Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi Pwani wakamata watuhumiwa 261, mirungi na silaha

Kamanda Wa Polisi Mkoa wa Pwani Salim Morcase akizungumzia na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 8, 2026. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata watuhumiwa 261 kwa makosa mbalimbali ya jinai katika operesheni zilizofanyika kati ya Machi na Aprili 2026. Polisi pia walikamata silaha tano, mirungi, bangi, nyara za Serikali pamoja na magari yaliyokuwa yakikiuka sheria za usalama barabarani.

Kibaha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata watuhumiwa 261 kwa makosa mbalimbali ya jinai katika operesheni na misako maalumu iliyofanyika kati ya Machi na Aprili 2026.

Akizungumza Mei 7, 2026 mjini Kibaha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase amesema operesheni hizo zililenga kuimarisha usalama wa raia na mali zao pamoja na kudhibiti vitendo vya uhalifu mkoani humo.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, polisi walifanikiwa kukamata silaha tano zilizokuwa zikitumika kinyume cha sheria, zikiwemo gobole moja lisilo na namba za usajili, rifle moja ya kutengenezwa kienyeji na bunduki tatu aina ya Marker IV pamoja na risasi zake.

Katika oparesheni hizo, Aprili 28, 2026 askari waliokuwa doria eneo la Dagaza, Kata ya Zinga wilayani Bagamoyo walikamata gari aina ya Alphard lililokuwa na mifuko tisa ya sandarusi iliyoficha mirungi bunda 419 zenye uzito wa kilogramu 315.

Aidha, Aprili 29, 2026 katika kizuizi cha Maliasili eneo la Msata wilayani Chalinze, watuhumiwa wawili kutoka Korogwe mkoani Tanga walikamatwa wakisafirisha mirungi bunda 548 zenye uzito wa kilogramu 387.31 kutoka Kilimanjaro kwenda Dar es Salaam kwa kutumia gari aina ya Toyota Land Cruiser.

Polisi pia walikamata kilogramu 98.3 za mirungi, kilogramu 62.7 za bangi pamoja na lita 781 za pombe haramu aina ya moshi na mitambo mitatu ya kutengenezea pombe hiyo katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Pwani.

Kwa upande wa nyara za Serikali, watuhumiwa tisa walikamatwa wakiwa na vipande sita vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 42, nyama pori, miguu ya pundamilia pamoja na mikia ya twiga na nyumbu.

Jeshi hilo pia lilifanikiwa kuokoa mali mbalimbali za wananchi, zikiwemo televisheni sita, pikipiki 41, magari matano, kompyuta mpakato moja, lita 220 za mafuta ya dizeli pamoja na vifaa vingine.

Katika usalama barabarani, madereva 25 walifungiwa leseni huku wengine 40 wakifikishwa mahakamani kwa kukiuka sheria za usalama barabarani.

Aidha, magari 322 yaliyokuwa yakielekea nchi jirani yalikamatwa kwa kosa la kubeba abiria kinyume cha sheria. Kamanda Morcase amesema magari hayo ya IT hayaruhusiwi kisheria kupakia abiria.

Kwa mujibu wa polisi, kati ya kesi 197 zilizofikishwa mahakamani, kesi 130 zilimalizika kwa watuhumiwa kutiwa hatiani na kuhukumiwa vifungo mbalimbali.

Miongoni mwa waliohukumiwa ni Stephano Anyosisye Mwasala aliyefungwa kifungo cha maisha jela, Isihaka Christopher Njometi aliyefungwa miaka 60, pamoja na Munijadi Hamadi Abdallah aliyefungwa miaka 30 kwa makosa mbalimbali yakiwemo ubakaji.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limetoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.