Ujasusi wa Putin na mgogoro wake na Magharibi

Rais Vladimir Putin wa Russia akiwa na baadhi ya makamanda wa Jeshi la nchi hiyo.

Muktasari:

Baada ya kuingiwa sana na hamu ya kuwa jasusi, akiwa na umri wa miaka 18, Vladimir Putin alijiandikisha katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Leningrad mwaka 1970 na kujiwekea nafasi nzuri ya kujiunga na Idara ya Usalama na Shirika la Ujasusi la Urusi (KGB).

Baada ya kuingiwa sana na hamu ya kuwa jasusi, akiwa na umri wa miaka 18, Vladimir Putin alijiandikisha katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Leningrad mwaka 1970 na kujiwekea nafasi nzuri ya kujiunga na Idara ya Usalama na Shirika la Ujasusi la Urusi (KGB).

Ingawa katika chuo hicho kulikuwa na michezo mingi, mchezo wa tenisi ukiwa ndio ulipendwa zaidi kuliko mingine yote, Putin hakuwa mchezaji wa tenisi, lakini ujuzi wake kama mpiganaji judo ulimletea heshima.

Katika miaka yake ya mwanzo chuoni wakati wa mwaka wake mdogo katika Jimbo la Leningrad, alishinda Master of Sport katika tuzo ya juu na alishinda tena miaka miwili baadaye.

Mambo mengi kuhusu maisha yake ya chuoni hayakujulikana, lakini kwa mujibu wa mmoja wa marafiki zake, Sergei Roldugin, Putin alianza kuonyesha aina ya utulivu inayotarajiwa kwa mtu anayependa kufanya kazi ya siri kama za ujasusi.

Mwaka 1975 Putin alijiunga na KGB na kupata mafunzo huko Okhta, Leningrad. Baada ya kufuzu, kazi yake kubwa ilikuwa ni kufuatilia nyendo za wageni na maofisa wa ubalozi huko Leningrad. Septemba 1984 alikwenda Moscow kwa mafunzo zaidi katika Taasisi ya Yuri Andropov Red Banner.

Baadaye alikwenda kufanya ujasusi huko New Zealand, ambako inadaiwa alikuwa akitumia majina tofauti na wakati mwingine akijifanya ni mfanyabiashara wa viatu vya bata katika miji ya Wellington na Auckland.

Mwishoni mwa mwaka 1984 alikwenda Dresden, Ujerumani Mashariki, kufanya kazi ya kijasusi huku akijifanya mkalimani. Alikaa huko hadi mwaka 1990.

Baada ya kushika nyadhifa nyingi mbalimbali, Jumamosi ya Julai 25, 1998 Rais Yeltsin alimteua Putin kuwa Mkurugenzi wa Shirika Kuu la Kijasusi na Usalama la Shirikisho la Urusi (FSB) lililorithi kazi zake kutoka KGB.

Jumatatu ya Agosti 9, 1999, Putin aliteuliwa kuwa mmoja wa naibu mawaziri waku watatu wa kwanza, na baadaye siku hiyo aliteuliwa na Rais Yeltsin kuwa kaimu waziri mkuu wa Serikali ya Shirikisho la Urusi. Siku hiyo hiyo Yeltsin pia alitangaza kwamba anataka Putin awe mrithi wake.

Ijumaa ya Desemba 31, 1999, Rais Yeltsin alijiuzulu bila kutarajiwa na, kulingana na Katiba ya Urusi, moja kwa moja Putin akawa Kaimu Rais wa Shirikisho la Urusi.

Wakati wapinzani wake wakijiandaa kwa uchaguzi wa Juni 2000, kujiuzulu kwa Yeltsin kulisababisha uchaguzi wa rais kufanyika mapema zaidi, Machi 26, 2000. Putin alishinda katika duru ya kwanza kwa asilimia 53 ya kura zote na kuapishwa Jumapili ya Mei 7, 2000.

Uchaguzi wa kumpata Rais wa nchi hiyo ulifanyika Jumapili ya Machi 26, 2000 ikiwa ni miezi mitatu kabla ya tarehe iliyokuwa imepangwa awali. Putin alishinda uchaguzi huo kwa asilimia 53 na kuapishwa Mei 7, 2000 kuwa Rais wa nchi hiyo.

Uchaguzi mwingine ulikuja Jumapili, Machi 14, 2004 Putin alichaguliwa kuwa Rais kwa muhula wa pili, akipata asilimia 71 ya kura.

