Ujenzi kituo cha afya Uzi kunufaisha wakazi 3,800

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah akipanda mti wakati wa uzinduzi kituo cha afya Uzi, Mkoa wa Kusini Unguja kilichojengwa na Tasaf

Muktasari:

  • Wakazi wa Shehia ya Uzi na Ng'ambwa sasa hawatalazimika kuvuka mkondo wa bahari kufuata baadhi ya huduma za afya baada ya kukamilika kwa kituo chao cha afya.

Dar es Salaam. Wakazi wa Shehia ya Uzi na Ng'ambwa, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar sasa hawatalazimika kuvuka mkondo wa bahari kufuata baadhi ya huduma za katika eneo lingine, baada ya kukamilika kwa Kituo cha Afya Uzi.

Kituo hicho kilichowekewa huduma mbalimbali ambazo hazikuwapo awali, kimejengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) huku kikigharimu Sh360.8 milioni.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kituo hicho, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman  Abdullah leo Alhamisi Desemba 28, 2023, amesema kukamilika kwa kituo hicho kutarahisisha upatikanaji wa  huduma za afya kwa wakazi zaidi ya 3,800 wa Shehia za Uzi na Ng’ambwa.

Amesema wakati mwingine wananchi hao walikuwa wakishindwa kuzifikia huduma za afya kwa haraka hasa mkondo huo unapojaa maji. Mkondo huo ukijaa haukuzuia watembea kwa miguu pekee, bali hata vyombo vya moto ikiwemo magari yanashindwa kupita.

“Tasaf wamefanya kazi nzuri ya kujenga kituo hiki cha afya, sasa ni jukumu letu kukitunza ili kudumu kwa muda mrefu kwa ajili ya upatikanaji rahisi wa huduma za afya,” amesema Abdullah.

Kituo cha afya Uzi ambacho kimezinduliwa leo, kilianza kujengwa Septemba mwaka jana ikiwa ni moja ya sehemu ya shamrashamra za kusherehekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kilele chake  ni Januari 12, 2024.

Abdullah ametumia nafasi hiyo kuipongeza Tasaf kwa kujenga miundombinu hiyo muhimu ya afya kwa viwango stahiki.

 Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Mazrui na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais Sera , Uratibu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Hamza Hassan Juma wamesema kukamilika kwa kituo hicho kutaongeza idadi ya watu wanaopata huduma katika shehia hizo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Shedrack Mziray ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano mkubwa inaotoa katika kufanikisha utekelezaji wa shughuli za mpango wa kunusuru kaya maskini visiwani hapo.