Uchawa, utamaduni CCM vinavyojenga presha urais wa Samia muhula wa pili

Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa katika moja ya ziara zake

Muktasari:

Januari 2, 2024, mkutano mkuu wa CCM, wilaya ya Ruangwa, Lindi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema “fomu iwe moja” katika chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025. Mlengwa wa fomu hiyo ni Rais Samia Suluhu Hassan.

Karne ya 19, marais watatu wa Marekani, John Tyler, Andrew Johnson na Chester Arthur, walikumbana na upinzani ndani ya vyama vyao, walipokuwa wanawania urais muhula wa pili.

Tyler, Rais wa 10 wa Marekani, alishika usukani alipofariki dunia Rais wa tisa, William Harrison.

Johnson, Rais wa 17, aliapishwa baada ya kifo cha Rais wa 16, Abraham Lincoln. Arthur, Rais wa 21, aliingia madarakani kufuatia kifo cha Rais wa 20, James Garfield.

Tyler, Johnson na Arthur, wote walikuwa Makamu wa Rais, kisha wakawa marais baada ya vifo vya watangulizi wao.

Walidhibitiwa na vyama vyao kugombea mihula ya pili, sababu ikielezwa hawakupata uungwaji mkono wa kutosha, maana walikuwa wagombea wenza. Hawakuwa wagombea kamili.

Matokeo yake, vyama vyao, Whig (Tyler), Democratic (Johnson) na Republican (Arthur), vilipoteza uchaguzi. Sababu ya kushindwa ni moja; mgawanyiko ndani ya vyama.

Karne ya 21, sauti nyingi zinasikika kadiri Tanzania inapoelekea kwenye misimu ya uchaguzi. Huu ni mwaka 2024, uelekeo wa nchi ni Uchaguzi wa serikali za mitaa. Mwaka ukigota 2025, itakuwa Uchaguzi Mkuu.

Januari 2, 2024, katika mkutano mkuu wa CCM, wilaya ya Ruangwa, Lindi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema “fomu iwe moja” katika chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025. Mlengwa wa fomu hiyo ni Rais Samia Suluhu Hassan.

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana alisema utamaduni wa chama hicho utaendelezwa kwa Rais madarakani kuongezewa muhula wa pili. Aliongeza kwamba hakuna sababu ya kumzuia Rais Samia kuongoza muhula wa pili.

Kinana ameweka vizuri; rais madarakani atokanaye na CCM kupita bila kupingwa kuelekea muhula wa pili ni la kiutamaduni. Si haki ya Rais kutopingwa. Ni utamaduni wana-CCM kumwacha mwanachama mwenzao aende kushindana na vyama vingine kuwania muhula wa pili.

Utamaduni na uchawa

Utamaduni wa CCM unafahamika. Hata hivyo, isiwe sababu ya kuminya demokrasia. Anapotokeza mwana-CCM mwenye utashi wa kumpa changamoto Rais aliye madarakani, atendewe haki. Demokrasia inapaswa kuwa na nguvu kuliko utamaduni.

Kelele za kutotaka Rais Samia asipingwe, zimekuwa na upacha wa hali ya juu na uchawa. Lipo kundi halisemi “fomu moja” kwa sababu ya kutetea utamaduni wa CCM, bali ni majaribio yao ya kuingia kwenye kitabu kizuri cha Rais Samia.

Je, kuna watu wanajipanga kumdhibiti Rais Samia au ni hofu ya kisichokuwepo? Ni watu wenye nia njema ya kumsafishia njia Rais Samia au wanabweka kumzubaisha tajiri, aone wapambanaji wapo kazini?

Mayowe kama haya yalikuwepo kipindi cha Rais wa awamu ya tano,  John Magufuli. Sauti zikasikika nyingi kuwa kulikuwa na watu walijipanga kumhujumu. Matokeo yake, kelele hizo hazikumsaidia, zaidi zilijenga chuki na uhasama ndani ya chama.

