UCSAF kuboresha mawasiliano Kagera

New Content Item (1)
UCSAF kuboresha mawasiliano Kagera

Muktasari:

  • Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (Ucsaf), umejipanga kuboresha huduma za mawasiliano ya simu na usikivu wa redio na runinga katika maeneo ya mipakani ili kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo wapate huduma hiyo muhimu.

Kagera. Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (Ucsaf), umejipanga kuboresha huduma za mawasiliano ya simu na usikivu wa redio na runinga katika maeneo ya mipakani ili kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo wapate huduma hiyo muhimu.

Hili litasaidia kuhakikisha usalama wa nchi kwa kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyoweza kufanywa kwa kutumia mawasiliano na taarifa za nchi nyingine kama uvamizi, uporaji na uhamiaji haramu.

Hayo yamebainishwa na ofisa Mtendaji Mkuu wa Ucsaf, Justina Mashiba mkoani humo katika ziara iliyowajumuisha wajumbe wa bodi ya mfuko huo kwa lengo la kukagua huduma za mawasiliano katika wilaya zinazopakana na nchi jirani ndani ya mkoa huo. Wilaya hizo ni Misenyi, Karagwe, Kyerwa na Ngara.

Akiwa katika Kata ya Kakunyu, Kijiji cha Bungango mpakani mwa Tanzania na Uganda, Mashiba alisema Wananchi wengi katika eneo hilo hawapati huduma za mawasiliano ya mitandao ya simu kutoka Tanzania bali hupata kutoka nchi za jirani.

“Kwa namna moja ama nyingine inaweza kuhatarisha usalama wa wananchi hao na nchi kwa ujumla,” alisema

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti aliipongeza Ucsaf kwa hatua hiyo huku akiongeza kuwa ni muhimu mkoa ukapewa kipaumbele.

Mkoa wa Kagera unapakana na nchi nne kati ya nane ambazo Tanzania tunapakana nazo, ambazo ni Rwanda, Burundi na Uganda na kupitia ziwa Victoria inapakana na Kenya.

Gaguti alisema mbali na usalama lakini mawasiliano hayo yanaweza pia kuboresha hali ya uchumi wa mkoa huo mkoa na wananchi wa maeneo hayo kwa ujumla.

“Asilimia 50 ya kahawa ya Tanzania inatoka Kagera na asilimia 80 ya kahawa katika Mkoa huu inatoka katika Wilaya za mipakani, tumekuwa na changamoto kubwa ya kufikia huduma za kifedha kwa sababu huduma hii inahitaji mitandao ya simu,” alisema

Ameongeza kuwa kutokana na changamoto hiyo wakulima wengi Mkoani humo wamekuwa wakiuza kahawa nchi jirani na imekuwa ngumu kuwabana kutokana na kuwepo kwa changamoto ya mawasiliano ya simu na huduma za kifedha.