Uhamiaji yafafanua zuio bosi Coca cola

Wednesday November 25 2020
uhamiaji pic
By Kelvin Matandiko

Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji nchini imesema imemzuia bosi mpya wa kampuni ya Coca-Cola Kwanza, Andrew Musingo kwa sababu ya kutokuwa na kibali cha kazi na cha kuishi nchini.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano katika idara hiyo, Paul Mselle jana aliliambia gazeti hili kuwa Musingo anayetakiwa kuanza majukumu yake kama Mkurugenzi mtendaji mpya wa kampuni hiyo alitakiwa kukata kibali cha kazi kinachotolewa na Wizara ya Kazi kabla ya kushughulikia kuomba kibali cha kuishi.

Hata hivyo, juhudi za kuupata uongozi wa kampuni hiyo yenye ofisi zake Jijini Dar es Salaam hazikufanikiwa baada ya kuwatafuta kwa njia ya simu ya mkononi bila mafanikio ya kupokelewa.

Kabla ya ufafanuzi huo, taarifa za kuzuiliwa kuingia nchini kwa bosi huyo zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii kuanzia Jumatatu.

“Kwa mwaka huu, alikuwa akitumia business pass inayotolewa mara moja kwa mwaka mmoja, ina uhai wa miezi mitatu na kwamba kwa mwaka huu aliomba na akapewa mara mbili. Sasa wanaotoa hiyo business pass wakasema haiwezekani aendelee kutumia mwanya huo,” alisema Mselle.

“Ndio maana wakati anakuja wakamwambia hapana, inabidi apate kabisa kibali cha kazi na kibali cha kuishi. Kisheria hairuhusiwi pia kufanya utaratibu wa kupata kibali cha kazi ukiwa hapa nchini.”

Advertisement

Mselle alisema haijafahamika kama bosi huyo alishaanza kushughulikia upatikanaji wa vibali hivyo.

Advertisement