Mayowe yalipoanza CCM, matamko ya watu waliojipambanua kuwa watetezi wa Dk Magufuli, ilionekana ni vita dhidi ya hofu ya mambo ambayo hayakuwepo.

Hata hivyo, dunia ni ileile ambayo wahenga walitahadharisha kuwa “mzaha mzaha hutumbua usaha.”

Tamko lilipotoka kuwa Magufuli anahujumiwa, usaha ukatunga. Matamko yalivyoendelea, jipu nalo likavimba. Mwishowe, usaha ulipotumbuka, ikawa dhahiri CCM ilikuwa na mpasuko. Makatibu wakuu wa zamani, Yusuf Makamba na Kinana, ikabainika hawakuiva chungu kimoja na Magufuli.

Kinana na Makamba, waliandika waraka kulaumu kuwa walisemwa maneno mabaya na mtu aliyelindwa na nguvu isiyohojiwa na yeyote. Maneno hayo moja kwa moja yalimgusa Magufuli, ambaye ndiye alikuwa Rais, kwamba aliwalinda waliowashambulia.

Ongezea nyakati za kuvuja kwa sauti za wenye kumteta Magufuli.Hata sasa, inawezekana kelele zinavyopigwa, ndivyo usaha unatungwa. Kuna watu wataparuriwa. Utakapowadia muda wa wajeruhiwa kujitokeza, kitakuwa kipimo cha usaha kutumbuka. CCM wajiepushe na mzaha-mzaha.

Usaha ulipotumbuka sawasawa CCM, Membe alitangaza hadharani nia ya kumpinga Magufuli. Matokeo yake, Membe alifukuzwa uanachama. Alikimbilia ACT Wazalendo, alikopewa tiketi ya kuwa mgombea urais.

Dunia ilishuhudia kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ulivurugwa. Kama ungekuwa huru na haki, ni vigumu kupima matokeo yangekuwaje na CCM ingeathirika kiasi gani kwa namna usaha ulivyotumbuka ndani ya chama, tena kumwelekea Rais ambaye ndiye alikuwa mgombea mkuu.

Tahadhari ya kihistoria

Vikwazo ambavyo Tyler, Johnson na Arthur, walikutana navyo Marekani Karne ya 19, ndicho hichohicho kilichomharibia Gerald Ford, alipowania muhula wa pili wa urais Marekani, karne ya 20. Hoja ni ileile, hakupata uungwaji mkono wa kutosha kwenye chama, maana awali walikuwa wagombea wenza.

Ford, Rais wa 38, alishika usukani baada ya Rais wa 37, Richard Nixon, kulazimishwa kujiuzulu kwa kashfa ya Watergate. Upekee wa Ford ni kwamba hakuwa hata mgombea mwenza, aliapishwa kuwa Makamu wa Rais kufuatia aliyekuwa mtangulizi wake, Spiro Agnew, kujiuzulu kutokana na kubainika kutenda makosa ya rushwa.

Ford, alikuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Kiongozi wa Upinzani (Leader of Minority). Agnew alipokabiliwa na kashfa ya ufisadi na kutakiwa kujiuzulu, Ford aliteuliwa, akapitishwa na Baraza la Wawakilishi kuwa Makamu wa Rais. Alitumikia nafasi hiyo miezi nane kabla ya kukalia kiti cha urais.

Kuelekea uchaguzi wa urais Marekani mwaka 1976, Republicans walimpa tiketi Ford kuwania muhula wa pili kwa mbinde dhidi ya Ronald Reagan, baada ya kusimangwa kwa maneno kuwa aliingia madarakani bila kupitishwa na chama, vilevile alikosea kutangaza msamaha kwa mtangulizi wake, Nixon, aliyekumbwa na kashfa ya Watergate.

Maneno hayo yalisababisha mgawanyiko mkubwa. Matokeo yake, mgombea wa Democratic, Jimmy Carter, alishinda kiti. Hasara ya juu kwa Republican ilichangiwa na maneno kuzunguka uteuzi wa Ford kuwa mgombea urais.

