Udumavu unavyoitesa Nyanda za Juu Kusini

Iringa. Karibu kila kiongozi mgeni au mwenyeji wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini akisimama kutoa hotuba lazima agusie suala la udumavu.

Udumavu ni hali inayotokea wakati uwiano kati ya urefu na umri wa mtoto vinakuwa chini kwa vigezo vya ukuaji vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani.

Hii ni changamoto ya kiafya inayotokana na ukosefu au upungufu wa lishe sahihi, inayosababisha viongozi kukuna vichwa juu ya namna ya kupambana nayo.

Licha ya kuwepo juhudi kubwa za kumaliza tatizo hilo, takwimu zinaonyesha mikoa ya Rukwa, Njombe, Iringa na Mbeya bado ni vinara wa udumavu nchini.

Utafiti wa idadi ya watu na afya na utafiti wa viashiria vya malaria (TDHS) wa mwaka 2022, Tanzania ina asilimia 30 ya watoto waliodumaa.

Februari 7, mwaka huu, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akizindua ripoti ya awali ya viashiria vya afya ya uzazi na mtoto na malaria ya mwaka 2022, alisema Mkoa wa Iringa unaongoza kwa udumavu kwa asilimia 59.9, Njombe ikifuatia kwa asilimia 50.4 ukifuatiwa na Rukwa asilimia 49.8.

Mikoa hii inatajwa vinara wakati ikifahamika kuwa ndiyo inayolisha chakula (nafaka) kwa wingi, hivyo kuibua tatizo la msingi linalohitaji kutupiwa jicho la mpangilio wa mlo kamili.

Hali ya lishe

“Nikiwaacha watoto asubuhi nawaandalia ugali na mboga, watakula asubuhi ninapoondoka kisha mchana. Jioni nikirudi napika chakula kingine. Siyo kwamba hawali, wanakula sana,” anasema mmoja mama wa watoto wawili, katika Kijiji cha Ilambilole, wilayani Iringa.

Kwa sababu ilikuwa asubuhi, Mwananchi ilishuhudia mboga za majani zilizokuwa zimepikwa na kuiva sawasawa.

Afya za watoto wa mama huyo hazikuakisi uwepo wa lishe bora, licha ya kuwa, nje kulikuwa na lundo la mahindi yaliyokuwa yametoka kuvunwa.

Ni ukweli usiopingika kuwa baadhi ya wazazi na walezi wamebanwa na kazi kiasi cha kushindwa kuandaa mlo mzuri kwa watoto wao.

“Haya mahindi ni yangu, natarajia kupata magunia hadi 30. Sioni kama kuna tatizo kubwa hapa na sio kwamba siachi chakula, naacha cha kutosha,” alisema mama huyo.

Wakati mama huyo anasema hayo, Ofisa Lishe wa Kijiji cha Mabaoni, Kata ya Magungu, Bonde la Mgololo, Janeth Kayage alisema baadhi ya wazazi na walezi hawapo makini katika kuzingatia lishe bora kwa watoto wao.

Alisema wengi wao wakiamka asubuhi wanawaza kufanya kazi za kilimo huko watoto wakiachiwa lishe duni, jambo linaloongeza kasi ya udumavu.

"Yaani mama akimpikia wali au ugali na kuondoka na mtoto wake kwenda shamba au kazini anahisi amemaliza. Kunahitajika kuwepo na vikao vya mara kwa mara kuwaelimisha akina mama hao,” alisema Kayage.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk David Ntahindwa alisema sababu ya mkoa huo kuwa kinara na kutajwa kwenye udumavu ni kutokana lisha bora kutopewa kipaumbele na wananchi.

Alisema wananchi wanapaswa kuendelea kukumbushwa namna bora ya kutunza afya kwa kuzingatia lishe bora kama ambavyo wataalamu wa afya wanashauri.

Alisema mkoa huo una vyakula lakini tatizo kubwa ni kwa wananchi wenyewe kuweka vipaumbele kwenye kazi za uchumi bila kukumbuka kuhudumia familia zao.

"Maana mkiona asilimia kubwa hapa sura zenu zimetakata si kwamba uchumi ni mbaya bali suala kubwa ni vipaumbele," alisema Dk Ntahindwa.

Alisema ni muhimu kula vyakula vyenye protini kama nyama hususani nyama nyeupe kama kuku, samaki na simbili ambayo wengi wanaidharau lakini ubora wake unaizidi hata nyama ya ng'ombe.

