Uhaba wa mafuta waanza kuitesa dunia

Madereva bajaji wakiwa kwenye foleni kuelekea kituo cha mafuta nchini Sri Lanka ambako uhaba w anishati hiyo ni mkubwa kiasi cha kusababisha watu kukaa kwenye foleni yenye urefu mpaka kilomita tatu. Picha ya Mtandaoni

Muktasari:

Wakati Serikali ikichukua hatua kadhaa kukabiliana na kupanda kwa bei ya mafuta nchini, mataifa kadhaa barani Asia yanapitia kipindi kigumu kiasi cha kusababisha vifo kwenye foleni ya kupata nishati hiyo na viongozi wa Serikali kujiuzulu.

Wakati Serikali ikichukua hatua kadhaa kukabiliana na kupanda kwa bei ya mafuta nchini, mataifa kadhaa barani Asia yanapitia kipindi kigumu kiasi cha kusababisha vifo kwenye foleni ya kupata nishati hiyo na viongozi wa Serikali kujiuzulu.

Achana na kupanda kwa bei ambako hatua zinazochukuliwa na Serikali katika mataifa tofauti duniani kunaweza kudhibitiwa, hali imeanza kung’ata zaidi baada ya mambo kwenda harijojo.

Nchini Sri Lanka kwa mfano, wananchi wanapanga foleni inayofika urefu wa kilomita tatu kusotea nishati hiyo huku maduka yakilazimika kufungwa mchana wa saa nane ili kupunguza matumizi ya umeme unaozalishwa zaidi kwa mafuta.

Huko India na Pakistan, kukatika kwa umeme kumeilazimu Serikali kufunga shule, huku wajasiriamali wakifunga biashara zao. Wananchi hawawashi tena viyoyozi licha ya joto kupanda na kufika sentigredi 37 mchana.

Hata mataifa yenye uchumi mkubwa kidogo mfano Australia nayo yanahangaishwa na suala la mafuta, kwani bei ya umeme nchini humo ilipanda kwa asilimia 141 katika robo ya kwanza mwaka huu na Serikali ikawaomba wananchi kupunguza matumizi majumbani mwao.

Juni 15, Serikali ya Australia ilitangaza hatua kadhaa za kupunguza bei ya umeme na kuzuia mgawo wa kitaifa wa nishati hiyo muhimu. Hali kama hiyo pia inashuhudiwa nchini India ambako Mei 28 Serikali ililiruhusu shirika lake, Coal India, kuagiza makaa ya mawe kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2015 ilipozima mitambo yake katika juhudi za kupunguza uchafuzi wa mazingira. India ni mchafuzi mkubwa wa tatu duniani wa mazingira kutokana na wingi wa viwanda ilivyonavyo.


Viongozi wajiuzulu

Mapema Aprili, mawaziri wote 26 wa Serikali ya Sri Lanka waliwasilisha barua ya kujiuzulu kwa Rais Gotabaya Rajapaksa. Viongozi hao walimjumuisha Waziri wa Fedha, Basil Rajapaksa, Waziri wa Kilimo, Chamal Rajapaksa na Waziri wa Michezo, Namal Rajapaksa.

Wakati mawaziri hao wanajiuzulu kutokana na maandamano yasiyokoma ya wananchi, Rais Gotabaya Rajapaksa na Waziri Mkuu Mahina Rajapaksa ambaye ni kaka yake waliendelea kubaki madaraka ila mwezi mmoja baadaye, Mei 9, waziri mkuu naye alilazimika kujiuzulu.

Kujiuzulu kwa Mahina Rajapaksa kulimpa nafasi Waziri wa Fedha, Ranil Wickremesinghe kuchukua nafasi hiyo. Akiwa na kofia hizo mbili, Jumatano ya wiki iliyopita alitangaza kwamba “uchumi wa Sri Lanka umeanguka kabisa.”

Kutoka Islamabad yalipo makao makuu ya Serikali, Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan alijiuzulu Aprili 9 baada ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye. Kati ya sababu zilizochangia Khan kuchukua uamuzi huo ni ongezeko la gharama za maisha kulikotokana na kupanda kwa mfumuko wa bei kwa tarakimu mbili.

Hali hiyo ilimlazimu Khan kuchukua hatua kadhaa ambazo hazikumsaidia. Mapema Februari, waziri mkuu huyo alitangaza kupunguza bei ya mafuta na umeme akitangaza nafuu hiyo ingedumu mpaka Juni, lakini hakufika akiwa madarakani. Aliondoka kupisha fikra mpya.


Uviko-19, vita Ukraine

Ingawa kila Taifa lina changamoto yake, chanzo ni athari za janga la Uviko-19 pamoja na vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine. Kinachosumbua zaidi ni mahitaji kutolingana na uzalishaji baada ya Russia kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani.

