Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Udhibiti dawa za kulevya Tanga wapunguza waraibu

Mraibu wa dawa za kulevya akiwa ameshikilia kibiriti cha gesi wakati akijiandaa kuwasha msokoto wa bangi.

Muktasari:

  • Udhibiti wa dawa ya kulevya aina ya heroini jijini Tanga umechangia kupungua kwa watumiaji, huku baadhi ya waraibu wakitumia dawa feki au kukimbilia bangi na pombe.

Tanga. Upatikanaji wa dawa ya kulevya aina ya heroini umeelezwa kuwa mgumu katika Jiji la Tanga, hali inayotajwa kuwa matokeo ya kuimarika kwa udhibiti dhidi ya uingizwaji na usambazaji wa dawa hizo.

Daktari wa afya ya akili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo, Wallace Karata, amesema kupungua kwa upatikanaji wa heroini ni ishara ya mafanikio ya juhudi za mamlaka. Hata hivyo, ameonya kuwa uhaba huo umeibua changamoto mpya, ikiwamo matumizi ya dawa bandia zinazochanganywa na valium na kuuzwa kama heroini.

“Matumizi ya heroini yamepungua. Wapo wanaodhani wametumia heroini, lakini vipimo vinaonyesha sivyo. Hii inaonyesha udhibiti umezaa matunda, ingawa kuna hatari ya dawa feki,” amesema Karata.

Mkuu wa kitengo cha huduma za waraibu katika Mkoa wa Tanga, Dk Wallace Karata akizungumza na Mwananchi hali halisi ya waraibu wa dawa za kulevya Tanga. Picha na Mbonea Herman

Kwa mujibu wake, zaidi ya waraibu 1,300 wamesajiliwa tangu kuanzishwa kwa huduma ya methadone mwaka 2020, huku zaidi ya 600 wakipata huduma hiyo kila siku. Amesema huduma hiyo imekuwa nyenzo muhimu katika kupunguza utegemezi wa heroini na kusaidia waraibu kurejea katika maisha ya kawaida.

Ofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Shaban Miraji, amesema katika Kanda ya Kaskazini kuna vituo vitatu vya tiba saidizi (MAT) katika mikoa ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro, huku Manyara ukitarajiwa kupata kituo hicho hivi karibuni. Ameongeza kuwa kituo kingine kinajengwa Muheza kupunguza adha ya waraibu kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.

Wadau wanasema pamoja na mafanikio ya kudhibiti uingizwaji wa heroini, mapambano yanapaswa kuendelea ili kukabili dawa bandia na mbinu mpya za usambazaji. Wanasisitiza ushirikiano wa karibu kati ya mamlaka, wataalamu wa afya na jamii ili kuimarisha udhibiti na kulinda vijana dhidi ya athari za dawa za kulevya.