Kwa upande wake, Vaileth Sumbi, mkazi wa Mtaa wa Ichenjezya alisema tatizo ni watu kuwa ‘bize’ na mambo yao na kusahau jukumu la malezi ikiwemo kuandaa chakula chenye mchanganyiko unaohitajika kwa watoto.

“Nashauri wazazi kubeba jukumu linalowahusu ili kuhakikisha watoto wanapata lishe bora kwa ajili ya afya zao,” alisema.

Baadhi ya wananchi mkoani Njombe akiwemo Recho Msigwa na Castory Ndendiya aliyezungumza na Mwananchi, walikiri baadhi yao kuwa shughuli nyingi na kutojali ulaji hasa wa watoto.

“Sasa nimejua hata kuandaa uji wa lishe, kwa hiyo hata nikirudi nyumbani itakuwa somo la kulea familia yangu kwa kupitia somo la lishe tulilojifunza leo,” alisema.

Pamoja na lishe, pia linatajwa suala la unyonyeshaji watoto kwa usahihi kama njia ya kuepuka udumavu.

Ofisa Lishe Mkoa wa Njombe, Berha Nyigu alisema hata maandiko matakatifu yameeleza ni moja ya majukumu ya mama kunyonyesha mtoto mpaka miaka miwili au zaidi ikiwezekana.

Alisema mama anayenyonyesha amefananishwa kwenye vitabu hivyo na mtu ambaye anapigana katika njia, hivyo atakapokufa ana haki zake mbele ya Mungu.

"Kwahiyo wewe mama ambaye unanyonyesha na ukamwachisha mtoto wako kunyonya kabla muda wake, tambua kabisa unamkosea Mwenyezi Mungu," alisema Nyigu.

Sababu nyingine ya kukithiri kwa udumavu inatajwa ni ulaji wa vyakula kwa mazoea.

Hii inathibitishwa na Jonathan Hankungwe, mkazi wa Ihanda mkoani Songwe, aliyesema katika mazingira yao wamekuwa wanakula ugali wa sembe na mara nyingi mboga ni maharage, isipokuwa mara chache wanapotumia mbogamboga, samaki au nyama.

“Sisi usipokula ugali basi siku hiyo unajihesabu umelala njaa tofauti na maeneo mengine ambayo wamekuwa wanakula vyakula kwa kubadilisha mara kwa mara,” alisema Hankungwe.

Elimu muhimu

Kutokana na ukubwa wa tatizi hilo, viongozi wametakiwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya kuandaa lishe bora kwa watoto kupitia mikutano ya vijiji, vitongoji.

Wazazi nao kwa upande wao wanashauriwa watoe kipaumbele kwa watoto wao na kuacha kutoa kipaumbele kwa shughuli za uchumi za kujiongezea kipato pekee.

Wadumavu kutambuliwa

Kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya Mji wa Njombe, Dk Kisulila Matanga alisema kwa sasa wanaendelea na jitihada za kusajili watoto, kujua afya zao na kuendelea kutoa elimu ya afya.

Alisema kwa wale watakaobainika kuwa na changamoto ya udumavu, wanawapa huduma bora na kuhakikisha wanahudhuria kliniki.

Alisema jitihada pia zimewekwa katika utunzaji wa kumbukumbu za kupima hali ya lishe kwa watoto kwani wengi wao hupoteza mawasiliano wakiwa nyumbani hivyo kusababisha kushindwa kumfuatilia mtoto hali yake ya kiafya.

"Kutoa matone ya Vitamini A kwa watoto na kuonyesha kwa vitendo makundi ya vyakula na mapishi yanavyopikwa nui moja ya mbinu za kukabiliana na tatizo hilo," alisema Matanga.

Katika hatua nyingine, ili kupambana na udumavu, Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) kimeanza kuzalisha mbegu bora za ulezi aina tisa ambazo zinahili mabadiliko ya tabia nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tari-Uyole, Dk Denis Tipe ameliambia Mwananchi kuwa kati ya tafiti zikizofwa kwenye aina hizo, tayari tatu zimesajiliwa na kusambazwa kwa wakulima.

Alisema kuwa lengo la kuboresha tafiti za mazao yenye virutubisho ni kuhakikisha udumavu una kuona Mkoa unaondokana na tatizo la udumavu kwa watoto.