Ujenzi jengo PAPU wafikia asilimia 80, kutoa fursa ya ajira

Mwenyekiti wa Bodi TCRA, Dk Jones Killimbe (wa pili kutoka kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dk Jabiri Bakari (wa kwanza kushoto) wakipewa maelezo kuhusu maendeleo ya ujenzi wa  jengo la Makao Makuu ya PAPU jijini Arusha

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari amefanya ziara katika ujenzi wa jengo la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) linalojengwa jijini Arusha.

Kupitia jengo hilo anga la Arusha litabadilika pindi utakapokamilika ujenzi wa  jengo hilo refu kuliko yote katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, ambalo linajengwa kwa ubia  kati ya  Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Umoja wa Posta Afrika (PAPU). Jengo litatumika kama Makao Makuu ya PAPU. 

Taarifa ya maendeleo ya Ujenzi wa jengo hilo iliyotolewa wakati wa ziara ya Bodi ya Wakurugenzi ya TCRA kwenye mradi huo mwishoni mwa wiki iliyopita inaonyesha kuwa, ujenzi wa jengo hilo la ghorofa 19 umefikia asilimia 80.

Bodi ya TCRA ikiongozwa na Mwenyekiti wake Dk Jones Killimbe alieambatana na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dk Jabiri  Bakari ilifanya ziara kwenye jingo hilo ili kujiridhisha na maendeleo ya ujenzi wake.

Jengo hilo litakuwa na  huduma mbalimbali zikiwemo ofisi, maeneo ya biashara aina mbalimbali za kiwango cha Kimataifa, ukumbi wa kisasa, wenye viti vya kuhamishika kwa mfumo wa umeme na hoteli  yenye hadhi ya utalii wa kimataifa linararajiwa kutoa ajira na fursa nyingi kwa mamia ya wakazi wa Arusha na mikoa Jirani.

Sifa nyingine ya jengo hilo  ni kuwa mifumo mingi kwenye jengo hilo  itathibitiwa kwa mifumo ya kielektroniki itakayowezesha utoaji wa huduma kwa haraka na ubora wa viwango vya juu.

Ujenzi wa ghorofa hilo ni sehemu ya mkakati wa PAPU kujitegemea kiuchumi katika uendeshaji, badala ya kutegemea michango ya kila mwaka ya nchi wanachama.

PAPU ilianzishwa mwaka 1980, kwa mchango mkubwa wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere chini ya uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambao SASA unajulikana Umoja wa Afrika (AU). PAPU ni Taasisi ya kushughulikia masuala ya huduma za Posta Barani Afrika, ambapo, mkutano ulioanzisha ulifanyika Arusha hapa nchini.