Ingawa janga la Uviko-19 lilishusha bei ya mafuta katika soko la dunia kutokana na watu kuzuiwa kutembea hivyo magari mengi kubaki yameegeshwa huku wafanyakazi wakilazimika kufanya kazi kutoka nyumbani, uchumi sasa umeanza kurudia kawaida baada ya viwanda vingi kurejesha uzalishaji, hivyo nishati nyingi zaidi kuhitajika.

Kurudi kwa viwanda vingi kumeongeza mahitaji ya makaa ya mawe, mafuta hata gesi asilia kwa ajili ya nishati ya uzalishaji. Bidhaa hizi zote, zinapatikana kwa wingi nchini Russia, mzalishaji mkubwa wa tatu wa mafuta duniani na msambazaji wa tatu.

Vikwazo vilivyowekwa na Marekani pamoja na Jumuiya ya Ulaya kwa Russia vimesababisha uhaba wa mafuta, kwani mataifa mengi yanashindwa kupata mbadala hivyo kuongeza ushindani kwa nchi chache zinazozalisha mafuta.

Ongezeko la mahitaji limepandisha bei ya malighafi zote zinazotumika kuzalisha nishati. Bei ya makaa ya mawe imepanda mara tano zaidi ya ilivyokuwa mwaka jana huku ile ya gesi asilia ikipanda mara 10 kipindi hicho. Mataifa yasiyo na chanzo cha nishati hizo ndiyo waathirika wakubwa.

“Kwa nchi zenye uchumi unaoinukia kama Sri Lanka ambazo zinatakiwa kununua mafuta na gesi asilia kutoka nje ya nchi, zinaumia zaidi kwa sababu zinalazimika kutumia fedha nyingi kununua bidhaa hizo huku zenyewe zikiuza kidogo. Zinauza bidhaa nyingi ili kuagiza kiasi kidogo cha mafuta au gesi asilia,” alisema Mark Zandi, mchumi mwandamizi wa Moody’s Analytics alipohojiwa na CNN.

Wachambuzi wanasema nchi nyingi zenye uchumi mdogo ambazo zina viwanda vichache vinavyozalisha bidhaa muhimu zitaathirika zaidi, kwani zinalazimika kushindana na mataifa makubwa kiuchumi kupata mafuta kwa ajili kuendesha mitambo na kuzalisha umeme.


Wadau watahadharisha

Mataifa hayo ya Asia yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa inasemwa kuwa huenda ukawa ni mwanzo tu lakini hali kama hiyo inaweza kushuhudiwa hata nchini.

Mhadhiri wa Chuo cha Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory anasema ingawa Serikali imechukua hatua muhimu kupunguza kupanda kwa bei ya mafuta nchini, lakini hazitoshi kwani nishati ni muhimu kwa uchumi na kosa lolote likifanyika unaweza kuanguka kama ilivyotokea Sri Lanka.

“Serikali iangalie namna ya kupunguza matumizi kwenye maeneo yasiyo na athari mfano sherehe za uhuru, zinaweza kusitishwa hata mbio za mwenge, zinaweza kupunguzwa ukakimbizwa maeneo muhimu tu na hela zilizotengwa zikaelekezwa kupunguza bei ya mafuta,” anashauri Dk Pastory.

Ongezeko dogo la bei ya mafuta yanayotumika viwandani na kwenye magari yanayosafirisha bidhaa zilizotengenezwa hata mazao ya shambani anasema humwangukia mteja wa mwisho ambaye uwezo wake wa kununua ukipungua utakuwa mwanzo wa kudorora kwa uchumi.

Rais wa Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA), Godvictor Lyimo anasema uchumi wa Tanzania bado uko vizuri, kwani akiba ya fedha za kigeni na wawekezaji kutoka nje wanazidi kuongezeka hivyo kulihakikishia Taifa fedha za kigeni kuagiza bidhaa, yakiwamo mafuta kutoka nje.

“Utalii nao unafufuka, wageni wengi wanaingia nchini. Deni la Serikali ni himilivu. Tofauti na mataifa mengine, sisi tunazo rasilimali zote muhimu, mfano gesi asilia na makaa ya mawe, huu ni wakati wa Serikali kuwekeza huko ili kupunguza utegemezi kwenye mafuta,” ameshauri Lyimo siku chache baada ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania kusema imetoa leseni 14 kwa wafanyabiashara kujenga vituo vya kujaza gesi kwenye magari.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Usimamizi wa Rasilimali za Asili (NRGI) kanda ya Afrika, Silas Olang anasema “Serikali iendelee kutoa ruzuku zaidi kuulinda uchumi. Hatua za ndani ni muhimu kwa sababu hatuwezi kubadili chochote kama vite vitaendelea kati ya Russia na Ukraine.”