Prime
Mirungi kutoka Ethiopia ilivyomsotesha gerezani siku 2,465
Dar es Salaam. Zilikuwa ni siku 2,465 za mfanyabiashara wa Sakina Jijini Arusha, Taqabbal Mwasha kuwa nyuma ya kuta za gereza, akipigania haki ya kuwa hana hatia katika tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kutoka Ethiopia na kwenda Uingereza.
Hii ni kuanzia Septemba 5, 2019 alipokamatwa na maofisa wa Mamlaka ya Dawa za Kulevya (DCEA) Jijini Dar es Salaam hadi Juni 5, 2026 Mahakama Kuu Divesheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, ilipomwachia huru kuwa hana hatia.
Siku hiyo, Taqabbal alikamatwa katika kitengo cha kusafirisha vifurushi ya Shirika la Posta Tanzania, Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam, akidaiwa kusafirisha kilo 214.85 za dawa za kulevya aina ya mirungi kutoka Ethiopia na kwenda Uingereza.
Lakini alikanusha tuhuma hizo kuanzia siku aliyokamatwa na maofisa hao na kupelekwa polisi.
Akiwa mahakamani aliendelea kuzikanusha tuhuma hizo, hadi Juni 5, 2026 Jaji Sedekia Kisanya wa Mahakama hiyo alipomwachia huru.
Katika hukumu yake iliyowekwa katika tovuti ya Mahakama Jumamosi ya Juni 6, 2026, Jaji Kisanya alisema upande wa mashitaka ulikuwa umeshindwa kutimiza jukumu lake la kuthibitisha shitaka dhidi yake pasipo kuacha shaka.
“Kwa kuzingatia uchambuzi wa ushahidi wa pande mbili, Mahakama imeona kwamba upande wa mashtaka haujatoa mzigo wa ushahidi unaohitajika katika kesi za jinai, yaani ushahidi usio na shaka,”alisema Jaji Kisanya.
“Upungufu wa ushahidi, kutofautiana kwa mashahidi na shaka ambayo haijatatuliwa katika kesi ya mashtaka lazima, kisheria, itatuliwe kwa faida au upendeleo wa mshtakiwa, ambaye amekana kuhusika na kielelezo P3.”
“Kwa hiyo, mshitakiwa, Taqabbal Ayoub Mwasha, hakupatikana na hatia kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya kama ilivyodaiwa.”
“Mahakama pia inaamuru mshtakiwa achiliwe huru mara moja, isipokuwa kama anashikiliwa kwa kosa lingine. Arudishwe pasipoti yake na kwamba dawa za kulevya zinazoshikiliwa na DCEA ziharibiwe kwa mujibu na sheria,”anasisitiza Jaji.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka, uliongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali Elizabeth Muhangwa akisaidiwa na mawakili wa Serikali ambao ni Marietha Maguta, Glory Kilawe, Blandina Mnung’a, Erick Davies na Erick Kamala.
Upande wa mashitaka uliita mashahidi 10 na kutoa vielelezo 10 katika kujaribu kuthibitisha kesi yake huku mshtakiwa awali akitetewa na wakili wa kujitegemea Benjamin Mageni na baadaye akatetewa na Wakili Mohamed Majaliwa.
Alivyokamatwa
Kulingana na ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri, matukio yaliyosababisha kukamatwa kwa Taqabbal yalianzia kwa shahidi wa sita, Gabriel Seleman ambaye ni ofisa usalama na nchunguzi katika Ofisi ya Shirika la Posta jijini Dar es Salaam.
Alieleza kuwa Agosti 23, 2019 akiendelea na majukumu ya kukagua vifurushi kwa mashine alibaini vifurushi vitatu ambavyo alivitilia shaka na moja ya kifurushi hicho kilikuwa kina jina la Taqabbal A. Mwasha.
Picha, alizoziona katika mashine zilitoa ishara zote kuwa ndani ya kifurushi kulikuwa na majani hivyo alimjulisha mkuu wa idara ambaye alimtaka kuvitenga na kuwajulisha maofisa wa DCEA waliofika na kuchukua taarifa za mtumaji.
Baada ya kuchukua taarifa hizo, maofisa hao waliondoka na yeye akapeleka vifurushi hivyo katika stoo ya ulinzi kwa ajili ya kuvihifadhi na kuvitunza.
Siku sita baadaye, Agosti 29,2019, shahidi huyo alikutana na maboksi mengine 10 yakitokea Addis Ababa Ethiopia kwenda Arusha huku mpokeaji akiwa ameandikwa Taqabbal Ayoub Mwasha na mashine ilibaini uwepo wa majani.
Shahidi huyo akamjulisha mkuu wake wa kazi ambaye alimtaka awajulishe DCEA na alifanya hivyo na walifika na kuchukua anuani za mpokeaji wa mizigo hiyo.
Siku iliyofuata, Agosti 30 2019, shahidi huyo alipokea tena maboksi mengine mawili yakitokea Arusha kwenda Uingereza, yalikuwa na jina la mtumaji ambaye ni Taqabbal Ayoub Mwasha na hayakuwa na vibali vya kusafirisha mimea.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa Septemba 5, 2019, baada ya kubaini kuwa mizigo yake haijafika kule ilipokuwa inakwenda, mshitakiwa alifika ofisi za Posta kati ya saa 4:00 na 5:00 asubuhi kuulizia mizigo yake iko wapi.
Baada ya kufika, alikutana na shahidi namba 4, Selestine Nyoni ambaye baada ya kushauriana na shahidi namba sita, walimjulisha ni kweli kuna maboksi 10 kutoka Ethiopia na maboksi mengine matatu yaliyokuwa yamezuiwa ofisini hapo.
