Wimbi la mirungi lashtua, basi la abiria lakutwa na kilo 101
Muktasari:
- DCEA yakamata zaidi ya tani moja kwa mwezi mmoja za mirungi iliyoingizwa kutoka nchi jirani, yakamata pia msimamizi wa hosteli iliyokutwa na skanka.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imebaini ongezeko kubwa la ukamataji wa dawa za kulevya aina ya mirungi, hali inayozua hofu mpya kuhusu kuibuka kwa mitandao mipya ya usafirishaji, hususan kutoka maeneo ya mipakani kuelekea miji mikubwa.
Taarifa ya DCEA inaonesha kwamba Machi 2026 pekee, jumla ya kilogramu 1,267.12 za mirungi zilikamatwa, sawa na asilimia 64 ya dawa zote za kulevya zilizokamatwa katika kipindi hicho.
Akizungumza leo Jumatatu, Aprili 13, 2026, jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema katika operesheni zilizofanyika nchi nzima ndani ya Machi, mamlaka hiyo imekamata kilogramu 1,983.31 za dawa mbalimbali za kulevya, pamoja na kilogramu 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu.
Pikipiki ikiwa imekamatwa na mzigo wa mirungi wakati wa operesheni iliyofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya mwezi Machi.
Aidha, vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya vilikamatwa, huku ekari 55.5 za mashamba ya bangi zikiteketezwa.
Sambamba na hilo, watuhumiwa 77 walikamatwa, na vyombo vya usafiri vilivyotumika katika uhalifu huo vikiwemo magari tisa, pikipiki 12 na bajaji moja vilikamatwa.
Lyimo amesema uchambuzi wa mwenendo wa ukamataji unaonesha kuwa ongezeko hilo la mirungi linatokana na mkakati wa DCEA kuelekeza nguvu katika operesheni za mashambani, baada ya kudhibiti kwa kiasi kikubwa mitandao ya dawa za kulevya za viwandani.
Amesema hatua hiyo imeibua taswira mpya ya vita dhidi ya dawa za kulevya, na wahalifu wamezidi kubadili mbinu kwa kutumia njia zisizo za kawaida kusafirisha bidhaa hizo haramu.
“Matokeo ya operesheni za Machi yamefichua uwepo wa mitandao mipya na mbinu mpya za usafirishaji. Mwenendo huu unaonesha wazi kuwa wahalifu wanabadilika kulingana na mazingira, lakini nasi tunaendelea kuimarisha mikakati ya kukabiliana nao,” amesema Lyimo.
Mtuhumiwa Alphonce Martini Mitema akiwa na vifurushi vya mirungi alivyokamatwa navyo na maafisa wa DCEA akiwa amevifunga mwilini, mkoani Tanga.
Katika operesheni iliyofanyika jijini Dar es Salaam eneo la Tegeta Kibo, dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 101.2 zilikutwa zimefichwa ndani ya basi la abiria aina ya Yutong la kampuni ya Abood lililokuwa likisafiri kutoka Mombasa, Kenya kwenda Dar es Salaam.
“Dawa hizo zilifichwa kwa ustadi mkubwa ndani ya mfumo wa hewa (AC) wa basi hilo pamoja na sehemu nyingine, hatua iliyolenga kukwepa ukaguzi wa kawaida.
“Watuhumiwa waliokamatwa ni dereva Ramadhan Mohamed (52), kondakta Salma Sanga (26), pamoja na abiria watatu Twahilu Athuman (38), Mohamedy Mikidadi (37) na Ibrahim Mohamed (39),” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Mirungi pia imekamatwa katika mikoa mbalimbali. Mkoani Pwani, kilo 419.09 za mirungi zilikamatwa zikiwa njiani kuelekea Dar es Salaam, wakati mkoani Mwanza, kilo 52 zilikamatwa katika kizuizi cha Magu na Bandari ya Mwanza South.
Katika tukio hilo la Mwanza, mirungi hiyo ilisafirishwa kwa gari aina ya Fuso ikiwa imefichwa katikati ya mizigo ya mitumba.
Wilayani Misungwi, pia mkoani humo, kilo 184.9 za mirungi zilikamatwa ndani ya nyumba ya wanandoa Chrispin Shoo (62) na Esther Pastory (55), huku zikipatikana pia kwenye magari mawili.
Mkoani Tanga, kilo 32.95 za mirungi zilikamatwa zikiwa zimechanganywa na maembe ndani ya mfuko, huku mtuhumiwa Seif Omar (38), maarufu kama Haniwao, akikamatwa.
Mirungi pia imekamatwa Arusha, wilayani Longido, ambapo kilo 106.25 zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kwa gari aina ya Toyota Wish, huku watuhumiwa wawili, akiwemo diwani wa Kimokouwa, Solomon Koholo (38), wakikamatwa.
Katika hatua nyingine, mamlaka hiyo imekamata paketi 141 za bangi aina ya skanka zilikamatwa ndani ya hosteli ya wanafunzi katika mtaa wa Nzasa, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
“Tunaona jinsi matumizi ya bangi, hasa hii aina ya skanka, yanavyozidi kushamiri kwa vijana wetu wakiwemo wanafunzi wa vyuo. Katika tukio hili tumemkamata Semvua Sangi (31), msimamizi wa hosteli hiyo.
“Niendelee kutoa wito kwa vijana na jamii kwa ujumla, tuwe makini kuhakikisha tunatokomeza biashara ya dawa za kulevya katika maeneo yanayozunguka taasisi za elimu, kinyume na hivyo itakuwa hatari kwa mustakabali wa vijana,” amesema.
Mamlaka hiyo pia kwa kushirikiana na taasisi nyingine ilifanya ukaguzi katika kampuni za kemikali, maduka ya dawa na bandari kavu na kubaini uwepo wa kemikali bashirifu zinazotumika kutengeneza dawa tiba za kulevya.
Ukaguzi huo uliwezesha kukamata kilo 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu, zikiwemo potassium permanganate, hydrochloric acid, acetone na sulphuric acid.