Rais Samia aliingia madarakani baada ya kifo cha Magufuli. Je, maneno ya “fomu moja” ni kijembe kwa wanaojaribu kusema Rais Samia hakupata uungwaji mkono kamili ndani ya CCM mwaka 2020 kwa kuwa alikuwa mgombea mwenza?

Kwa vyovyote vile, CCM watambue kuwa maneno mengi ya utetezi kwa Rais Samia au jaribio lolote la kumdhibiti asiwanie muhula wa pili, halitakiacha chama salama. Mifano nimeshatoa na mingine nitaongeza.

Rais wa 36 wa Marekani, Lyndon Johnson, aliponyimwa tiketi kuwania muhula wa pili, chama chake, Democratic, kilipoteza kiti dhidi ya Republican. Hata Rais wa 33, Harry Truman, aliponyimwa fursa ya kugombea muhula mwingine mwaka 1952, Democrats walipoteza kiti kwa Republicans.

Sababu ya chama cha UDF Malawi kudidimia jumla ni jaribio lake la kumdhibiti Rais aliyekuwa madarakani, Bingu wa Mutharika. Chama cha Labour, UK, kilipoteza uongozi mara kilipogawanyika na kumlazimisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Tony Blair aachie kiti kumpisha Gordon Brown.

Hoja ni hii

Kushindana na Rais madarakani kuwania tiketi ya chama ni kawaida. Inawezekana hata kumshinda. Jambo la kuzingatia ni kuwa Rais aliye ofisini, anapokuwa na fursa ya kuwania muhula mwingine, hiyo ni karata mali (trump card).

Kwa kuzingatia turufu hiyo, umekuwa utamaduni duniani kote, Rais aliye madarakani anapowania muhula wa pili, chama chake kinampa tiketi bila kupingwa.

 Hata inapotokea mwanachama mwingine kujaribu kusogelea tiketi, uongozi wa chama humalizana naye kidiplomasia ili kudhibiti mpasuko.

CCM walimudu kumtuliza Dk Mohammed Gharib Bilal, alipojaribu kumpa changamoto aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk Amani Abeid Karume kuelekea Uchaguzi Mkuu 2005.

Hata John Shibuda, alipotaka kumkabili Rais wa Nne, Jakaya Kikwete mwaka 2010, alijiondoa kwa amani. Bila shaka alitulizwa chini kwa chini.

Hakuna Rais madarakani mwenye kupenda kupingwa. Kila mmoja hutamani amalize vipindi vyake vya kikatiba. Inapotokea chama kinamnyima tiketi, mpasuko hufuata. Madhara nimeshatangulia kuyaeleza kwa mifano ya kutosha.

Kisichopaswa kusahaulika ni kuwa kumkabili Rais Samia ndani ya chama, maana yake unashindana na mtu mwenye madaraka ya aina nne ya kipekee; Mkuu wa Nchi, Amiri Jeshi Mkuu, Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa CCM (chama kinachoongoza dola).

Mtu wa aina hiyo, akikosa tiketi ya chama chake, ni rahisi kujenga nguvu pembeni na kuimarika haraka. Ndivyo iliwezekana kwa Bingu  wa Malawi, ambaye wala hakuwa na uongozi wa chama. Haitashindikana kwa Samia mwenye mamlaka yote. Hasara kubwa itakuwa kwa CCM.

Uchaguzi wa urais Marekani 2020, Republicans walijishauri sana kumnyima tiketi Rais wa 45 wa nchi hiyo, Donald Trump. Busara ya juu ikawa, kuliko kusababisha mgawanyiko, bora kumwacha aendelee muhula mwingine. Trump akashindwa  na Joe Biden wa Democratic.

Busara za aina hiyo zimekuwa zikitumika maeneo mengi. Kuliko kuua chama, bora kumwacha Rais amalize muhula wake mwingine wa miaka minne au mitano. Hii ni tahadhari ya juu. Lengo si kutisha au kutafsiri vinyongo na matamanio ya wengine, bali  ndiyo hali halisi.