Siku hiyo hiyo baadaye, shahidi namba nane Eva Moshi na Juliana Komba nao walithibitisha juu ya uwepo wa mizigo mitatu iliyotumwa kutoka Arusha na baada ya kuwasiliana na mkuu wao wa kazi, waliamua kuachilia mizigo hiyo.
Lakini siku hiyo hiyo saa 9:00 alasiri, shahidi namba saba, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Lubambe Kinyumbu kutoka DCEA alipokea taarifa ya uwepo wa mshitakiwa katika ofisi hizo kwa ajili ya kuchukua mizigo inayoshukiwa kuwa na dawa hizo.
ASP Kinyumbu na makachero wengine wa DCEA walifika katika ofisi hizo na walidai walipofika walikuta mshitakiwa akiwa na mizigo hiyo, alikamatwa na upekuzi na baadae uchunguzi wa kimaabara ulithibitisha ilikuwa na dawa hizo.
Akijitetea kortini kama shahidi pekee wa utetezi, Taqabbal, alieleza kuwa Septemba 5,2019 alikwenda ofisi za Posta Dar es Salaam baada ya kupigiwa simu na mmoja wa maofisa akijulishwa kuwa kuna matatizo katika mizigo yake.
Baada ya kufika katika ofisi hizo alikamatwa na maofisa wa DCEA wakimtuhumu kusafirisha dawa za kulevya, tuhuma ambazo alizikanusha wakati anakamatwa na maofisa hao na aliendelea kuzikanusha hata alipofikishwa mahakamani.
Kulingana na yeye, vitu pekee ambavyo vilichukuliwa kutoka kwenye mfuko wake na begi dogo alilokuwa nalo ni pamoja na simu mbili za kiganjani, risiti ya EFD, fedha taslimu na nyaraka nyingine na vitu hivyo vilirekodiwa katika kielelezo D3.
Alikanusha umiliki, kukutwa navyo au kuwa na ufahamu na maboksi 13 ambayo ni kielelezo P3 yanayodaiwa kuwa na dawa za kulevya na kwamba yeye alionyeshwa tu maboksi hayo baada ya kuwa kukamatwa na kuambiwa yeye ndio mmiliki.
Mshitakiwa huyo alikanusha pia kuwahi kupokea maboksi kutoka Ethiopia au kupokea yaliyokuwa yakisafirishwa kwenda Uingereza.
“Ingawa alikiri kujishughulisha na biashara ya mazao ya misitu na huko nyuma aliwahi kusafirisha bidhaa kutoka Arusha hadi Uingereza,alishikilia kuwa hakuwa na uhusiano wowote na maboksi 13 yaliyotolewa kama ushahidi,”alisema Jaji.
“Mshitakiwa pia ilipinga ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka ambao walidai kwamba vifurushi vya maboksi 10 vimekabidhiwa kwake kwenye ofisi ya Posta au kwamba alikuwa amefanya malipo kuhusiana nao,”alieleza Jaji.
Hukumu ya Mahakama
Katika hukumu yake, Jaji Kisanya alisema ni suala kuu linalopaswa kutolewa uamuzi na Mahakama hiyo ni kama upande wa mashtaka umetekeleza wajibu wake wa kuthibitisha mashtaka dhidi ya mtuhumiwa pasipo shaka yoyote.
Jambo la kwanza kwa mujibu wa jaji ni kuamua endapo kielelezo P3 cha upande wa mashitaka kilithibitishwa kweli ni dawa za kulevya aina ya mirungi, lakini kwa maoni yake sheria na miongozo ya uchukuaji wa sampuli haikuzingatiwa.
“Kimsingi kielelezo P3 juu ya kujumlisha na kuchanganya, bila kuoneshwa kufuata sheria na ulinzi wa kisayansi unaosimamia utaratibu huo,” alisema jaji katika hukumu yake hiyo na kuongeza:
“Upungufu huu sio tu utaratibu katika asili, lakini unakwenda hadi kwenye mzizi wa kutegemewa kwa uchambuzi wa mahakama ambayo upande wa mashtaka unategemea kujenga kesi yao,”anasema.
“Kwa kukosekana kwa kufuata mfumo uliowekwa wa sampuli, Mahakama hii haiwezi kukubali kwa usalama kwamba kila kifurushi ndani ya masanduku yote ni mirungi. Dosari hizo zinakwenda hadi kwenye mzizi wa kesi hii.”
Jaji alisema ni jambo lisilobishaniwa kwamba upekuzi ambao ndio kilele cha kukamatwa kwa kielelezo P3 kulifanyika bila agizo la upekuzi iliyotolewa ama na Kamishna Jenerali au na afisa aliye chini ya mamlaka yake.
“Katika mazingira hayo, Mahakama inapata ugumu kukubali ushahidi wa shahidi namba saba kwa madai kuwa upekuzi ulipaswa kufanywa mara moja kwa sababu inasemekana mshitakiwa alikuwa ni mtu aliyekaribia kuondoka eneo hilo,” alisema.
“Katika mazingira haya Mahakama hii inashikilia kuwa hakuna msingi wa ukweli unaoweza kuusamehe upande wa mashitaka kushindwa kupata hati ya upekuzi chini ya kifungu cha 43 cha CPA (Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai).”
“Upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kuwepo kwa mambo ya kipekee unaohalalisha kuondoka kwa utaratibu wa kawaida, upekuzi na ukamataji wa kielelezo P3 na hauwezi kusemwa kuwa ulifanywa kwa mujibu wa sheria.”
Ni kutokana na uchambuzi wa ushahidi wa upande wa Jamhuri, Mahakama inaona upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya mshitakiwa kwa viwango vinavyokubalika hivyo inamwachia huru mara moja.