UCHOKOZI WA EDO: Hotuba za Mwalimu Nyerere zimetuachia macho ya makengeza

Huwa nawasikiliza wakubwa mbele ya vipaza sauti. Nacheka kwelikweli. Iwe kwa wanaotutawala au wapinzani. Hucheka pale wanapochota maneno ya Mwalimu Julius Nyerere katika hotuba au vitabu alivyoandika.

Wanachota wanachokipenda kutoka katika hotuba hizo, halafu wanajifanya vipofu katika maneno mengine aliyowahi kuyasema. Nacheka kwelikweli. Inanikumbusha jinsi ambavyo kuna watu wanatumia vitabu vya dini kuanzisha madhehebu. Wanachota mistari fulani, wanaitafsiri wanavyotaka, wanaanzisha dhehebu.

Kwa hotuba za Mwalimu tunafanya hivyo hivyo. Utaona kiongozi anasimama anasema ‘Mwalimu Nyerere katika hotuba yake ya mwaka fulani alisisitiza amani’. Unatulia kidogo kudhani kwamba kiongozi huyo huyo atasisitiza suala la uhuru wa mawazo kama Mwalimu alivyowahi kusema huko nyuma. Hilo hautolisikia, hilo hawezi kumkariri Mwalimu.

Utasubiri kusikia labda atasema Mwalimu aliwahi kusema ‘Kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake, ana haki ya kusikilizwa, hapaswi kutiwa woga’. Hilo hauwezi kusikia. Amechota alichotaka kutoka kwa Mwalimu ili kuhalalisha anachokifanya.

Kuna nukuu za Mwalimu ambazo zimezagaa mitandaoni. Sisikii viongozi wetu wa wakiziingiza katika hotuba zao. Huwa nashangaa. Hawatafungua midomo kuzikariri nukuu za kinabii ambazo Mwalimu aliwahi kuzisema huko nyuma.

Inaonekana Mwalimu amebakia kuwa alama ya kuhalalisha unachotaka kufanya bila ya kujali kwamba pia aliacha wosia wa mambo ambayo kiongozi husika hakupaswa kuyafanya. Ndio maana leo kila mtu ananukuu maneno ya Mwalimu. Watawala wetu wanayafanya maneno yake kuwa ngao, wapinzani nao wanayatumia kuwa ngao.

Sisi Darasa la saba tuna mistari yetu katika hotuba za Mwalimu, mafisadi wana mistari yao, watawala wana mistari yao, wapinzani nao wana yao. Unachukua kipande kinachokufurahisha halafu unajifanya umekunja sura kama vile una uchungu sana na maneno husika yaliyosemwa na Mwalimu. Vile vifungu ambavyo haviendani na matendo yako unajifanya huvioni.

Mwalimu akipewa nafasi ya kurudi tena duniani japo kwa siku mbili tu, atashangaa sana. atajikuta akiuliza tu ‘Hata huyu na hizi tabia zake anatumia maneno yangu?’. Atashangaa sana. Atacheka sana. ‘Yaani hata huyu ananinukuu?’.