Udart yataja sababu mabasi yake kuonekana Barabara ya Pugu
Kituo cha Mwendokasi katika Barabara ya Nyerere kuelekea Gongo la Mboto kilichopo eneo la Tazara jijini Dar es Salaam. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Mabasi mapya 99 ya Udart yaliingizwa nchini Januari mwaka huu yakitanguliwa na moja lililoletwa mwaka jana(2025) kwa ajili ya majaribio.
Dar es Salaam. Kampuni ya mabasi Yaendayo Haraka (Udart), imetoa ufafanuzi kuhusu mabasi yake kuonekana katika barabara ya Pugu.
Wiki iliyopita video za magari hayo zilisambaa katika mitandao ya kijamii na kukawa na madai kuwa, pengine yanafanyika majaribio.
Akizungumza na Mwananchi leo, Jumatatu Juni 15, 2026 kuhusiana na suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Udart, Pius Ng'ingo amesema hawajaanza kutoa huduma wala hawakuwa wakifanya majaribio kama inavyoelezwa na baadhi ya watu.
“Yale mabasi yalikuwa yanapelekwa kuegeshwa katika eneo maalumu Gongo la Mboto Mwisho baada ya kumaliza mchakato wa kuyalipia usajili wake kwa Mamlaka ya Mapato (TRA).”
"Awali magari haya yalikuwa chini ya TRA kwa kuwa yalikuwa hayajalipiwa kodi na kuegeshwa karakana ya Mbagala.
"Lakini hivi karibuni tushamaliza taratibu za kuyalipia na ukishafikia hapo unapaswa kuyaondoa mikononi mwao na kwa kuwa eneo tulilopata la kuegesha ni Gongo la Mboto tumeyapeleka huko baadhi," amesema.
Ameeleza mabasi yaliyopelekwa Gongo la Mboto ni 40 huku mengine 60 yakiegeshwa katika karakana ya Ubungo.
Mabasi mapya 99 ya Udart yaliingizwa nchini Januari mwaka huu yakitanguliwa na moja lililoletwa mwaka jana(2025) kwa ajili ya majaribio na hivyo kufanya magari mapya ya kampuni hiyo yanayotumia gesi kuwa 100.
Kuhusu kuanza kufanya kazi katika barabara hiyo ya Pugu, Ng'ingo amesema bado kwa kuwa baadhi ya miundombinu haijakamilika, lakini Udart ipo tayari.
Wakati Mkurugenzi huyu akisema hayo, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ambao ndio wanajenga barabara hiyo kupitia kwa Meneja ujenzi wa mradi wa Mabasi ya Yaendayo Haraka (BRT) kutoka Tanroads, Frank Mbilinyi alisema ujenzi wake umefikia asilimia 99 huku asilimia moja iliyobaki inahusisha taa za kuongozea magari na ufungwaji mifumo ya umeme ndani ya vituo na waliahidi wangekamilisha Aprili 2026.
Barabara ya Pugu (barabara ya Gongo la Mboto) ambayo ni mradi wa awamu ya tatu kutekelezwa una urefu wa kilomita 23.3 ukiwa na jumla ya vituo 32 vya kuchukua na kushushia abiria.
Aidha barabara hiyo unahusisha kutoka Posta hadi Gongo la Mboto na barabara inayopita Buguruni (kipande cha barabara ya Mandela na Uhuru) hadi makutano ya taa za Boma Karume.