8, 2026 na ameunganishwa na viongozi wengine wanane wa CWT wanaokabiliwa na mashtaka hayo yaliyofunguliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Awali, wenzake walifikishwa mahakamani Mei 25, 2026, siku ambayo hakuwapo, hivyo leo ameungana na wengine akiwamo aliyekuwa rais wa CWT, Leah Ulaya aliyewahi kuwa katibu Mkuu, Maganga Japhet, Nashon Kidudu (mweka hazina) na katibu mkuu wa sasa, Joseph Misalaba.
Wengine ni Baraka Mbonalibha ambaye katika mashtaka anatajwa kuwa alikuwa mkaguzi wa ndani, Wambura Kihengu, Angelina Wambura pamoja na kampuni ya Pyrite and Industries Company Limited.
Upande wa mashtaka unadai kuwa washtakiwa hao walijipatia Sh2.2 bilioni, kinyume na Katiba ya CWT na pia kujinufaisha na Sh1.3 bilioni kutoka kampuni ya Pyrite and Industries Company Limited kwa lengo la kupitisha zabuni ya kutengeneza fulana na kofia za chama hicho.
Baada ya kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi, Ikomba hakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza na kuamua mashauri hayo katika hatua ya sasa.
Akizungumza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Denis Mpelembwa, Wakili wa Serikali, Gothard Mwingira ameiambia mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
Hata hivyo, Mwingira amesema Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) bado hajatoa kibali cha kuamua kama kesi hiyo itasikilizwa katika mahakama hiyo au kuhamishiwa katika Mahakama ya uhujumu uchumi.
Wakili wa utetezi, Meshack Ngamando amesema hatua ya kuwafikisha washtakiwa mahakamani kabla ya kukamilika kwa upelelezi inawanyima uhuru kwa kuwa wanaendelea kushikiliwa rumande.
“Kati ya mashtaka 14 yanayowakabili, yapo yenye dhamana, hivyo kucheleweshwa kwa upelelezi kunasababisha washtakiwa waendelee kusota rumande wakati kesi ingeanza kusikilizwa na baadhi yao wangekuwa nje kwa masharti ya dhamana na kuhudhuria kesi wakiwa nyumbani,” amesema Ngamando.
Katika uamuzi wake, Hakimu Mpelembwa ameutaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi na kukamilisha taratibu zote zinazohitajika ili shauri hilo lianze kusikilizwa mapema, na kuhakikisha kibali cha DPP kinapatikana ili haki iweze kutendeka.
Wakati hayo yakiendelea Mahakamani, CWT katika kikao chake cha Juni Mosi, 2026 chini ya uongozi wa Makamu wa rais, Shaban Ambindwile kilipendekeza jina la James Asagwile kuwa mweka hazina wao.
Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji Taifa (KUT), kimepewa mamlaka katika Ibara ya 31 (c) ya CWT kufanya uteuzi wa mmoja wa wajumbe wake kuwa mweka hazina wakati Makamu rais na Naibu Katibu Mkuu kamati imewakaimisha nafasi za juu yao.
Kesi ya Temesa nayo yaahirishwa
Wakati huohuo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma imeahirisha kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili watumishi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa) hadi Juni 22, 2026 baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa upelelezi haujakamilika.
Washtakiwa katika shauri hilo ni Lazaro Kilahara, Mathias Rutaguza, Sambayeti Magoko, Kennedy Manene, Peter Bongole, Clavery Busunzu, Mbisho Kinguti, Renatha Juma, Vicent Lutebuka, Michael Assey, Caesar Chambo, Nassoro Igangule, Deus Matiku pamoja na kampuni ya Kentra Tanzania Limited.
Mahakama imeelezwa kuwa pamoja na kutokamilika kwa upelelezi, kibali cha DPP cha kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo bado hakijapatikana.