Udumavu wakithiri Rukwa, Njombe, Iringa

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza wakati akizindua Ripoti ya awali ya viashiria vya afya ya uzazi na mtoto na malaria ya mwaka 2022 Jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Mikoa ya Rukwa, Njombe na Iringa yatajwa tena kuongoza kuwa na watoto wenye udumavu nchini.

Dodoma. Licha ya Serikali kufanya jitihada kumaliza tatizo la udumavu nchini, Mikoa ya Rukwa, Njombe na Iringa imebaki kuwa mikoa inayoongoza kwa tatizo la udumavu nchini.

Hata hivyo, ripoti ya utafiti wa Hali ya Uzazi ya Afya ya Mama na Mtoto na Malaria inaonesha kuwa hali ya udumavu imepungua nchini hadi asilimia 30 mwaka 2022.

Kwa mujibu wa utafiti wa Tanzania Demographic Health Survay (TDHS) wa mwaka 2018 umeonesha kuwa asilimia 31.8 ya watoto walidumaa.

Taarifa ya mikoa hiyo imetajwa leo Februari 7, 2023 na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akizindua ripoti ya awali ya viashiria vya afya ya uzazi na mtoto na malaria ya mwaka 2022 Jijini Dodoma.

Waziri Ummy amesema mkoa wa Iringa unaongoza kuwa na tatizo la udumavu kwa asilimia 59.9, Njombe asilimia 50.4 ukifuatiwa na Rukwa asilimia 49.8.

Kufuatia hali hiyo Waziri Ummy amehoji kuhusu bajeti ya kupambana na udumavu iliyotengwa na Serikali mkoani Iringa kwa ajili ya lishe kuwa imefanya kazi gani.

“Lazima tukachakate hizo takwimu kwa sababu inaonekana kuwa Iringa katika kila watoto 100 walio chini ya miaka mitano watoto 56 wamedumaa, watafiti twende mbali zaidi tukaangalie tatizo ni nini,” amesema.

Mikoa hiyo imetajwa kuongoza kuwa na hali ya udumavu mwaka 2020/2021, ambapo Mkoa wa Njombe ulikuwa na udumavu kwa asilimia 53.6, Rukwa asilimia 47.9 na Iringa asilimia 47.1.

Aidha Waziri Ummy amewataka wakuu wa mikoa na halmashauri kubadilishana uzoefu katika sekta hiyo ambayo mikoa mingine inafanya vizuri.