Jumapili Machi 4, 2012, Putin alishinda uchaguzi wa Rais kwa mara ya tatu baada ya kupata asilimia 63.6 ya kura zote.

Ulipokuja uchaguzi mwingine wa Rais uliofanyika Jumapili ya Machi 18, 2018, Putin alishinda kwa zaidi ya asilimia 76 ya kura zote zilizopigwa. Muhula wake wa nne ulianza Jumatatu ya Mei 7, 2018, na utadumu madarakani hadi 2024.

Katika kipindi chote cha kuwapo madarakani, Putin amekuwa kama udhia kwa nchi za magharibi, hasa Marekani. Kwa muda mrefu Russia hajawa rafiki wa Marekani, na ziko sababu tatu za msingi. Hata hivyo, mzozo mkubwa kati ya Russia na nchi za Magharibi hivi sasa ni uvamizi wake Ukraine.

Kwa miezi kadhaa kabla ya uvamizi huo, Rais Putin alikuwa amekanusha kuwa angevamia Ukraine, lakini hatimaye alituma vikosi vya jeshi lake kuvuka mipaka ya kaskazini, mashariki na kusini mwa Ukraine.

Sasa anashutumiwa kwa kuvunja amani barani Ulaya na kitakachofuata kinaweza kuhatarisha muundo mzima wa usalama wa bara hilo. Viwanja vya ndege na makao makuu ya jeshi vilipigwa kwanza, karibu na miji kote Ukraine pamoja na uwanja mkuu wa ndege wa kimataifa wa Boryspil huko Kyiv.

Rais Putin mara kwa mara amekuwa akiishutumu Ukraine kwa kuchukuliwa na watu wenye itikadi kali, tangu Rais wake anayeiunga mkono Russia, Viktor Yanukovych, kuondolewa madarakani mwaka 2014 baada ya miezi kadhaa ya maandamano dhidi ya utawala wake.

Kisha Russia ililipiza kisasi kwa kuliteka eneo la kusini la Crimea na kuanzisha uasi mashariki mwa nchi hiyo, ikiunga mkono watu wanaotaka kujitenga ambao wamepigana na vikosi vya Ukraine katika vita vilivyogharimu maisha ya watu 14,000.

Mwishoni mwa 2021 alianza kupeleka idadi kubwa ya wanajeshi wa Russia karibu na mipaka ya Ukraine. Kisha mwishoni mwa Februari mwaka huu alitupilia mbali mkataba wa amani wa 2015 kwa upande wa mashariki na maeneo yaliyotambuliwa chini ya udhibiti wa waasi kuwa huru.

Urusi kwa muda mrefu imekuwa ikipinga hatua ya Ukraine kuelekea kujiunga Umoja wa Ulaya na muungano wa kijeshi wa kujihami wa nchi za Magharibi (Nato). Akitangaza uvamizi wa Russia, aliishutumu Nato kwa kutishia “mustakabali wetu wa kihistoria kama taifa.”

Russia imekataa kusema kama inataka kupindua Serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Ukraine, lakini wachambuzi wa mambo ya siasa za ulimwengu wanaona hivyo ndivyo itakavyokuwa.

Wachambuzi hao wanaona kuwa uvamizi wa Russia Ukraine unatishia amani na usalama wa bara la Ulaya na una madhara makubwa kwa nchi nyingine nyingi zinazopakana na Russia na Ukraine.

Kama ilivyosimuliwa katika mfululizo wa makala hizi, Rais Putin anasema kwa sehemu amechukua uamuzi wa kuivamia Ukraine kutokana na upanuzi wa Nato kuelekea mashariki. Hapo awali alilalamika kuwa Russia “haikuwa na mahali pengine pa kurudia - wanadhani tutakaa tu bila kufanya kitu?”

Ukraine bado ina nia ya kujiunga na Nato na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Ryabkov, alieleza: “Kwetu sisi ni lazima kabisa kuhakikisha Ukraine kamwe, kamwe haitakuwa mwanachama wa Nato.”

Katika macho ya Rais Putin, nchi za Magharibi ziliahidi mwaka 1990 kwamba Nato isingejipanua hata kwa “inchi moja kuelekea mashariki” lakini hawakutunza ahadi yao. Kwa maoni ya Putin, hiki ndicho kilichomsukuma hata akaivamia Ukraine.

Kwa kadiri hali ya mambo itakavyokwenda Russia na nchi za Magharibi, kwa kadiri atakapokuwapo Putin kama Rais wa Russia, uhusiano wa shaka utaendelea kuwapo kati ya Russia na nchi za Magharibi.