Uhamiaji watakiwa kuboresha huduma kwa wageni

Katibu Mkuu Wizara ya  Mambo ya ndani ya nchi  Kaspar Mmuya, akizungumza makamanda wa jeshi la uhamiaji Tanzania bara na Visiwani. Picha na Fina Lyimo

Muktasari:

  • Makamanda wa Jeshi la Uhamiaji Tanzania wametakiwa kuboresha huduma za wageni wanaoingia na kutoka nchini katika viwanja vya ndege na mipakani ili kuepuka malalamiko yasiyo ya lazima.

Moshi. Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Kaspar Mmuya amewataka makamanda wa Jeshi la Uhamiaji Tanzania Bara na Visiwani kuboresha huduma kwa wageni wanaoingia na kutoka nchini katika viwanja vya ndege na mipakani.

Ameyasema leo Jumatano julai 12, 2023 wakati akifungua kikao kazi cha maofisa wa uhamiaji kutoka Tanzania Bara na Visiwani kilichofanyika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amesema kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wageni wakilalamikia huduma isiyorizisha kutoka kwa maafisa uhamiaji wa viwanja vya ndege na mipakani jambo ambalo halileti picha nzuri kwa taifa.

Mmuya amesema makamanda hao wana wajibu wakuhakikisha wanatoa huduma nzuri kwa wageni wanaoingia hapa nchini ili kuweza kuongeza mapato ya serikali.

Amesema kwa sasa Tanzania imekuwa ikipokea watalii wengi kutoka mataifa ya nje baada ya Serikali kufungua milango kupitia filamu ya Royal Tour iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema lazima maofisa wanaopangwa kufanya kazi maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege kuwa na lugha nzuri kwa wageni wanaoingia na kutoka hapa nchini.

“Lugha nzuri zikitumika kwa wageni wanoingia na kutoka hapa nchini wageni, wataongezeka  kutoka kwenye  mataifa yao kwa kuwa watapeleka sifa nzuri za hapa nchini ambazo zitakuwa zimetengenezwa kwa kauli zenu,” amesema.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji, Dk Anna Makakala amesema lengo la kukutanisha makamanda hao ni kujadili upungufu uliopo kuufanyia kazi.

Dk Makakala amesema kikao kazi hicho kimejumuisha makamishna wa uhamiaji, makamanda wa mikoa na wakuu wa divisheni ambapo watajadili changamoto kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.