Mbunge CCM ataka mirungi iwe zao halali, ahoji waliotunga sheria kuita dawa za kulevya
Mbunge wa Kondoa Mjini (CCM), Mariam Ditopile akizungumza bungeni Dodoma. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Katika mchango wake, mbunge huyo ameanza kwa kueleza kuwa, katika mchango wake wako watakaombeza na wengine watamuunga mkono lakini kwake hajali ila anataka kulisaidia Taifa kupata mapato.
Dodoma. Mbunge wa Kondoa Mjini (CCM), Mariam Ditopile ameitaka Serikali kuhalalisha mirungu ili iweze kusaidia kwenye pato la nchi.
Mbali na takwa lake, lakini amehoji Bunge lililopitisha sheria ya kuzuia zao hilo la kuliweka kwenye kundi la dawa za kulevya lilitumia kigezo kipi kwani anaamini mirungu ni salama.
Ditopile ametoa kauli hiyo leo Jumatano Aprili 29, 2026 wakati akichangia kwenye hotuba bajeti ya Kilimo na akaomba asaidiwe kupitia kumbukumbu rasmi za kibunge kujua nani alipendekeza hilo.
Katika mchango wake, Mbunge huyo ameanza kwa kueleza katika mchango wake wako watakaombeza na wengine watamuunga mkono lakini kwake hajali ila anataka kulisaidia Taifa kupata mapato.
Amepinga kauli za kuwa mirungi inasababisha saratani au magonjwa mengine badala yake amehoji iweje namna hiyo wakati kuna pombe kali ambazo zinaruhusiwa na hakuna historia kwamba kuna mtu aliwahi kutumia mirungi akashika panga kuumiza mtu.
“Mheshimiwa mwenyekiti katika mchango wangu ninaokwenda kuutoa najua wengine watanibeza lakini baadhi watanielewa, hapa nataka kulisaidia taifa langu ili lisiendelee kupoteza mapato,” amesema Ditopile.
Mbunge huyo amesema kitendo cha kuendelea kulifanya zao hilo kuwa la gizani, ni kunufaisha mataifa jirani ambayo kwao yamehalalisha lakini Tanzania inatumiwa kama njia.
Ametolea mfano wa Kenya na Somalia wanapata fedha nyingi za kutosha kutokana na ushuru utokanao na mirungu baada ya kuhalalishwa lakini akataja kuwa duniani zao la mirungu linachangia zaidi ya dola 3 bilioni.
Wakati akichangia, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara alikuwa akiomba kumpa taarifa lakini mwenyekiti wa Bunge, Nagma Giga alimzuia akieleza muda wa mchangiaji ulikuwa umekwisha.
Hata hivyo, Giga alimweleza Ditopile mchango wake hauwezi kujibiwa na Waziri wa Kilimo kwa kuwa unagusa suala la sheria na wizara nyingine na mchangiaji alisema ingawa anajua lakini ujumbe umefika na akaeleza kwenye suala la hoja linaweza kufikiwa kwa namna yoyote.