Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uchunguzi wabaini eneo la ardhi lililotitia Same, halifai kwa makazi ya watu

Muktasari:

  • Mpaka sasa, wananchi wa Kijiji cha Marieni, kara ya Chome wilayani Same mkoani Kilimanjaro wamehifadhiwa kwa ndugu, jamaa na marafiki wakisubiri tamko la Serikali kuhusu kuondoka katika eneo hilo.

Same. Siku chache baada ya wataalamu wa jiolojia kufika katika eneo ambalo ardhi yake ilikuwa ikititia na kusababisha mipasuko kwenye makazi ya wananchi katika Kijiji cha Marieni, Kata ya Chome, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa eneo hilo halifai kwa makazi ya binadamu kutokana na udongo wake kuwa laini jambo ambalo ni hatari.

Mpaka sasa, kaya 10 zimeyakimbia makazi yake katika kijiji hicho huku moja ya nyumba ya ibada ikishindwa kutumika, baada ya kutengeneza nyufa zilizosababishwa na hali hiyo.

Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Marieni, kata ya Chome, akionyesha moja ya eneo ambalo limeathiriwa na mpasuko wa ardhi ambao umepelekea baadhi ya maeneo kutitia.

Kufuatia hali hiyo, baadhi ya wananchi ambao maeneo yao yameathiriwa wamehamisha familia pamoja na mali zao na kwenda kuhifadhi kwenye maeneo ambayo wamepata hifadhi ya muda wakisubiri muafaka wa Serikali.

Hata hivyo, Mwananchi lilipotembelea eneo hilo, Aprili Mosi, 2026, lilishuhudia moja ya kanisa likiwa limeachwa wazi baada ya kuta zake kupasuka nyufa kubwa, huku sakafu yake ikionyesha dalili za kutitia.

Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Marieni, kata ya Chome, akionyesha moja ya eneo ambalo limeathiriwa na mpasuko wa ardhi ambao umepelekea baadhi ya maeneo kutitia.

Akizungumza na Mwananchi leo Mei 14, 2026, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Ally Samaje amesema baada ya kufanya utafiti katika eneo hilo wamebaini kuwa hali ya udongo wa eneo hilo kutoka juu ya ardhi mpaka kwenye safu ngumu chini ni laini na hivyo kuhatarisha maisha ya watu.

Aidha, amesema kutokana na hali hiyo eneo hilo halifai kwa makazi ya watu na badala yake linaweza kutumika kwenye shughuli za kilimo kwa sababu hakuna mgandamizo mzito chini ya ardhi.

Baadhi ya wananchi wakionyesha eneo karibu na kanisa la Wasabato Kungwini ambalo limepata mpasuko mkubwa kutokana na baadhi ya vipande vya aradhi kupishana.

"Katika uchunguzi ambao tumefanya, matokeo ya awali yanaonyesha kuwa udongo wa eneo lile una tabaka kubwa la udongo laini na miamba migumu ikiwa chini zaidi. Hivyo, nyumba zinazojengwa katika eneo hilo hujengwa juu ya udongo laini. Udongo huo unapolowana kwa maji huwa rahisi kusogea au kucheza, hali inayoweza kusababisha ardhi au nyumba kutitia.

Amesema, "ukumbuke pia maeneo hayo pia yana milima mingi, inayoongeza hatari ya kutokea kwa mmomonyoko au kusogea kwa ardhi. Eneo hilo linafaa zaidi kwa shughuli za kilimo, kwani kwa upande huo hakuna uhatarishi mkubwa. Hata hivyo, kwa wananchi kuishi na kujenga nyumba katika eneo hilo si salama na haishauriwi, kutokana na hali ya udongo kutokuwa imara."

Moja ya eneo la kanisa la Wasabato, ambalo lipo katika Kitongoji cha Makandeni, Kijiji cha Marieni, ambalo limeachana   kutokana na ufa mkubwa ambao umepita katika eneo hilo la kanisa.

Aidha, amesema tayari walishatoa taarifa ya mrejesho wa ripoti hiyo kwa uongozi wa wilaya ili wawasiliane na wananchi wa kijiji hicho kwa ajili ya kuchukua tahadhari kusitokee madhara.

"Wakati tukiendelea kuchakata ripoti zetu, lazima tahadhari zichukuliwe na tayari tushafahamisha uongozi wa wilaya ili waweze kuchukua tahadhari kwa wale wananchi ili kusitokee madhara na maafa,"amesema Samaje

Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Marieni, kata ya Chome, akionyesha moja ya eneo ambalo limeathiriwa na mpasuko wa ardhi ambao umepelekea baadhi ya maeneo kutitia.

Akizungumza mmoja wa wananchi wa eneo hilo, Marry Godfrey amesema mpaka sasa hawajui kinachoendelea na kama watatakiwa kuondoka katika eneo hilo wanaiomba Serikali kuwatafutia maeneo mengine mbadala ya kwenda kuishi.

"Hapa tulipo hatujui kinachoendelea kwenye hili eneo, tumepata tu hifadhi kwa ndugu zetu, tunachosubiri ni tamko la Serikali kama tutarudi kwenye maeneo yetu au la,"amesema mwananchi huyo

Cathbert Wilfred, ambaye pia ni mkazi wa kijiji hicho amesema wanasubiri majibu ya Serikali kama watatakiwa kuendelea kuishi katika eneo hilo au kuondoka.