Mbinu za kukomesha mianya rushwa miradi ya maendeleo
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Francis Chalamila akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Shinyanga.
Muktasari:
- Kwa sasa Takukuru ina ofisi 145 nchini zikiwemo ofisi za mikoa, wilaya na vituo maalumu huku majengo 70 pekee yakiwa yanamilikiwa na taasisi hiyo na majengo 11 yanaendelea kujengwa katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Shinyanga. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Crispin Chalamila ameeleza kuwa uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika kusimamia miradi ya maendeleo ni nyenzo muhimu katika kuziba mianya ya rushwa.
Akizungumza Juni 4, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa ofisi mpya ya Takukuru Mkoa wa Shinyanga iliyofanyika katika ofisi hiyo iliyopo Manispaa ya Shinyanga, Chalamila amesema kuwa uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi itasaidia kuziba mianya ya rushwa.
“Jengo hilo limejengwa kwa gharama ya Sh1,6 bilioni na ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuhakikisha ofisi za Takukuru nchini zinakuwa na makazi ya kudumu yanayokidhi mahitaji ya utendaji kazi wa kisasa.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Francis Chalamila akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa jengo jipya la Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Shinyanga.
“Pia, kwa sasa Takukuru ina ofisi 145 nchini zikiwemo ofisi za mikoa, wilaya na vituo maalumu huku majengo 70 pekee yakiwa yanamilikiwa na taasisi hiyo na majengo 11 yanaendelea kujengwa katika mwaka wa fedha 2025/2026,” amesema Chalamila.
Pia, ameongeza kuwa: “Uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika kusimamia miradi ya maendeleo ni nyenzo muhimu katika kuziba mianya ya rushwa, na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana katika miradi inayotekelezwa. Watumishi tutunze majengo na vifaa vinavyotolewa na Serikali ili viendelee kutoa huduma kwa muda mrefu na kuleta tija iliyokusudiwa.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro ambaye akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema jengo hilo ni uwekezaji muhimu utakaoongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa katika mkoa huo, akisisitiza vita dhidi ya rushwa vinahitaji ushiriki wa kila mwananchi na si jukumu la Takukuru pekee.
“Vita dhidi ya rushwa vinahitaji ushiriki wa kila mmoja wetu, tujenge utamaduni wa kupinga rushwa kwa vitendo katika jamii zetu, pia, jengo hili liwe kitovu cha haki, uwajibikaji na uadilifu kwa wananchi wetu na maeneo jirani,” amesema Mtatiro.
Muonekano wa jengo jipya la ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Shinyanga.
Naye, Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Erenestina Richard, akimwakilisha Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, ameipongeza Takukuru kwa juhudi zake katika mapambano dhidi ya rushwa na kuomba taasisi hiyo kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu kwa wananchi wa vijijini.
“Wananchi wengi wa maeneo ya vijijini bado wanahitaji elimu zaidi kuhusu madhara ya rushwa na namna ya kushiriki katika kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa, tunaiomba Takukuru kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wa vijijini ili waelewe madhara ya rushwa na wajibu wao katika kuzuia vitendo hivyo,” amesema Erenestina.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi, Mkurugenzi wa Milki wa Takukuru, Dk Emmanuel Kiyabo, amesema ujenzi wa jengo hilo ulitekelezwa kwa kipindi cha miezi 10 kwa gharama ya Sh1.6 bilioni, ukihusisha ujenzi wa jengo lenye ghorofa moja na miundombinu mingine muhimu na samani za kisasa kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi.