Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Upelelezi umekamilika kesi ya Najim na mkewe wanaodaiwa kusafirisha kilo 3,000 za 'unga'

Mshtakiwa Najim Mohamed na Juma Abas wanaodaiwa kusafirisha kilo 3050 za Heroine na Methamphetamine, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

Muktasari:

  • Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha heroini yenye uzito wa kilo 882.71 na Methamphetamine yenye uzito wa kilo 2167.29, tukio wanalodaiwa kulitenda Desemba 15, 2023 eneo la Kibugumo Shule, wilayani Kigamboni

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kusafirisha shehena ya kilo 3,050 za dawa za kulevya, inayomkabili mfanyabiashara Najim Mohamed(52) na mkewe Maryam Najim Mohamedi (50) pamoja na  mfanyakazi wa ndani, Juma Abbas(37), umekamilika.

Mohamed na wenzake anakabiliwa na kesi ya uhujumu namba 53 ya mwaka 2023 yenye mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 882.71 na Methamphetamine zenye uzito wa kilo 2167.29.

Washtakiwa hao, wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mahakama hiyo imepanga Juni 12, 2026, washtakiwa hao watasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo   na kisha kesi hiyo ihamishiwe Mahakama Kuu.

Leo, Jumatatu Juni 8, 2026 kesi hiyo imeitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuwasomewa washtakiwa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Wakili wa Serikali, Judith Msenga ameieleza Mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wakati kesi hiyo ilipoitwa.

Hata hivyo, mshtakiwa Najim hakuletwa Mahakama hapo kutokea mahabusu, wakati kesi hiyo ilipotajwa, huku mkewe Maryam na Abas, wao walikuwepo mahakamani hapo.

Mshtakiwa Maryam Mohamed, anayekabiliwa na kesi ya kusafirisha dawa za kulevya akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

"Mheshimiwa hakimu, hapa mahakamani naona mshtakiwa wa pili na watatu, lakini mshtakiwa wa kwanza (Najm) hajaletwa kutokea mahabusu, hivyo tunaomba tupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea maelezo yao na ya mashahidi," amedai wakili Msenga.

Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza maelezo ya Jamhuri alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha hadi Ijumaa, Juni 12, 2026 kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo yao.

"Kesi naiahirisha hadi Ijumaa na pia natoa hati ya kuwaita washtakiwa wote wa kesi hii, siku hiyo waletwe mahakamani hapa kwa ajili ya Jamhuri kuwasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo," amesema Hakimu Lyamuya.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Desemba 29, 2023 na kusomewa kesi hiyo, ambayo hawakutakiwa kujibu chochote.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Desemba 15, 2023 katika eneo la Kibugumo Shule lililopo wilaya ya Kigamboni, walisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 882.71.

Shtaka la pili, siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zenye uzito wa kilo 2167.29.